1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wakimbizi waendelea kuwasili Ulaya

Admin.WagnerD17 Juni 2015

Wahariri wanatoa maoni juu ya hukumu iliyotolewa na mahakama kuu ya Ulaya,kuunga mkono mpango wa Benki Kuu ya Ulaya wa kuzisaidia nchi zenye matatizo. Na pia wanatoa maoni juu ya sera ya Umoja wa Ulaya kuhusu wakimbizi

https://p.dw.com/p/1FiVf
Waziri wa fedha wa Ujerumani Wolfgang Schäuble na Rais wa Benki Kuu ya Ulaya Mario Draghi
Waziri wa fedha wa Ujerumani Wolfgang Schäuble na Rais wa Benki Kuu ya Ulaya Mario DraghiPicha: Dunand/AFP/Getty Images

Gazeti la "Nordwest" linazungumzia juu ya mgogoro wa wakimbizi miongoni mwa nchi za Umoja wa Ulaya. Mhariri wa gazeti hilo anasema licha ya nchi za Umoja wa Ulaya kujaribu kuonyesha ukali, wakimbizi wanaendelea kuja barani Ulaya. Na nchi za Umoja wa Ulaya zinazopakana na bahari ya Mediterania zinazidi kulemewa na mzigo wa wakimbizi hao.


Mhariri wa gazeti la "Nordwest" anatilia maanani kwamba katika heka heka za kuutafuta mkakati wa kukabiliana na wahalifu wanaowasafirisha wakimbizi hao, nchi za Umoja wa Ulaya zinasahau, kwamba wale wakimbizi ambao tayari wameshawasili barani Ulaya, wanahitaji kusaidiwa. Gazeti la"Münchner Merkur" linauzungumzia uamuzi wa Mahakama Kuu ya Ulaya wa kuunga mkono mpango wa Benki Kuu ya Ulaya wa kuzisaidia nchi zenye matatizo katika Ukanda wa sarafu ya Euro.

Mpango wa ECB waungwa mkono na mahakama

Mhariri wa gazeti hilo anaeleza kwamba hukumu ya Mahakama Kuu ya Ulaya ya kuunga mkono mpango wa Benki Kuu ya Ulaya, ECB, halikuwa jambo la kushangaza. Benki hiyo inanunua dhamana za serikali za nchi zenye matatizo makubwa ya madeni. Mhariri anasema lengo ni kuzisaidia nchi hizo. Hata hivyo uamuzi wa Mahakama ya Ulaya hautilii maanani kwamba Benki Kuu ya Ulaya inapaswa kuwa na mipaka katika kutoa misaada.

Gazeti la "Braunschweiger " linatoa maoni juu ya hukumu ya kifungo cha miaka mitatu, kwenye kituo cha mahabusi, iliyotolewa kwa kijana Sanel M aliepatikana na hatia ya kumuua mwanafunzi aliekuwa anawatetea watoto wawili kwenye mkahawa.Mwanafunzi huyo aliekuwa na umri wa miaka 22, Tugce Albayrak alikufa kutokana na kupigwa na kuanguka chini.

Mhariri wa gazeti la "Braunschweiger" anauliza jee ni sawa kwa kijana huyo,Sanel M kufungwa japo kwenye kituo cha mahabusi kwa muda wa miaka mitatu? Mhariri anasema hakuna jibu la swali hilo.Lakini anaeleza kwamba jambo moja ni wazi kabisa, kuwa baada ya miaka hiyo mitatu ,Sanel M atayaanza maisha yake upya. Lakini Tugce hatakuwa tena na fursa hiyo. Amekufa.

Mwandishi: Mtullya Abdu/Deutsche Zeitungen.

Mhariri: Mohammed Khelef