1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Maoni ya wahariri,juu ya Syria,Ugiriki na Napolitano

Abdu Said Mtullya23 Aprili 2013

Wahariri wanauzungumzia msimamo wa Ujerumani juu ya Syria,na pia wanatoa maoni juu ya kuchaguliwa tena kwa Rais wa Italia Napolitano.

https://p.dw.com/p/18LF1
Waziri wa mambo ya nje wa Ujerumani Guido Westerwelle
Waziri wa mambo ya nje wa Ujerumani Guido WesterwellePicha: Reuters

Gazeti la "Emder" linatoa juu ya uamuzi wa Ugiriki na Cyprus wa kuwapa vibali vya kuishi nchini wawekaji vitega uchumi ambao si raia wa Umoja  wa Ulaya.Serikali za nchi hizo zitatoa vibali hivyo kwa wafanyabiashara watakaonunua au kukodi mali katika sekta ya ujenzi thamani ya Euro zaidi ya laki mbili na nusu.Lengo la uamuzi huo ni kuifufua sekta ya ujenzi.

Juu ya uamuzi huo gazeti la"Emder" linasema ni vizuri kwamba serikali za nchi hizo zinajaribu kuwa na ubunifu katika juhudi za kupambana na mgogoro wa madeni. Hata hivyo gazeti la "Emder"linasema uamuzi huo unatoa picha kwamba yeyote mwenye fedha anaweza kuununua uraia wa Umoja wa Ulaya.Gazeti hilo linauliza jee sera hiyo itaipeleka wapi Ulaya? Nchi nyingine za Ulaya zinapaswa kuchukua hatua za haraka ili kuizuia sera hiyo

Silaha kwa wapinzani, Syria?

Umoja wa Ulaya umelegeza vikwazo dhidi ya Syria. Kulingana na uamuzi huo nchi za Umoja huo zitaruhusiwa kuyanunua mafuta ya Syria yanayodhibitiwa na wapinzani wa serikali. Lakini Uingereza na Ufaransa zinataka vikwazo vya silaha pia   viondolewe. Lakini Ujerumani inaupinga mtazamo huo.

Gazeti la "Straubinger Tagblatt" linatoa maoni juu ya msimamo huo wa Ujerumani kwa kusema kwamba msimamo huo ni sahihi hata ikiwa unaonekana kuwa siyo wa kiungwana.Sababu ni kwamba hakuna anaeweza kutoa uhakika kwamba silaha kutoka Ujerumani hazitatumika kwa ajili ya kupigania kuunda nchi ya itikadi kali ya   kiislamu. Uamuzi wa kulegeza vikwazo vya mafuta ni sahihi,kwa sababu vikwazo hivyo vimewaathiri zaidi wananchi kuliko utawala wa kidhalimu wa Hafez al.Assad. Na ili kuwasaidia wananchi wa Syria, kinachotakiwa ni maendeleo ya kiuchumi badala ya kuwapa mahema na mikate ya resheni.

Napolitano achaguliwa tena:

Gazeti la "Neue Osnabrücker "linatoa maoni juu ya kuchaguliwa tena kwa Giorgio Napolitano kuwa Rais wa  Italia.Mhariri  wa gazeti hilo anasema kuchaguliwa tena kwa Napolitano kuwa Rais wa Italia kunathibitisha adhma na hisia za kuwajibika za kiongozi huyo mwenye umri wa miaka 87.Ni jambo la hakika kwamba Italia ingelikuwa na uwezo wa kuyatatua matatizo mengi,  laiti pengekuwapo watu  wengi kama Napolitano.Lakini kwa bahati  mbaya watu kama yeye hawapo. Na badala yake vipo vyama vya kisiasa vinavyokingamana,kuchafuliana sifa na kushikilia upinzani. Mhariri wa gazeti la "Neue Osnabrücker" amesema kwa mambo hayo mtu anagonga  vichwa vya habari, lakini hajengi  nchi.

Mwandishi:Mtullya Abdu /Deutsche Zeitungen.

Mhariri:Mohammed Abdul-Rahman