1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

ubaguzi nchini Israel

5 Mei 2015

Wahariri wa magazeti leo wanatoa maoni juu ya maafa ya tetemeko la ardhi nchini Nepal,mgogoro wa nchini Yemen na juu ya kadhia ya ubaguzi wa rangi nchini Israel

https://p.dw.com/p/1FKJo
Misaada yamiminika Nepal
Msaada yamiminika NepalPicha: DW

Juu ya maafa ya tetemeko la ardhi nchini Nepal gazeti la "tageszeitung" linasema Nepal ni jamii iliyojengeka katika mfumo wa matabaka ya watu unaozingatia tofauti baina yao. Lakini licha ya tofauti hizo moyo wa mshikamano miongoni mwa watu umejitokeza katika nyakati hizi ngumu nchini humo . Mhariri wa gazeti la "tageszeitung" anatilia maanani kwamba jirani wanashirikiana katika malazi na chakula. Mhariri huyo anasema hiyo ni fursa nzuri ya kuziondoa tofauti za muda mrefu baina ya watu wa Nepal na kuijenga jamii mpya.

Gazeti la"Neues Deutschland" linazungumzia juu ya mgogoro wa nchini Yemen kuhusiana na madai kwamba majeshi yanayoongozwa na Saudi Arabia yametumia mabomu ya mtawanyiko kuwashambulia waasi . Mhariri wa gazeti hilo anasema hadi sasa hakuna yeyote alielalamika,siyo nchini Saudi Arabia wala nchini Marekani.

Usuhuba baina ya Marekani na watawala wa Saudi Arabia ni mfano unaothibitisha kwamba uhalifu wa kivita unatazamwa kwa macho tofauti na nchi za magharibi na hakuna kilichobadilika

Ubaguzi dhidi ya Waisraeli kutoka Ethiopia

Askari mmoja wa Israel mwenye nasaba ya Ethiopia alishambuliwa na polisi bila ya sababu yoyote. Ukanda wa video uliotolewa umeionyesha kadhia hiyo. Mhariri wa gazeti la "Süddeutsche" anasema pana hatari kubwa ya kutokea mgogoro nchini Israel na kwa hivyo viongozi wa nchi hiyo wanapaswa kuchukua hatua za haraka.

Mhariri huyo anatilia maanani kwamba kwa muda wa miaka mingi Waisrael wenye nasaba ya Ethiopia wamekuwa wanapambana na bughudha ya ubaguzi. Suala la kuwajumuisha katika jamii Waisraeli 135,000 wenye nasaba ya Ethiopia linapaswa kupewa kipaumbele katika ajenda za serikali mpya ya nchini Israel. Mhariri wa gazeti la "Süddeutsche" anasema jambo muhimu ni kuituliza hali ya ndani, kwani nje ya nchi, Israel inayo migogoro ya kutosha.

Shirika la ujasusi la Ujerumani matatani

Sakata la shirika la ujasusi la Ujerumani bado linaendelea.Sakata hilo linatokana na madai kwamba shirika hilo la Ujerumani, BND liliwapeleleza wanasiasa wa Ulaya na makampuni kwa niaba ya Marekani.

Gazeti la "Thüringer Allgemeine" linasema sasa kiongozi wa nchi, Kansela Angela Merkel hawezi tena kujiweka kando ya kashfa hiyo. Mhariri wa gazeti hilo anasema mambo yanatokota juu ya kashfa hiyo.

Makamu wa Kansela, Bwana Sigmar Gabriel ambae ia ni Mwenyekiti wa chama cha SPD amesema Kansela Merkel alimhakikishia kwamba ujasusi wa viwandani haukuwamo katika orodha ya shughuli za shirika la BND. Mhariri huyo anasema mambo hayajawahi kuwa ya moto,kisiasa kwa Kansela Merkel kama ilivyo sasa, kutokana na kashfa hiyo.

Mwandishi:Mtullya Abdu.Deutsche Zeitungen.

Mhariri:Josephat Charo