1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Korea Kaskazini yahatarisha amani

Admin.WagnerD7 Januari 2016

Wahariri wanazungumzia juu ya jaribio la bomu la nyuklia lililofanywa na Korea Kaskazini.

https://p.dw.com/p/1HZdg
Kiongozi wa Korea Kim Jong Un
Kiongozi wa Korea Kim Jong UnPicha: picture-alliance/dpa

Mhariri wa gazeti la "Berliner" anasema kwa mara nyingine dikteta wa Korea Kaskazini Kim Jong Un anaiweka dunia roho juu.

Mhariri huyo anasema dikteta Kim hajatosheka na kuiendeleza jadi ya iliyoanzishwa na baba yake ya kufanya majaribo ya silaha za nyuklia; sasa Kim Jong Un anajiimarisha na bomu la nyuklia lenye nguvu kubwa zaidi la Hydrojeni.

Mhariri wa "Berliner Zeitung" anasema ingawa haijathibitishwa kwamba jaribio hilo lilikuwa la bomu la Hydrojeni,shabaha anayoilenga dikteta Kim Jong Un ,inaonekana wazi.

Gazeti la "Hannoversche Allgemeine" pia linatilia maanani kuwa ,hata ikiwa dikteta wa Korea Kaskazini amesema uongo, haitakuwa sahihi kupuuza ukweli,kwamba mtu huyo, ni katili na ,geugeu .

Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa lailaani Korea Kaskazini
Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa lailaani Korea KaskaziniPicha: picture-alliance/AP Photo/F. Franklin II

Mhariri wa gazeti hilo anashauri kwamba jumuiya ya kimataifa inapaswa kuwa makini juu ya hatari inayotokea Korea Kaskazini, sambamba na changamoto zinazotokana na migogoro iliyopo katika Mashariki ya Kati,Afrika na barani Ulaya. Pana hatari kwamba huenda siku moja, dikteta Kim kweli akazitumia silaha za nyuklia na kusababisha madhara makubwa, hata ikiwa siyo kwa bomu la Hydrojeni.

Silaha za nyuklia dhidi ya magharibi
Jaribio jipya la silaha za nyuklia lililofanwya na Korea Kaskazini ni mwendelezo wa sera ya utawala wa nchi hiyo ,kwamba itaweza kujihami dhidi ya mashambulio ya nchi za magharibi kwa silaha hizo. Mhariri wa "Nordwest Zeitung" anakubaliana na sera hiyo kwa kuuliza, jee Rais Bush angeliivamia Irak, laiti Saddam Hussein angelikuwa nazo silaha za nyuklia?

Lakini hiyo haina maana kwamba dikteta wa Korea Kaskazini aachiwe ukumbi wa kilisakata dansi apendavyo! Ni sahihi kabisa kuendelea kuitenga nchi hiyo,hatahivyo, juhudi za kuundoa utawala wa Kim zinapaswa kutokea ndani.

Mhariri wa "Märkische Oderzeitung" anasisitiza umuhimu wa China katika mgogoro mzima wa Korea Kaskazini. Mhariri huyo anasema China ndio nchi yenye uzito mkubwa wa kisiasa juu ya Korea Kaskazini. Ukweli ni kwamba vikwazo vyote vilivyowekwa na nchi za magharibi, pamoja na Umoja wa Mataifa, havijaleta tija hadi sasa. Korea kaskazini bado inaendelea na siasa ya ushari na vitisho.

Sasa ni juu ya mshirika mkuu wa nchi hiyo, yaani China, kuchukua hatua zinazostahili, ili kuepusha maafa,yawe ya kuanzishwa kwa bahati mbaya au kwa kudhamiria.!

Mwandishi: Mtullya Abdu. Deutsche Zeitungen

Mhariri: Mohammed Khelef