1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Maoni ya wahariri

Abdu Mtulya13 Februari 2008

Leo wahariri wanazungumzia juu ya kuongeza fedha kwa ajili ya watoto

https://p.dw.com/p/D772
Waziri wa familia wa Ujerumani Ursula von LeyenPicha: picture-alliance/dpa

Vyama vikuu vilivyomo katika serikali ya mseto vinaelekea kwenye masikizano juu ya kuongeza pesa kwa ajili ya malezi ya watoto nchini Ujerumani.

Lakini katika maoni yao wahariri wa magazeti wanasema suala hilo linatumiwa kwa shabaha ya kampeni za uchaguzi.

Gazeti la LANDESZEITUNG linasema mvutano baina ya vyama vikuu vya serikali ya mseto juu ya kuongeza fedha kwa ajili ya watoto nchini Ujerumani ni njama za kujipatia kura zaidi badala ya kutatua tatizo. Mhariri wa gazeti hilo anasema vyama vya Social Democratic na Christian Democratic Union sasa vimekurupuka juu ya suala hilo kwa sababu ya kukihofia chama cha mlengo wa kushoto kinachoweka mkazo katika haki za kijamii katika sera zake.

Lakini gazeti la KIELER NACHRICHTEN , katika kuzungumzia suala la kuongeza fedha kwa ajili ya watoto linakumbusha juu ya deni la nchi.

Mhariri wa gazeti hilo anasema vyama vya SPD na CDU vinaponda fedha kana kwamba vimesahau kuwa serikali ya Ujerumani bado inadaiwa.Anasema njia sahihi ya kuwasaidia watoto ingelikuwa kuweka sawa bajeti ya nchi ili vizazi vijavyo visiwe na mzigo wa deni.

Mhariri wa gazeti la FRANKFURTER RUNDSCHAU anaunga mkono hoja hiyo kwa kusema , kuongeza posho kwa ajili ya watoto siyo sera ya kuwajibika.

Akifafanua hoja hiyo mhariri huyo anaeleza , kuwa vyama vikuu vya siasa nchini Ujerumani, vinashindana juu ya nani ni mwenye sera bora zaidi kwa manufaa ya familia.?

Gazeti linaeleza kuwa msimamo wa mwenyekiti wa chama cha Social Democratic, kuunga mkono nusu nusu, pendekezo la kuongeza posho kwa ajili ya watoto unaonesha jinsi chama chake kinavyokabiliwa na ugumu katika kurejesha tena umaarufu wake juu ya sera za kisasa kuhusu familia.

Likizungumza kwa ufupi juu ya mvutano wa vyama vikuu vya siasa juu ya suala la fedha kwa ajili ya watoto gazeti la THÜRINGER ALLGEMEINE linasema mvutano huo ni habari mbaya.

Na kutoka Düsseldorf mji mkuu wa jimbo la Northrhein Westphalia gazeti la HANDELSBLATT linavilaumu vyama vya SPD na CDU juu ya sera zao za familia.Gazeti linasema vyama hivyo vinacheza mchezo wa sungura na nungungunu: siku zote mmojawao anajaribu kufika kwenye manufaa kabla ya mwengine.

Hivi karibuni tu makamu wa chama cha SPD bwana Peer Steinbrück ambae pia ni waziri wa fedha alisema hataongeza pesa kwa ajili ya watoto, na badala yake fedha hizo zitatengwa kwa ajili ya malezi ya watoto kwenye sehemu za malezi. Gazeti linasema mtazamo huo ni sahihi kabisa, lakini uamuzi huo ni fursa kwa chama cha CDU kutembea kifua mbele na kujitapa kuwa chama chenye hisani kubwa kwa familia.