1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Maoni ya wahariri wa magazeti

Abdu Said Mtullya22 Aprili 2010

Askofu Walter Mixa wa dayosis ya Augsburg amejiuzulu,wahariri watoa maoni yao.

https://p.dw.com/p/N2t0
Askofu Walter Mixa wa Dayosis ya Augsburg.Picha: apn

Sakata linalohusu kunyanyaswa na kuharibiwa  watoto wa kiume na makasisi  wa kanisa katoliki bado   linaendelea. Hapa nchini   Ujerumani askofu Walter Mixa amejing'atua.

 Wahariri wa magazeti wanatoa maoni yao juu ya askofu huyo.

Wahariri hao pia  wanazungumzia  juu ya udhaifu uliojitokeza katika  umoja wa nchi za Ulaya kufuatia janga lililosababishwa na mlipuko wa volkano,na vile vile wanatupia macho matukio ya kisiasa nchini Poland baada  ya kifo cha rais Kaczynski.

Magazeti karibu yote ya hapa  nchini leo yanatoa maoni juu ya kujizulu kwa askofu wa dayosisi  ya  Augsburg,  Walter Mixa kutokana na kashfa zinazoendelea kuliandama kanisa katoliki. Askofu huyo amejiuzulu baada ya kukiri kwamba alikuwa na mkono mwepesi katika kuwarudi watoto, yaani alikuwa  anawapiga watoto.

Mhariri wa gazeti la Heilbronner anasema hatimaye Askofu Walter Mixa ameng'atuka.Amefikia uamuzi huo baada  ya kutambua   kwamba ushahidi dhidi yake ulikuwa unaongezeka kila siku, juu ya kuwapiga watoto na juu ya kudokoa fedha kutoka kwenye mfuko wa  yatima.Mhariri wa gazeti la Heilbronner anasema majuto aliyoyaonyesha askofu huyo yalikuja aherini sana. Kwa  hiyo uamuzi wake wa  kujiuzulu ni ukombozi kwa kanisa katoliki ambalo kwa sasa linakabiliwa na mgogoro mkubwa.

Juu ya askofu huyo gazeti la Darmstädter Echo  linasema  kwa kadri alivyokuwa anaendelea  kung'ang'ania kiti, ndivyo alivyokuwa anazidi kuvuruga wajihi wa kanisa.

Na kanisa ndiyo nguzo ya mfumo wa maadili nchini  Ujerumani, anasema mhariri wa gazeti hilo la Darmstädter Echo.

Mhariri wa gazeti la Hessische/Niedersächsiche Allgemeine anasema askofu Mixa angeliweza kujiondoa kanisani kwa heshima ,lakini hakuitumia fursa  aliyokuwa nayo.

Mhariri huyo pia anasema alichofanya askofu huyo kinawakilisha kilele cha kile kinachoenda kinyume na imani ya waumini.


Magazeti ya Ujerumani leo pia yanazingatia masuala ya kimataifa ,kwa mfano juu ya mgogoro uliosababishwa na mlipuko wa volkano.

Mhariri wa gazeti la Neue Presse anasikitika kwamba Ulaya haikuzungumza na  sauti moja juu ya mgogoro  huo.Mhariri huyo anaeleza kwamba nchi za Ulaya bado  zipo mbali sana na umoja. Lakini mgogoro uliosababishwa na mlipuko  wa volkano umeonyesha  umuhimu wa kuwapo umoja  huo.Gazeti hilo linasema tofauti  zilizokuwapo juu  ya kukabilliana  na hatari ya volkano zimeonyesha  kuwa mgawanyiko unaweza  kuleta maafa.

Gazeti la Berliner Zeitung linatoa  maoni  juu ya Poland baada  ya kifo cha rais wa  nchi hiyo  Lech Kazcyinski.

Gazeti hilo  linasema,kufuatia kifo cha Kaczynski uchaguzi   utakaofanyika utaonyesha  iwapo mshindi-yaani rais  mpya- atayaunga mkono    mageuzi  yanayoletwa sasa na waziri mkuu .


Mwandishi/Mtullya Abdu/Deutsche Zeitungen/

Mhariri/Abdul-Rahman