1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Maoni ya wahariri wa magazeti

Abdu Said Mtullya2 Novemba 2010

Wahariri wa magazeti leo wanatoa maoni yao juu ya uchaguzi wa nchini Marekani.

https://p.dw.com/p/PwJ0
Rais Barack Obama katika heka heka za kampeni ya uchaguzi wa bunge.Picha: AP

Wahariri wa magazeti ya Ujerumani leo wanatoa maoni yao juu ya uchaguzi wa nchini Marekani ,na juu ya matokeo ya uchaguzi wa urais nchini Brazil Lakini pia wanazungumzia juu ya hatari ya ugaidi katika usafiri wa ndege.

Juu ya uchaguzi wa Marekani mhariri wa gazeti la Darmstädter Echo anasema uchaguzi huo unaonyesha mgogoro mkubwa unaowakabili wamarekani; ni uchaguzi unaoionyesha nchi iliyomo katika mteremko wa matatito makubwa kiasi cha kuwafanya wamarekani wasahau juu ya kile kinachoitwa ndoto ya Marekani. Ingawa watu katika sehemu nyingine za dunia wapo mbali na uchaguzi huo wanajiuliza jee, furaha ile kubwa ya hapo awali imeenda wapi, nderemo za kumshangilia Barack Obama?

Na mhariri wa gazeti la Schwäbische anauliza, wapo wapi wale waliosababisha matatizo hayo?Anajibu swali hilo kwa kueleza kwamba miaka miwili iliyopita wahafidhina wa Republican waliadhibiwa kwa kusababisha nakisi kubwa na kuacha miundombinu katika hali mbaya nchini. Na hasa waliadhibiwa kutokana na vita vya Irak .Lakini leo Republican wanajifanya kana kwamba hawana hatia juu ya matatizo yanayoikabili nchi. Na kutokana na hali ya kukata tamaa wapiga kura nchini Marekani hawana subira ya kusikiliza ufafanuzi wowote juu ya matatizo hayo. Wanamfuata yeyote yule anaehubiri chochote kile. Mhariri wa gazeti la Schwäbische anasema mambo yanaweza kubadilika haraka sana nchini Marekani.

Watu wa Brazil wamemchagua Rais wa kwanza mwanamke awaongoze,na wote wameridhika. Hayo anayasema mhariri wa gazeti la Financial Times Deutschland.Mhariri huyo anasema watu wa Brazil wameridhika na rais wao Lula amefurahi kwa sababu anaondoka madarakani baada ya kumsaidia mgombea wake Dilma Roussef kupata kura na kushinda.

Lakini pamoja na ushindi wa mwanasiasa huyo mwanamke, mhariri wa gazeti la Financial Times Deutschland anatahadharisha kwamba Brazil inahitaji kupiga hatua katika sekta ya malighafi. Inapaswa kuondokana na hali tegemezi sambamba na kuongeza thamani ya bidhaa inazoziuza nje.Mhariri huyo anasema haitoshi kwa bibi Dilma Roussef kuahidi tu kwamba atafanya vile vile kama rais Lula.

Rais mpya atapaswa kutambua kwamba nchi yake inahitaji wawekaji vitega uchumi na hasa katika sekta ya miundombinu.

Gazeti la Mittelbayerische linazungumzia juu ya hatari ya ugaidi katika usafiri wa ndege. Mhariri wa gazeti hilo anatoa maoni yake juu ya suala hilo kuhusiana na vifurushi vya mabomu vilivyopakiwa nchini Yemen.Mhariri wa gazeti hilo ameshtushwa na anauliza inakuaje kwamba abiria wanasumbuliwa sana wanapokaguliwa wakati vifurushi vinapakiwa katika ndege bila ya kuchunguzwa.

Ujanja wa kuficha mabomu katika vifurushi uling'amuliwa siku nyingi. Lakini inavyoelekea idara za usalama zimeipuuza hatari hiyo. Kwa hiyo sasa wakati idara hizo zinajaribu kutafuta njia za kuliziba pengo , akina Osama bin Laden watakuwa tayari wameshagundua ujanja mwingine wa kuwadhuru binadamu.

Mwandishi/Mtullya Abdu/Deutsche Zeitungen/

Mhariri/Othman Miraj/