1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Magazetini.

Mtullya, Abdu Said24 Julai 2008

Magazeti ya Ujerumani leo yanazungumzia juu ya vitambulisho vipya na juu ya ziara ya seneta Barack Obama nchini Ujerumani.

https://p.dw.com/p/EizY
Waziri wa mambo ya ndani ya Ujerumani Wolfgang Schäuble.Picha: picture-alliance/ dpa


Wahariri wa magazeti ya Ujerumani leo wanazungumzia juu ya uamuzi wa serikali kuidhinisha utaratibu wa vitambulisho vipya. Lakini hawakumsahau Obama katika maoni yao.

Wajerumani wana wasi wasi juu ya kubanwa kwa maisha yao ya faragha kutokana na serikali kuidhinisha utaratibu wa vitambulisho vya alama za vidole. Waziri wa mambo ya ndani Wolfgang Schäuble anasema kuwa utaratibu huo utaimarisha usalama wa ndani. Lakini mhariri wa gazeti la Kieler Nachrichten anasema,madhal utaratibu huo utakuwa wa hiari,wahalifu hawatakubali vidole vyao vinakiliwe.

Gazeti la Dresdener Nueste Nachrichten pia linasisitiza katika maoni yake kuwa vitambulisho hivyo vipya havitaongeza usalama lakini vinafaa kujaribiwa.


Mhariri wa gazeti hilo anaeleza kuwa, tayari walinzi wa data wanatahadharisha juu ya vitambulisho hivyo vipya ambapo vidole vya wananchi vitanakiliwa katika mashine.

Waziri wa mambo ya ndani amesema haitakuwa rahisi kwa wahalifu kupachiza vitambulisho hivyo ,lakini gazeti linasema ,wahalifu wanatenda uhalifu popote pale wanapopata mwanya, na wala hawasubiri kusikia, kuwa jambo fulani haliwezekani.

Hatahivyo mhariri wa gazeti hilo anashauri kuwa utaratibu huo unafaa kutiliwa maanani katika nyakati hizi ambapo sehemu ,kubwa ya biashara inafanyika kwa njia za mashine.


Juu ya seneta Barack Obama gazeti la Bild Zeitung linasema mji wa Berlin ambapo Obama anatarajiwa kutoa hotuba yake upo katika heka heka-mithili ya kuwepo chini ya hali ya hatari. Mhariri anasema wajerumani nao wanatamani wangelikuwa na mwanasiasa kama huyo.Gazeti linasema mwanasiasa huyo ana haiba ya nguvu, tabasamu inayovutia, mtu huyo ni wa kupendeka tu.

Lakini,mhariri anasema Obama anataka kuwa rais wa Marekani. Maana yake ni kwamba ,akichaguliwa kuwa rais, atatetea maslahi ya Marekani hata pale ambapo mtazamo wa wajerumani utakuwa tofauti.

Gazeti la Märkische Allgemeine pia linasema kuwa pana sababu nyingi zinazomfanya Obama apendeke.

Mhariri anasema kwanza ni jambo la kuvutia kutambua kwamba Obama ni mtu mweusi wa kwanza anaeweza kuwa rais wa Marekani.Lakini awali ya yote, mwanasiasa huyo anawakilisha matumaini ya kujenga Marekani tofauti, hasa baada ya utawala rais Bush kuboronga mambo mengi.Lakini,pamoja na yotehayo ,lazima wajerumani wawe waangalifu.

Kwanza, Obama hajawa rais, na pili yeye siyo malaika.Obama amesema yes we can- kuwa tunaweza, ni msemo utakaopaswa kutekelezwa kwa matendo.

Gazeti la Münchner Merkur nalo linatilia maanani kuwa katika uchaguzi wa kugombea kiti cha rais nchini Marekani pana washindani wawili.Barack Obama na John McCain. lakini gazeti linasema washindani hao hawana tofauti kubwa baina yao.