1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Maoni ya wahariri

14 Juni 2007

Katika maoni yao wahariri wa magazeti karibu yote leo wanazungumzia juu ya vita vya wenyewe kwa wenyewe kwenye Ukanda wa Gaza.

https://p.dw.com/p/CHSh


Juu ya hali katika Ukanda wa Gaza gazeti la STUTTGARTER ZEITUNG linaeleza katika maoni yake kwamba mambo yameshaenda mrama kiasi kwamba hata jumuiya ya kimataifa haiwezi kufanya kitu chochote.

Mhariri wa gazeti hilo anasema kuwa uwezekano kwa jumuiya ya kimataifa kufanya lolote ni mdogo sana. Mhariri huyo anaeleza kuwa hata pendekezo la Israel juu ya kupeleka jeshi la kulinda amani ni jambo lisilowezekana.Gazeti linahoji kuwa hatua kama hiyo lazima ikubaliwe kwanza na pande zinazopigana yaani Hamas na Fatah.

Katika maoni yao baadhi ya wahariri wanaeleza wasi wasi mkubwa juu ya chama cha Hamas kuwa mtawala wa pekee katika Palestina. Gazeti la HAMBURGER ABENDBLATT pia limezungumzia hayo.

Gazeti hilo linaeleza kuwa lengo la chama cha Hamas ni kujenga dola ya kidini katika Palestina na kuleta utamalaki wa uislamu duniani kote. Mhariri wa gazeti hilo anatilia maanani mtazamo wa chama cha Hamas unaosema kuwa masuluhisho ya amani ni kinyume na misingi yake. Gazeti hilo linaona kuwapo kigezo mshabaha katika siasa ya Hamas ya kuua raia na yanayotokea nchini Irak kwa maelekezo ya magaidi wa Alkaida.

Mharriri wa gazeti la mjini DÜSSELDORF,HANDELSBLATT anaafikiana na tathmini hiyo katika maoni yake. Na anafafanua kwa kusema kwamba Ukanda wa Gaza unaweza kugeuka Irak nyingine.

Anasema mbali na kuyafanya maisha ya watu kuwa magumu katika Ukanda Gaza,wapalestina wenye siasa kali pia wanahatarisha usalama wa Israel, Misri na Jordan. Mhariri huyo anasema hatari hiyo inaweza kufika barani Ulaya vilevile.Na ndiyo sababu mhariri huyo anaunga mkono wazo la kupeleka jeshi la Umoja wa Ulaya kulinda amani kwenye Ukanda wa Gaza.

Lakini gazeti la THÜRINGER ALLGEMEINE halikubaliani na wazo hilo!Linasema kuwa jukumu la jeshi kama hilo litashindikana. Mhariri ametoa mfano wa matatizo yanayolikabili jeshi la kimataifa linalolinda amani nchini Lebanon.

AM.