1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Maoni ya wahariri

9 Oktoba 2007

Mvutano ndani ya chama cha Social Demokratik –nchini Ujerumani unaendelea kushtadi. Mwenyekiti wa chama hicho bwana Kurt Beck na makamu wake Franz Münterfering wanaoneshana vidole . Katika maoni yao wahariri wa magazeti ya leo wanazungumzia hayo.

https://p.dw.com/p/C7lT

Gazeti la ABENDBLATT linasema yaelekea kana kwamba katika chama cha Sozial demokratik hakuna anaetaka kutambua kuwa enzi za kukifanya chama hicho kuwa cha kutoa hisani zimeshapita. Mhariri wa gazeti hilo anasema msimamo wa mwenyekiti wa chama hicho juu ya kutaka kufanya mageuzi katika sera za mageuzi unamdhoofisha makamu wake pamoja na watarajiwa wakubwa wa chama hicho , yaani waziri wa mambo ya nje Frank Walter Steinmeier na waziri wa fedha Peer Steinbrück.

Gazeti linasema chama cha SPD kinajaribu kupuuza mvutano uliopo,lakini baada ya mkutano wake mkuu majeraha yataanza kuonekana.

Na gazeti la mji wa Berlin Der TAGESSPIEGEL linaeleza kuwa makamu mwenyekiti Münterfering anatambua kwamba pendekezo la mwenyekiti wake hakika litakuwa na athari fulani.

Lakini makamu mwenyekiti huyo ni mtu muhimu kwa chama chake, na ana msimamo imara katika kupinga pendekezo la mwenyekiti wake.

Gazeti la FRANKFURTER ALLGEMEINE linaeleza kuwa umakamu wa bwana Münterfering unatokana na mizizi ya uenyekiti aliokuwa nao hapo awali katika chama chake.

Kwa hiyo akitaka kuendelea na mtazamo ule ule hana budi aonyeshe ishara thabiti kabla ya kufanyika mkutano mkuu wa chama. Lazima athibitishe kwamba anathamini kazi yake.


Mhariri wa gazeti la NORDBAYERISCHE KURIER anazungumzia juu ya kizungumkuti kilichopo katika siasa za Berlin.

Mhariri huyo anafafanua kwa kusema kwamba waziri wa chama cha Social demokratik anaungwa mkono na chama cha cha CDU lakini siyo na chama chake.

Na wakati huo huo yupo Kansela anaenyamaa kimya . Lakini gazeti linasema ,lazima Kansela huyo atambue kwamba mvutano uliopo ndani ya chama cha SPD unaweza kuiathiri serikali yake.

Sababu ni kuwa mwenyekiti wa chama cha SPD bwana Beck anadhamiria kuingia katika pambano ambapo ni upande mmoja tu utakaoshinda.

Beck anakiondoa chama chake kutoka kwenye njia ya mageuzi. Anataka chama chake hicho kiwe na mwelekeo mpya ima faima.

Gazeti linatabiri kuwa Chama chake kitamfuata na makamu wake Franz Münterfering atawekwa kando.

Na gazeti la NEUE RHEIN/NEUE RUHR ZEITUNG linakubaliana na hayo kwa kusema kwamba,kutokana na kutoweza kujitathmini yeye mwenyewe bwana Münterfing yumo katika mashua inayozama. Idadi kubwa ya wanachama wa SPD wanamwuunga mkono mwenyekiti wao bwana Kurt Beck.

AM.