1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Maoni:Msiba wa Lampeduza-Ulaya iwajibike

4 Oktoba 2013

Badala ya kuwafungia milango wakimbizi wanaokimbia shida na maafa,Ulaya ingebidi isaidie kwa dhati kupambana na sababu zinazowafanya watu kuyapa kisogo maskani yao

https://p.dw.com/p/19teM
Mkuu wa Idhaa ya kiswahili ya DW, Andrea SchmidtPicha: DW

Msiba mkubwa karibu na fukwe za Lampeduza ni ushahidi wa kushindwa nchi za Ulaya.Vifo vya watu wasiokuwa na hatia katika bahari ya kati lazma visitishwe haraka.Hakuna anaeipa kisogo nchi yake kama si kutokana na shida na kujitupa mikononi mwa magengi ya wanaosafirisha watu kinyume na sheria.Maelfu wamepita katika njia hiyo ya hatari miaka iliyopita wakijaribu kuingia Ulaya,kwasababu njia halali zimefungwa.Wakimbizi wanayatosa maisha yao katika mashua zisizo salama bila ya chakula wala maji ili kuyapa kisogo maeneo ya mizozo.Ulaya inabidi iachane na sera zake kali za kufunga milango yake na kusaka ufumbuzi utakaotanguliza mbele kinga ya binaadam ili kuepusha misiba kama hii.

Ulaya lazma ifunguwe milango yake kwa wakimbizi

Muda mrefu sasa hakuna kilichotendeka.Badala yake Umoja wa Ulaya inafika hadi ya kuitisha Ugiriki,mipaka itaanza upya kukaguliwa ikiwa mipaka ya nje ya nchi hiyo haitafungwa ipasavyo.Kwa kujizungushia ngome Ulaya inazidisha makali ya sera zake za kuwafungia milango wahamiaji.Kwanini hakisikilizwi kile kinachosemwa na mashirika ya haki za binaadam ambayo kwa miaka sasa yamekuwa yakidai ikomeshwe biashara haramu ya binaadam kupitia bahari ya kati na kusaka ufumbuzi?

Purukushani lazma ikome.Ulaya haistahiki kuziacha peke yao nchi mfano wa Italia.Nchi zote za Ulaya zinabidi zishirikiane kwa dhati ili kuwafungulia milango wale wanaohitaji kinga.Katika katiba za nchi wanachama wa Umoja wa ulaya kuna kifungu kinachozungumzia juu ya haki ya kuomba ukimbizi.Lakini wanaotokea katika nchi zenye mizozo wana nafasi gani ya kuomba kinga hiyo ya ukimbizi?Kwa wengi kati yao njia pekee ya kuingia ulaya,ni kupitia magengi ya wahalifu wanaojitajirisha kupitia jasho na maisha ya binaadam.Wahalifu hao wasiokuwa na huruma lazima washindwe nguvu.Wakati huo huo juhudi zinabidi ziendeshwe ili kuboresha hali ya maisha katika nchi zinazokabwa na mizozo.Wakimbizi wa kutoka Eritrea wanaipa kisogo nchi ambayo,miaka 20 baada ya kujipatia uhuru kutoka Ethiopia,inavunja mtindo mmoja haki za binaadam .Maelfu wanashikiliwa kama wafungwa wa kisiasa nchini humo bila ya kufikishwa mahakamani eti kwasababu ya kuiokosoa serikali."Nchi isiyotawalika",Somalia ingawa hivi sasa kuna serikali,lakini bado hakuna miundo mbinu wala taasisi za kuhakikisha usalama.

Mfumo wa kidemokrasi katika maeneo ya mizozo uimarishwe

Wakaazi wa maeneo ya mizozo wanatamani kuishi salama na kwa amani.Wanakimbia njaa,umaskini,vita na udhalilishaji.Na hayo hasa ndio maovu ambayo jumuia ya kimataifa inabidi iyashughulikie.Bara la Afrika ni jirani yetu.Tunabidi tuchangie kupambana na umaskini,njaa na hali duni na kuunga mkono kwa nguvu mageuzi ya kidemokrasia ili kubuni hali bora ya maisha kwa wote.Hadi lengo hilo litakapofikiwa Ulaya inabidi iwafungulie milango wale wanaohitaji kinga.

Mwandishi:Andrea Schmidt/Hamidou Oummilkheir

Mhariri:Mohammed Abdul-Rahman