1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Maoni ya wahariri

Abdu Said Mtullya3 Septemba 2013

Maoni ya wahariri wa magazeti juu ya mgogoro wa Syria na juu ya matatizo ya Ugiriki katika muktadha wa uchaguzi wa Ujerumani.

https://p.dw.com/p/19aep
Kansela wa Ujerumani Angela Merkel
Kansela wa Ujerumani Angela MerkelPicha: picture-alliance/dpa

Gazeti la "Stuttgarter Nachrichten" linatoa maoni juu ya mgogoro wa Syria, wakati ambapo Rais Obama anasubiri uamuzi wa bunge iwapo achukue hatua za kijeshi dhidi ya utawala wa Assad au la. Jee Kansela Angela Merkel anaweza kusaidia?

Mhariri wa gazeti hilo anasema ni kweli kwamba Kansela Merkel hawezi kulishawishi bunge la Marekani kwa namna yoyote ,lakini anaweza kumsaidia Rais Obama kupita njia nyingine. Na kwa hakika inapasa Merkel afanye hivyo haraka, kwani mkutano wa nchi za G 20 utakaofanyika wiki hii unatoa fursa ya kufikiria upya, yaani Rais Obama aubadilishe msimamo wa kuishambulia Syria bila ya kuwa na aibu usoni.

Mhariri wa gazeti la "Neue Osnabrücker" pia anatoa mwito kwa Rais Obama wa kuweka mbele busara. Mhariri huyo anasema: Rais Obama anapaswa kurejea katika busara kwa sababu alifanya pupa katika kufikiria juu ya kuchukua hatua za kijeshi ili kuuadhibu utawala wa Assad. Ingelikuwa bora kwake kurudi nyuma katika uamuzi wa kuchukua hatua za kijeshi, kuliko kuchagua hatari ya kuyapeleka majeshi yake vitani. Ni kutokana na uamuzi wa wabunge wa Uingereza kwamba nchi za Ulaya zimeepuka kuingia katika mtego ambapo zisingekuwa na njia ya kujinasua

Obama abakia peke yake:
Mhariri wa gazeti la"Neue Osnabrücker"anasema, pia ni jambo zuri kwamba mfungamano wa kijeshi wa NATO nao pia umeamua kujiweka kando na mpango wa kuishambulia Syria.Sasa Obama amebakia peke yake.Lakini ni bora kutamauka kwa Rais huyo, kuliko kutumbukia kwa askari katika janga la vita.Kwani nchi za magharibi zinataka nini? Kuangushwa kwa Assad na kutoa nafasi kwa waislamu wenye itikadi kali nchini Syria?

Uamuzi wa pupa wa Rais Hollande:

Gazeti la"Frankfurter Allgemeine" linauzingatia uamuzi wa pupa wa Rais Hollande wa Ufaransa wa kuunga mkono mpango wa kuishambulia Syria.Gazeti hilo linaeleza kuwa Rais Hollande analaumiwa kwa kuchelewa kuyapitisha maamuzi na kwamba anajaribu hadi dakika za mwisho kufikia mwafaka. Lakini anapofanya uamuzi wa haraka, unakuwa ni wa makosa.Amepitisha uamuzi wa haraka kuuunga mkono mpango wa kuishambulia Syria.Lakini kadri hatua za kuishambulia Syria zinavyochelewa ndivyo mashaka yanavyozidi kuwa makubwa nchini mwake. Kilichodhaniwa kitaleta ushindi, sasa kimegeuka kuwa tatizo kubwa.

Kauli ya Waziri Schäuble juu ya Ugiriki:

Na sasa tugeukie katika mgogoro wa madeni nchini Ugiriki,katika muktadha wa kauli iliyotolewa na Waziri wa fedha wa Ujerumani Wolfgang Schäuble.Waziri huyo amesema huenda Ugiriki ikahitaji msaada mwingine. Juu ya kauli hiyo gazeti la "Nordwest" linasema wapinzani nchini Ujerumani wanasema serikali ya Kansela Merkel inaficha ukweli, kwa kutoa taarifa nusu nusu juu ya gharama za kuisaidia Ugiriki. Kauli ya Schäuble imewatia wasi wasi wapiga kura wanaomuunga mkono Merkel ambao,tokea hapo awali nyoyo zinawadunda juu ya gharama za kuisaidia Ugiriki.Na kwa hivyo ikiwa chama cha wapinga Euro-kinachoitwa, chama mbadala cha Ujerumani, kitaingia bungeni, basi chama hicho kitapaswa kitoe shukurani kwa Waziri Schäuble.

Mwandishi:Mtullya Abdu/Deutsche Zeitungen:

Mhariri:Yusuf Saumu