1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Magazetini

Abdu Said Mtullya31 Machi 2009

Mkurugenzi wa kampuni ya reli ya Ujerumani ajiuzulu.Wahariri wa magazeti wanatoa maoni yao.

https://p.dw.com/p/HNYc
Mkurugenzi wa shirika la reli Hartmut Mehdorn aliejiuzulu.Picha: AP


Wahariri wa magazeti ya Ujerumani leo wanazungumzia juu ya kujiuzulu kwa mkurugenzi wa shirika la reli la Ujerumani bwana Hartmut Mehdorn kutokana na kashfa ya kuwapeleleza wafanyakazi.

Wahariri hao pia wanazungumzia juu ya kampuni ya Ujerumani ya Opel, yaani ndugu wa Generel Motors, inayokabiliwa na matatizo makubwa.

Kashfa ya kupeleleza wafanyakazi wake imemwangusha bwana Hartmut Mehdorn mkurugenzi wa kampuni ya reli ya Ujerumani.

Mkurugenzi huyo bwana Mehdorn alitangaza kujiuzulu jana kutokana na kashfa ya kudakiza mawasiliano ya barua pepe za wafanyakazi wa shirika lake.

Pia pamekuwapo madai kwamba shirika hilo lilikuwa linapeleleza data ,yaani habari juu ya waajiriwa wake.

Kuhusu kujiuzulu kwa bwana Mehdorn mhariri wa gazeti la Cellesche , anasifu kazi nzuri aliyofanya. Gazeti linamsifu kwa kulifanya shirika la reli la Ujerumani kuwa la kisasa na kuweza kuliorodhesha kwenye soko la hisa.

Gazeti hilo la Cellescshe linamwita bwana Mehdorn kuwa ni Napoleon wa reli.

Lakini yote hayo sasa yamefikia mwisho, anasema mhariri wa gazeti hilo.

Mhariri wa gazeti la Landeszeitung pia anasifu kazi nzuri aliyofanya mkurugenzi huo lakini anasema penye kapi pana usubi!

Mhariri anasema mkurugenzi huyo alikuwa anaamini kuwa wafanyakazi, fisadi na wale waliokuwa wana mwelekeo wa kugoma walipaswa kupigwa vita ili wasiwatie wasiwasi wawekaji vitega uchumi. Lakini msimamo huo pamoja na mwelekeo wake dhidi ya diplomasia umesababisha mwisho wa mkurugenzi huyo bwana Mehdorn.

Mhariri wa gazeti la Trierischer Volksfreund anazungumzia juu ya kiwanda cha magari cha Opel yaani kiwanda ndugu na, General Motors cha Marekani.Kiwanda cha Opel kwa sasa kinavuta pumzi ya faraja kutokana na kiwanda ndugu General Motors kupewa siku 60 na Ikulu ya Marekani ili kijirekebishe.

Juu ya hayo gazeti hilo, Trierischer Volksfreund linatilia maanani kwamba rais Obama hataiacha GM, ikate roho.

Lakini gazeti linasema kiwanda hicho pia kimebanwa, na ikiwa hapatatokea muujiza,kiwanda hicho hakitaponyoka muflisi.Hali hiyo itaathiri mustakabal wa kiwanda ndugu cha Ujerumani Opel, vilevile.Kwa hiyo ni mapema mno kwa Opel kufurahi sana.

Mhariri.M Abdulrahman.

Mwandishi.Mtullya Abdu.