1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Maoni ya wahariri

Abdu Said Mtullya14 Novemba 2012

Wahariri wa magazeti wanataoa maoni juu ya Ugiriki,bajeti ya Umoja wa Ulaya na uwezekano wa kukipiga marufuku chama cha mafashisti mamboleo nchini Ujerumani, NDP

https://p.dw.com/p/16iy1
Waziri wa fedha wa Ujerumani Wolfgang Schäuble.
Waziri wa fedha wa Ujerumani Wolfgang SchäublePicha: AP

 Gazeti la "Reutlinger General Anzeiger" linazungumzia juu ya bajeti ya Umoja  wa Ulaya. Mhariri wa gazeti hilo anasema Umoja wa Ulaya unakabiliwa na   changamoto kubwa zaidi kuliko ilivyodhaniwa hapo awali.

Wiki ijayo viongozi wa jumuiya hiyo wataijadili bajeti ya kipindi cha miaka saba kuanzia mwaka wa 2014 itakayofikia kiasi cha Euro Trilioni moja.  
Mhariri wa gazeti la "Reutlinger General Anzeiger "anasema ni lazima mapatano yafikiwe juu ya bajeti hiyo. Lakini anasema tayari inaonekana wazi kwamba Waziri Mkuu wa Uingereza,David Cameron, hatakuwamo katika masafa sawa na viongozi wengine. Mhariri huyo anakumbusha kwamba mnamo mwaka wa 1984, aliekuwa Waziri Mkuu wa Uingereza wa wakati huo Margareth Thatcher pia alidai  kurudushiwa fedha. Kwa hivyo ni jadi kwa Waingereza kuyazuia maamuzi juu ya bajeti ya Umoja wa Ulaya.

Gazeti la "Süddeutsche" linatoa maoni juu ya uamuzi wa Mawaziri wa fedha wa nchi za Umoja wa Euro. Mhariri wa gazeti hilo anasema ni uamuzi wa busara kwa mawaziri hao kuipa Ugiriki muda wa miaka miwili  zaidi ili iweze kulipunguza deni lake. Ni sahihi  kabisa kuisaidia Ugiriki ili iweze kuelekea katika njia sahihi.Kila mmoja anatambua kwamba kuanguka kwa Ugiriki kutaziathiri nchi nyingine. Swali la kuuliza ni jee nani atafuata ikiwa Ugiriki itaangukia nje ya Umoja wa sarafu ya Euro?Ni Ureno, Uhispania au nani?

Naye mhariri wa gazeti la "Westdeutsche" anasema ili kuiokoa Ugiriki,Ujerumani italipa.Lakini swali,ni kwa kiasi gani Ujerumani italipa.? Mhariri huyo anasema Ujerumani: Kufilisika kwa mwanachama mmojapo wa Umoja wa sarafu ya Euro kutakuwa na madhara kwa wanachama wengine. Ni bora kufumba macho na kuling'oa jino bovu, na kustahimili maumivu ya mara moja, kuliko kuendelea kuwa na maumivu kwa muda wote.

Jee ni sawa kuwapiga marufuku mafashishti mamboleo na chama chao cha National Democratic nchini Ujerumani?. Mhariri wa gazeti la "Neue Presse"  anasema hilo lingepasa kuwa suluhisho la pili.Mhariri huyo anaeleza kwamba kutumia njia za kisheria kukipiga marufuku chama cha mafashishsti mamboleo cha National Democratic nchini Ujerumani hakupaswi kuwa chaguo la kwanza. Jambo muhimu la kwanza kabisa ni kuuonyesha msimamo wa kidemokrasia. Ni lazima  wakati wote kuwakabili "Manazi" ili kuhakikisha kwamba watu hao hawaachiwi  barabara ili waweze kufanya maandamano.Lazima kuwakabili kwa uthabiti wote. Kama jinsi wananchi wa mji wa Frankfurt/oder walivyoonyesha mwishoni mwa wiki iliyopita.

Mwandishi:Mtullya  abdu/Deutsche Zeitungen:

Mhariri:  Yusuf Saumu