1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Maoni ya wahariri

Sekione Kitojo3 Agosti 2009

Wahariri wa magazeti ya Ujerumani leo wamezungumzia zaidi sera za mgombea wa ukansela kwa chama cha SPD, Frank-Walter Steinmeier za kutengeneza nafasi milioni nne za kazi ifikapo 2020.

https://p.dw.com/p/J2be
Mgombea wa kiti cha ukansela kwa chama cha SPD Frank-Walter Steinmeier (katikati), akiteta jambo leo Jumatatu mwanzoni mwa mkutano wa chama mjini Berlin.Picha: picture-alliance/ dpa

Wahariri wa magazeti ya leo wamezungumzia zaidi kuhusiana na sera za mgombea wa chama cha SPD katika kiti cha ukansela Frank-Walter Steinmeier za kutengeneza nafasi za kazi milioni nne iwapo atachaguliwa, pia kuhusu matatizo ya wastaafu nchini Ujerumani .

Tukianza na gazeti la Leipziger Volkszeitung kuhusu mgombea wa kiti cha ukansela Frank-Walter Steinmeier , gazeti linaandika:

Nafasi milioni nne mpya za kazi , linauliza gazeti hilo, na kuongeza nani anahitaji zaidi. Kwa maelezo haya kuhusiana na suala la kazi chama cha Social Democratic kimeweza kuvitupa nyuma chama cha mrengo wa shoto cha Die Linke pamoja na kile cha ulinzi wa mazingira cha Die Grünen. Akitafuta mada ya kuingia nayo katika kinyang'anyiro cha kampeni ya uchaguzi mgombea wa chama cha SPD Frank-Walter Steinmeier ameweza kugusa pale ambapo wananchi wamekuwa na wasi wasi napo, tangu wakati wa kipindi cha mzozo wa kiuchumi.

Lakini gazeti hilo linasema anacheza na moto, iwapo wito wake huu hautachukuliwa kuwa kweli na wapiga kura kama ilivyo kwa mtazamo wa kupunguza kodi kutoka kwa serikali inayotawala ya mseto na Waliberali. Hata hivyo gazeti linasema kuwa hilo ni jukumu lake katika mapambano ya uchaguzi, katika kujitetea asianguke.

Steinmeier hana nafasi kabisa ya kuwa Kansela. Na bado zimebaki siku 55 tu kabla ya uchaguzi ambapo ataweza kuwa na uhakika iwapo anaweza kuwa kansela ama la. Gazeti linaongeza.

Kwa wakati huu katika chama chake kuna hali tofauti ya matumaini, kwamba wanataka kuchukua udhibiti wa serikali baada ya uchaguzi. Huenda pia chama cha SPD kinaweza kutaka kuongoza kwa kutumia mafungamano na vyama vya mrengo wa shoto.

Gazeti la Financial Times Deutschland kuhusu suala hilo limeandika:

nafasi za kazi milioni nne anataka mgombea wa chama cha SPD kutengeneza hadi ifikapo mwaka 2020. Hii inakumbusha ahadi zilizovunjika za wakati uliopita.Katika mwaka 1998 Gerhard Schröder alisema kuwa angepunguza ukosefu wa kazi kutoka nafasi milioni nne hadi 3.5. Lakini haikutokea.

Likitubadilishia mada gazeti la Nordwest-Zeitung linazungumzia kuhusu masuala ya wastaafu na kodi. Gazeti linaandika.

Wastaafu wa Ujerumani wako katika matatizo. Kuhusu hilo pia haraka kukatolewa maelezo kutoka katika wizara ya fedha kuwa hakuna haja ya kutaharuki. Hata hivyo ni lazima wizara ionyeshe iwapo tamko hilo linaweza kuleta hatua za ujenzi wa imani. Na ni muhimu kuweka hali ya uwazi na hatimaye kutoa taarifa kamili.

Nalo gazeti la Neue Osnabrücker kuhusu mada hiyo linaandika.

Je waziri wa fedha amepoteza mwelekeo? Wananchi wanafuata uamuzi wa mahakama ya katiba wa mwaka 2002 kuwa wastaafu na wanaopokea malipo ya uzeeni washughulikiwe kwa usawa. Kitu kinacholeta mzozo ni kuwa mafao yanayoongozeka ya wastaafu hutozwa kodi kwa kadiri ya ongezeko.

Hayo ndio maoni kwa leo ya wahariri wa magazeti ya Ujerumani kama mlivyokusanyiwa na Sekione Kitojo.

►◄

Mwandishi:Sekione Kitojo/Dt Zeitungen

Mhariri:M.Abdul-Rahman