1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Maoni ya wahariri

Abdu Said Mtullya18 Juni 2014

Wahariri wa magazeti wanatoa maoni juu ya Iraq na kutekwa nyara vijana watatu wa Kiisraeli.Wahariri hao pia wanaizungumzia ziara ya Waziri wa ulinzi wa Ujerumani nchini Marekani

https://p.dw.com/p/1CL4L
Waziri wa ulinzi wa Ujerumani Ursula von der Leyen
Waziri wa ulinzi wa Ujerumani Ursula von der LeyenPicha: picture-alliance/dpa

Mhariri wa gazeti la "Rheinische Post" anaizungumzia hali ya nchini Iraq. Mhariri huyo anazungumzia juu ya makosa yaliyofanywa na Marekani kama kiini cha mgogoro unaoendelea sasa nchini humo.Anasema Marekani sasa inarudi tena nchini Iraq kwa kuutumia msemo adui wa adui yangu ni rafiki yangu.

Matokeo yake ,sasa Marekani inajenga mfungamano na Iran. Hata hivyo,mhariri wa gazeti la "Rheinische Post" anakiri kwamba Marekani haina njia nyingine,sasa ila kusikilizana na Iran. Lakini anashauri kwamba Marekani inapaswa kuutathmini ushirikiano wake na Iran katika msingi wa kuitambua hali halisi.

Mhariri wa gazeti la "Rheinische Post" anasema makosa yaliyofanywa na utawala wa Bush nchini Iraq sasa yanaonekana wazi. Lakini inaishauri Marekani ifikirie kuzihusisha Uturuki,Israel na hata Wakurdi.

Gazeti la "Thüringische Landeszeitung" pia linauzungumzia mgogoro wa Iraq. Linasema hatua kwa hatua Rais Obama atafika mahala ambapo atapaswa apitishe uamuzi juu ya hali ya nchini Iraq, hata ukiwa mgumu.Wapiganaji wenye itikadi kali kutoka duniani kote, hawatagwaya mbele ya kikosi cha askari 275 ambacho Marekani inakipeleka Irak.

Vijana wa kiyahudi watekwa nyara

Gazeti la "die tageszeitung" linazungumzia juu ya kutekwa nyara vijana watatu wa Kiisraeli. Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu anadai kwamba vijana hao wametekwa nyara na Hamas. Juu ya madai hayo gazeti la "die tageszeitung" linasema Waziri Mkuu Netanyahu amemlaumu kila mtu na kila upande.

Netanyahu amesema mkataba uliotiwa saini baina ya Rais Mahmoud Abbas na Hamas juu ya kuunda serikali ya Umoja wa Kitaifa ndiyo sababu ya kutekwa nyara vijana hao watatu. Ameulaumu Umoja wa Ulaya,ameilaumu Marekani kwa kushirikiana na Wapalestina na amemlaumu kila mtu ila yeye mwenyewe. Netanyahu anautumia mkasa wa vijana hao watatu kwa shabaha zake za kisiasa.

Ujerumani kuwa polisi mdogo wa dunia?

Waziri wa ulinzi wa Ujerumani Ursula von der Leyen anatarajia kufanya ziara nchini Marekani wakati ambapo Marekani yenyewe imeanza kuutua mzigo wa kuwa polisi wa dunia. Gazeti la "Nürnberger" linaitilia maanani ziara hiyo kwa kusema kwamba ziara hiyo ni kizungumkuti.

Wakati ambapo Marekani inarudi nyuma katika kulitekeleza jukumu la kuwa polisi wa dunia,Ujerumani inataka kuwa polisi mdogo wa dunia, lakini bila ya kutambuliwa na yeyote. Mpaka sasa dhima hiyo haijatiliwa maanani na Marekani licha ya kauli iliyotolewa na Rais wa Ujerumani juu ya kuitaka Ujerumani ishiriki kwa uthabiti zaidi katika juhudi za kuitatua migogoro ya dunia ,pia kijeshi.Ziara ya Waziri Ursula von der Leyen huko Washington haitaubadilisha msimamo wa Marekani.

Mwandishi:Mtullya Abdu/Deutsche Zeitungen.

Mhariri:Yusuf Saumu