1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Maoni ya wahariri

Abdu Said Mtullya16 Oktoba 2012

Wahariri hao leo pamoja na masuala mengine wanazungumzia juu ya mapambano ya hoja baina ya Rais Obama na mpinzani wake Mitt Romney.Na pia juu ya mkasa wa msichana wa Pakistan aliepigwa risasi na taliban.

https://p.dw.com/p/16Qfq
Rais Barack Obama.
Rais Barack Obama.Picha: Reuters

Mhariri wa gazeti la "Märkische Oderzeitung" anatoa maoni juu ya mdahalo baina ya Rais Obama na mpinzani wake Mitt Romney.

Mhariri wa gazeti hilo anasema Mitt Romney anajaribu kujitokeza kama mbadala halisi anaewakilisha mrengo wa kati .Amelegeza kamba juu ya madai yake kuhusu kodi na sera ya afya. Na pia amejiweka mbali na wafuasi wa mrengo wa kulia wa chama chake. Mhariri wa gazeti la "Märkische Oderzeitung" anasema hivi karibuni Romney alianza kuingia katika ulingo wa sera za nje. Amemshambulia Obama juu ya suala la Iran na pia amedai kwamba utawala wa Obama haukuweka ulinzi wa kutosha kwenye ubalozi wa Marekani mjini Benghazi.

Gazeti la"Neue Presse linatoa maoni juu ya msichana wa Pakistan aliepigwa risasi na Taliban kwa sababu ya kutetea haki ya wasichana ya kupata elimu. Gazeti hilo linaeleza kuwa mkasa wa msichana huyo unawafanya wasichana wengine waandamane barabarani, kana kwamba kushambuliwa kwa msichana huyo kumewafanya waondokane na uoga wa Taliban. Wanasiasa na viongozi wa kidini nchini Pakistan wamesimama pamoja na dada huyo. Ndiyo kusema Taliban wamejipiga risasi wenyewe....

Gazeti la "Wiesbadener Kurier"linatoa maoni juu ya vikwazo ambavyo Umoja wa Ulaya unakusudia kuviweka dhidi ya Iran. Mhariri wa gazeti hilo anasema kwa kadri vikwazo hivyo vitakavyoendelea kuwekwa na kuimarishwa ndivyo uwezekano wa kufanikiwa utakavyokuwa mkubwa. Sababu ni kwamba wananchi wa Iran wanaijadili sababu ya hali mbaya ya uchumi ambayo ni mpango wa nyuklia Watu wa Iran sasa wanaona kwamba hali ya uchumi wa nchi yao inazidi kuwa mbaya. Kwa hivyo Umoja wa Ulaya utafanya jambo la maana ikiwa utaviimarisha vikwazo dhidi ya Iran, kwani huo pia utakuwa ujumbe kwa Israel juu ya kutofanya pupa ya kutumia nguvu za kijeshi dhidi ya Iran.

Gazeti la "Handelsblatt" linawapongeza wanasayansi wawili waliotunukiwa nishani ya Nobel ya uchumi.Gazeti hilo linautilia maanani mchango walioutoa wanasayansi hao katika kuwasaidia watu wenye maradhi ya figo.

Mhariri wa gazeti la "Handelsblatt" anasema wataalamu hao waliotunukiwa nishani ya Nobel ya uchumi,Alvin Roth na Lloyd Shapley wametoa mchango mkubwa katika juhudi za kuwasaidia watu wenye matatizo ya mafigo. Kutokana na vigezo walivyovifafanua imewezekana kurahisisha utaratibu wa kuwapatia wagonjwa, mafigo yaliyotolewa na watu wengine bila ya kulipa chochote. Kwa njia hiyo wameyaokoa maisha ya binadamu wengi.


Waziri mwengine wa Ujerumani anakabiliwa na tuhuma za kunakili kazi za watu wengine katika tasnifu yake. Waziri huyo ni wa elimu na utafiti Annette Shavan. Juu ya tuhuma hizo mhariri wa gazeti la "Heilbronner Stimme" anasema Kansela wa Ujerumani Angela Merkel amesimama kidete kumtetea waziri huyo .Lakini gazeti la "Heilbronner Stimme" linakumbusha kwamba Kansela Merkel pia alijaribu kumtetea aliekuwa Waziri wa ulinzi,Karl Theodor zu Gutenberg ambae pia alikabiliwa na kashfa ya kughushi tasnifu. Mhariri wa gazeti hilo anakumbusha kwamba baada ya muda fulani Merkel alimwachia zu Gutenberg aanguke.! Hatahivyo mhariri wa gazeti la "Beliner Zeitung " anasena waziri Schavan anayo haki ya kutokuwa na hatia kwa sasa, mpaka hapo itakapothibitika kuwa ametenda kosa.

Mwandishi:Mtullya abdu /Deutsche Zeitungen.

Mhariri: Yusuf Saumu