1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Maoni ya wahariri wa magazeti

12 Februari 2007

Katika maoni yao leo,wahariri wa magazeti ya hapa nchini wanazungumzia juu ya hotuba kali aliyotoa rais Vladmir Putin wa Urusi kuilamumu Marekani kwa kuvuka mipaka katika sera zake za nje.

https://p.dw.com/p/CHTk

Rais Vladmir Putin ameilamu vikali Marekani kwa kuvuka mipaka katika kila namna kwa lengo la kulazimisha sera zake duniani kote.

Rais Putin alitumia maneno hayo makali katika hotuba aliyotoa kwenye mkutano wa kimataifa juu ya masuala ya usalama uliofanyika mwishoni mwa wiki katika mji wa Munic hapa nchini Ujerumani.

Juu ya lawama hizo kali za rais Putin, mhariri wa gazati la FRANKFURTER ALLGEMEINE anasema , katika demokrasia ya bwana Putin, siasa ya misuli inaenda sambamba na haja ya kutaka ushirikiano. Mhariri huyo anatilia maanani kuwa ni nguvu ya mafuta inayompa bwana Putin uhakika wa kijiamini pamoja na kutambua kwamba katika kutatua mizozo ya kimataifa Marekani pamoja na nchi za Ulaya zinaihitaji Urusi.

Gazeti la mjini Berlin NEUES DEUTSCHLAND linasema katika maoni yake kwamba kauli ya rais Putin inaakisi yanayozunguzwa na wapinzani wa siasa za rais Bush nchini Marekani kwenyewe.

Mhariri wa gazeti hilo anasisitiza kuwa sera za Marekani za kuzishurutisha nchi nyingine na kutaka kuwa na hodhi juu ya silaha pamoja na vita vya Irak zimesababisha vurumai duniani.

Mhariri wa gazeti la WIESBADENER KURIER anasemaa rais Putin ameikumbusha Marekani na madola mengine ya NATO kuwa Urusi bado ni taifa kubwa. Mhariri wa gazeti hilo anaeleza kuwa utakuwa uzembe kwa madola hayo kupuuza aliyosema rais huyo wa Urusi.

Gazeti linasema kuwa yumkini Urusi haina mawezekano makubwa katika kushiriki kikamilifu katika siasa za dunia lakini nchi hiyo ina uwezo wa kutibua na kuzuia maamuzi kadhaa.

Maamuzi juu ya kuiwekea Iran vikwazo, kutatua mgogoro wa Kosovo ama hatua yoyote haiwezi kuchukuliwa na baraza la usalama la Umoja wa mataifa dhidi ya Korea ya Kaskazini bila ya ridhaa ya Urusi.

Gazeti la STUTTGARETER linauliza iwapo rais Putin atarejea tena katika sauti ya ushirikiano baada ya kutoa kauli kali mwishoni mwa wiki iliyopita . Hatahivyo mhariri wa gazeti hilo anatilia maanani kwamba Urusi inahisi kuwa inatishiwa kutokana na mfungamano wa NATO kuendleea kujitandaza katika nchi za Ulaya ya mashariki.

Mhariri wa gazeti la WESTDEUTSCHE kutoka mji wa Düsseldorf pia anauliza, kwa nini rais Putin ametoa kauli hiyo ? Jee ametoa kauli hiyo kwa kuwa ana wasiwasi juu ya kuhatarishwaa amani ya dunia? Ama kwa sababu amefadhaika kuona kwamba nchi yake imewekwa mbele katika majina ya nchi zinazoongoza katika uovu wa rushwa?

Naye mhariri wa gazeti la MÄRKISCHE ALLGEMEINE ,kutoka mji wa Potsdam anasema hotuba ya rais Putin inakumbusha enzi za waziri mkuu wa Umoja wa Kisoviet Nikita Chruschtschow aliewahi kuvua kiatu na kupigapiga mezani kwenye mkutano wa baraza kuu la Umoja wa Mataifa mnamo mwaka wa 1960. Lakini hayo yalifanyika wakati wa kilele cha vita baridi baina ya mashariki na magharibi. Mhariri huyo anasema , kauli ya rais Putin ni ishara ya udhaifu.

Lakini mahariri wa gazeti la HELBRONNER STIMME anasema Marekani inapaswa kubadili sera zake za nje la sivyo mtazamo wa rais Putin utaungwa mkono na wapinzani wa siasa za Marekani ambao hapo awali hawakutiliwa maanani hata chembe.

Na ABDU MTULLYA.