1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Magazetini.

Mtullya, Abdu Said21 Oktoba 2008

Katika maoni yao ,wahariri wa magazeti ya Ujerumani leo wanazungmzia juu ya kuuliwa wanajeshi wawili wa nchi yao.

https://p.dw.com/p/Fe65
Waziri wa ulinzi Ujerumani Franz-Josef JungPicha: AP

Wanajeshi wawili wa Ujerumani wameuliwa nchini Afghanistan pamoja na watoto watano raia wa nchi hiyo.Wahariri wa magazeti karibu yote ya Ujerumani wanazungmzia shambulio hilo, katika maoni yao.

Shambulio hilo limetokea siku chache tu baada ya bunge la Ujerumani kupitisha uamuzi wa kuongeza idadi ya askari wake wanaolinda amani nchini Afghanistan. Na ndiyo sababu kwamba mhariri wa gazeti la Schwabische Zeitung anasema kuwa uamuzi huo ni sahihi. Anasema hatari inazidi kuwa kubwa nchini Afghanistan. Gazeti linaeleza kuwa wakiwa wengi, askari hao wataweza kujilinda vizuri zaidi wao wenyewe pamoja na wananchi.


Gazeti la Westfalenpost pia linazungumzia juu ya kuuliwa askari hao wawili wa Ujerumani. Linawaulumu mataliban kwa mauaji hayo. Linasema ugaidi wa mataliban unaelekezwa dhidi ya wote wale ,wanaofanya juhudi za kuijenga Afghanistan upya.

Gazeti linasema, katika chuki zao, mataliban hawapambanui baina ya wanajeshi na watoto wanaocheza ;lengo la mashambulio yao, gazeti linaeleza ni kulifanya jukumu la kulinda amani la jeshi la kimataifa kuwa halina maana yoyote na hivyo kuchochea mjadala juu ya kuondolewa kwa jeshi hilo. Lakini mhariri wa gazeti la Westfalenpost anasema jukumu hilo lazima liendelee kutekelezwa.

Lakini gazeti la Badische Neueste Nachrichten linatanabaisha juu ya matukio ya kusikitisha, ambapo mara kwa mara, raia wa Afghanistan wanauawa kutokana na mashambulio yanayofanywa na majeshi ya kimataifa.

Gazeti hilo linasema matukio hayo yanapalilia chuki. Linaeleza kuwa wanaejshi wa Ujerumani vilevile hawawezi kuepuka chuki hiyo. Mhariri wa gazeti la Badische Neueste Nachrichten anasema kilichobakia ni kutumai kwamba majeshi ya nchi za magharibi yanayolinda amani nchini Afghanistan yatafanikiwa kuwawezesha polisi na wanajeshi wa nchi hiyo kuchukua jukumu la kulinda usalama wa nchi yao.


Gazeti la Dresdener Neueste Nachrichten pia linasisitiza hayo kwa kusema kwamba ni lazima juhudi zifanyike ili watu wa Afghanistan waelewe sababu ya kuwepo majeshi ya kimataifa nchini mwao.

Na mhariri wa gazeti la Augsburger Allgemeine anatilia maanani kwamba watu zaidi na zaidi wanaendelea kujiunga na mataliban kutoka nchini Afghanistan na kutoka nje ya nchi hiyo.Fedha na silaha wanazoendelea kupata zinawaimarisha kiasi cha kuweza kuvuruga mafanikio yote ya jeshi la kimataifa.