1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Magazetini.

Mtullya, Abdu Said9 Septemba 2008

Katika maoni yao wahariri wa magazeti ya Ujerumani leo wanazungumzia juu ya mafanikio ya Umoja wa Ulaya katika mgogoro wa Georgia.

https://p.dw.com/p/FEa1
Rais Nicolas Sarkozy wa Ufaransa na rais Dmitry Medvedev wa Urusi.Picha: AP


Katika maoni yao wahariri wa magazeti ya Ujerumani leo wanazungumzia juu ya kinachoonekana kuwa mafanikio ya Umoja wa Ulaya katika mgogoro wa Georgia.

Wahariri hao pia wanazungumzia juu ya mabadiliko yaliyofanyika katika uongozi wa chama cha Social Demokratik kilichomo katika serikali ya mseto nchini Ujerumani.


Kuhusu juhudi za Umoja wa Ulaya katika kuutatua mgogoro wa Georgia gazeti la Flensburger Tageblatt linasema yawezekana kuwa mtu hapendi jinsi , Umoja huo unavyotekeleza sera zake za nje. Mambo mengi yamegangamaa kwenye makao makuu ya Umoja huo mjini Brussels; lakini licha ya hayo , gazeti linasema Umoja huo unafanya kazi. Mhariri anatilia maanani mafanikio ya jumuiya hiyo katika mgogoro wa Kaukasus. Ujumbe wa jumuiya hiyo umefanikiwa kuifanya Urusi ikubali kuondoa majeshi yake kutoka Georgia.


Mhariri wa gazeti la Dresdener Neueste Nachrichten anasisitiza hayo kwa kusema kuwa rais Dmitry Medvedev wa Urusi hakuwashushua wajumbe wa Umoja wa Ulaya kama jinsi ilivyohofiwa hapo awali.

Mhariri wa gazeti hilo anaeleza kuwa hayo yanatokana na siasa ya ustahimilivu ya Umoja wa Ulaya iliyoanzishwa hasa na Ufaransa pamoja na Ujerumani . Gazeti linatilia maanani ahadi iliyotolewa na rais Medvedev wa Urusi juu ya kuondoa majeshi ya nchi yake kutoka Georgia. Gazeti la Dresdener Neueste Nachrichten linasema dhima ya Umoja wa Ulaya katika kusuluhisha mgogoro wa Kaukasus imepata uzito wakati ambapo mishipa ya shingo imesimama mjini Moscow na Washington kutokana na kutoleana kauli kali.


Hatahivyo mhariri wa gazeti la Der neue Tag anasema ahadi ya rais Medvedev juu ya kuondoa majeshi yake haitoshi. Hatua zaidi zinalazimu kuchukuliwa ili kuweza kuleta amani.

Gazeti hilo linasema wajumbe 200 kutoka Umoja wa Ulaya watakaofuatilia utekelezaji wa hatua ya kuondolewa majeshi ya Urusi watapaswa pia kuenda katika majimbo ya Georgia, yaliyojitenga, ya Abkhazia na Ossetia kusini ili kuchunguza madai yanayotolewa na pande zote mbili juu ya mauaji ya kikabila.


Chama cha Social Demokratik ,SPD kilichomo katika serikali ya mseto nchini Ujerumani kimefanya mabadiliko ya uongozi.

Gazeti la Fränkischer Tag linasema mabadiliko hayo maana yake ni kwamba sera za mageuzi zilizoanzishwa na kansela wa hapo awali, Gerhard Schröder zitaendelea kutekelezwa.Gazeti linasema mageuzi hayo ni muhimu katika kuwasaidia watu wanaotambulika kuwa dhaifu kijamii.Lakini jambo muhimu pia ni kuwafanya watu watambue faida za mageuzi hayo.