1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Maoni ya wahariri

Admin.WagnerD5 Machi 2015

Wahariri wa magazeti wanazungumzia juu ya ubaguzi wa rangi nchini Marekani na juu ya uamuzi wa China kuongeza bajeti yake ya ulinzi. Pia wanatoa maoni juu ya shughuli za mashirika ya ujasusi

https://p.dw.com/p/1EmHF
Maandamano ya kupinga kuuliwa watu weusi na polisi nchini Marekani
Maandamano ya kupinga kuuliwa watu weusi na polisi nchini MarekaniPicha: picture-alliance/AP Photo/J. L. Magana

Mhariri wa gazeti la "Berliner Zeitung" anakumbusha kwamba zaidi ya karne moja iliyopita,Marekani ilitangaza rasmi kuondolewa uovu wa ubaguzi wa rangi nchini humo. Lakini mhariri huyo anasema uovu huo bado unaendelezwa na polisi wa nchi hiyo kwa kiwango cha kushtusha.

Mhariri wa gazeti la "Berliner " anasisitiza kwamba, kwa bahati mbaya, huo ndio ukweli juu ya Marekani.Polisi wengi, nchini humo, wanahisi kuwamo vitani dhidi ya watu wao wenyewe .Gazeti la "Berliner" linatilia maanani kwamba polisi nchini Marekani wanashamirishwa kwa silaha kupita kiasi, lakini hawalipwi vizuri.

Mafunzo mazuri kwa polisi ndilo suluhisho

Agahalabui polisi hawajui la kufanya wanapokuwamo katika hali ambapo busara ya kuepusha matumizi ya nguvu, ingelihitajika. Mhariri wa gazeti la "Berliner" anashauri kwamba mafunzo mazuri kwa polisi yangelisaidia sana nchini Marekani.

USA Ferguson PK Attorney General Eric Holder
Mwanasheria Mkuu wa Marekani Eric HolderPicha: Reuters/J.L. Duggan

China yaongeza bajeti ya ulinzi

Gazeti la "Die Glocke" linazungumzia juu ya uamuzi wa China wa kuongeza bajeti yake ya ulinzi. China imesema itaongeze bajeti hiyo kwa asilimia 10.1. Nchi hiyo imeeleza kwamba inahitaji kuongeza bajeti kwa manufaa ya jeshi lake lenye askari Milioni 2.3

Mhariri wa gazeti "Die Glocke" anasema uamuzi wa China juu ya kuongeza bajeti kwa ajili ya jeshi lake unaenda sambamba na sera yake ya tokea miaka mingi iliyopita. Lakini la kulitilia maanani ni kwamba, China inazidi kujiimarisha kijeshi barani Asia. Na kwa hivyo hautapita muda mrefu,mpaka hapo itakapofika siku ambapo dunia itakuwa inajiuma vidole, na kushika tama,wakati China inapandisha bendera yake kwenye visiwa vinavyosababisha mizozo baina nchi hiyo na jirani zake.

Majasusi wote ni sawa tu

Mhariri wa gazeti la "Süddeutsche" analiambia shirika la ujasusi la Ujerumani BND kwamba halina haja ya kulalamika juu ya mashirika mengine ya ujasusi ikiwa shirika hilo nalo,linavunja muamana baina yake na wananchi.

Mhariri huyo anasema mashirika ya ujasusi ya Marekani, Uingereza,China na Urusi siyo majahili wa pekee. Shirika la ujasusi la Ujerumani pia linadukiza sana .Raia wanaoishi katika nchi huru na ya kidemokrasia wanayo haki ya kuwa na imani na taasisi zao. Lakini shirika la ujasusi la Ujerumani, BND linakaribia kuuvunja muamana huo. Ikiwa halitafanya mageuzi,basi halitakuwa na haki ya kuyashutumu mashirika mengine,kama NSA la Marekani, kwa kufanya shuhguli za udukuzi.

Mwandishi:Mtullya Abdu/Deutsche Zeitungen.

Mhariri: Gakuba Daniel