1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Magazeti ya Ujerumani.

Abdu Said Mtullya16 Aprili 2009

Wahariri wa magazeti ya Ujerumani leo wanatoa a maoni yao juu ya uchaguzi wa India na juu ya mtuhumiwa John Demnjanjuk.

https://p.dw.com/p/HYJi
John Demnjanjuk akipelekwa mahakamani.Picha: picture-alliance/dpa

Wahariri wa magazeti ya Ujerumani leo wanamzungumzia aliekuwa mlinzi kwenye kambi ya mafashisti Demnjanjuk, anaetuhumiwa kuhusika na maangamizi ya wayahudi alfu 29.Wahariri hao pia wanatoa maoni yao juu ya uchaguzi wa India .

John Demnjanjuk alikuwa mlinzi kwenye kambi iliyotumiwa na mafashisti kuwatesa na kuwaangamiza wayahudi.Mtu huyo mwenye umri wa miaka 89 anadaiwa kuhusika na mauaji ya wayahudi alfu 29 waliokuwemo kwenye kambi hiyo wakati wa vita kuu vya pili. Sasa anatakiwa ajibu tuhuma hizo kwenye mahakama ya Ujerumani. Lakini anaishi Marekani. Uamuzi wa mahakama juu ya mtu huyo kuletwa Ujerumani umeahirishwa mara kadhaa nchini Marekani.

Juu ya hayo gazeti la Der neue Tag linasema nchi inayofuata sheria lazima ioneshe kwamba idara zake za uchunguzi zinafanya kazi bila ya dosari. Idara hizo zinapaswa kufanya kazi kama kamani ya saa.Mhariri wa gazeti hilo anasema hata kama miaka 66 imeshapita tokea wayahudi hao alfu 29 waangamizwe, lazima haki itendeke. Gazeti la Lausitzer pia linasisititiza kwamba waliohusika na maangamizi ya wayahudi wa Ulaya katika vita kuu vya pili lazima washughulikiwe kisheria kwa uthabiti wote.

Gazeti la Leipziger Volkszeitung leo linazungumzia juu ya uchaguzi mkuu utakayofanyika baadae mwaka huu hapa nchini Ujerumani.Mhariri wa gazeti hilo anasema ,anaetaka kuaminika na wapiga kura, atapaswa kuwa na mpango juu ya kudumisha nafasi za ajira, hasa wakati huu ambapo Ujerumani pia inakabiliwa na mgogoro mkubwa wa uchumi.

India inajivunia demokrasia yake , na wastahiki zaidi ya milioni mia saba wataonesha, ni kwa kiasi gani demokrasia hiyo ni imara? Gazeti la Augsuburger limeandika hayo katika ukurasa wake wa maoni juu uchaguzi wa India.Lakini mhariri wa gazeti hilo anatilia maanani zaidi umuhimu wa wastahiki hao katika kupiga kura itakayoshinda chuki dhidi ya waislamu zaidi ya milioni 170 nchini India. Gazeti linasema huo utakuwa mchango mkubwa katika kujenga uhusiano mzuri na jirani, Pakistan.Pia utakuwa mchango muhimu katika kuuzima moto unaoendelea kuwaka nchini Afghanistan.