1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Magazeti ya Ujerumani.

Mtullya, Abdu Said21 Mei 2008

Mpango wa kuongeza mishahara ya wabunge wasimamishwa nchini Ujerumani!

https://p.dw.com/p/E3fU
Renate Künast. Wabunge wa Ujerumani hawatapata nyongeza za mishahara kwa sasa.Picha: picture-alliance/ dpa


Mpango  wa  kuongeza  mishahara ya wabunge nchini Ujerumani umeachiliwa mbali. Katika maoni yao  leo  wahariri wa magazeti ya hapa  nchini wanazungumzia  juu ya  uamuzi huo.

Wahariri hao  pia  wanazungumzia juu ya kushambuliwa na kuuliwa  wageni hasa waafrika, nchini Afrika kusini.


Juu ya uamuzi wa kuacha mpango wa kuongeza mishahara ya wabunge  gazeti la Neue Osnabrücke linasema  wabunge lazima  wazingatie maoni ya  wananchi. Kila mbunge anapaswa kuwajibika kwa wapiga kura wake- anapaswa kueleza kwa nini anastahili kuongezewa mshahara.


Gazeti hilo linaeleza  kuwa uamuzi wa kughairi mpango huo pia unatokana na kutambua kwamba wapo wananchi wengi wenye hali mbaya.

Lakini gazeti la Nürnberger Nachrichten linasema uamuzi huo unaonesha kwamba  bunge la   Ujerumani halina ujasiri. Gazeti linasema, ndio wabunge wanastahili  kulipwa vizuri lakini  waache tabia ya kuvuka  mipaka inapohusu kujihakikishia malipo ya  uzeeni.

Gazeti la Financial  Times Deutschland linasema katika maoni yake  kuwa  licha ya kuamua kuacha mpango wa kuwaongezea  wabunge  mishahara, wabunge  hao hawataweza  kukwepa shutuma za wananchi.Wananchi wanawaona  wabunge hao kuwa watu wenye uchu wa fedha.

Hatahivyo mhariri anasema  utaratibu wa wabunge kuongezewa mishahara kila baada  ya muda fulani bado upo palepale. Ndiyo sababu kuwa pana haja ya kutafuta njia nyingine.

Gazeti la Berliner Zeitung linazungumzia juu ya matukio ya kusikitisha nchini Afrika Kusini ambapo raia wa kigeni wanashambuliwa na kuuliwa.

 Gazeti hilo linasema  katika  maoni yake kuwa kufumuka kwa ukatili dhidi ya wageni siyo jambo la kushangaza. Gazeti linasema hali hiyo inatokana na msongamano wa matatizo ya muda mrefu nchini humo.

Mhariri anaeleza kuwa, uchumi wa nchi unastawi na kunawiri,lakini wananchi wengi hawaambulii kitu.

Kutokana na kutamauka, maalfu ya wazalendo wanaelekeza ghadhabu zao kwa wageni. Na gazeti la Döbelner Anzeige linasema ,kinachotokea Afrika Kusini ni aibu kubwa , hasa kwa kutambua kwamba ,kwa karne nyingi waafrika walikandamizwa chini ya mfumo wa kibaguzi -apartheid.