1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Maoni:Wito wa kutofanya vita na Urusi una mapungufu

Josephat Nyiro Charo11 Desemba 2014

Wajerumani 60 mashuhuri wiki hii wametoa mwito dhidi ya kupigana vita na Urusi kuhusiana na mzozo wa Ukraine. Ingo Manteufel wa DW anasema mwito huo ni wa kuheshimika ila unapuuza masuala muhimu na ukweli halisi.

https://p.dw.com/p/1E2YK
Horst Teltschik / Sicherheitsberater
Horst TeltschikPicha: picture-alliance/dpa

Mwito huo ulianzishwa na Horst Teltschik, wa chama cha Christian Democratic Union, CDU, aliyewahi kuwa mshauri wa kansela wa Ujerumani, na Walter Stützle, aliyekuwa katibu wa dola aliyeshughulikia masuala ya usalama wa chama cha Social Democratic, SPD, pamoja na naibu spika wa zamani wa bunge la Ujerumani, Antje Vollmer wa chama cha Kijani.

Mwito huo uliokuwa na kichwa cha maneno "Vita vipya barani Ulaya? Sio kwa jina letu" ulisainiwa na Wajerumani 60 mashuhuri na wenye haiba kubwa wakiwa na lengo la kuepusha kutokea vita barani Ulaya na wakipendelea kuwepo mdahalo na Urusi. Miongoni mwao ni kansela wa zamani wa Ujerumani Gerhard Schröder wa chama cha Social Democratic, SPD na rais wa zamani Roman Herzog wa chama cha Christian Democratic Union, CDU.

Wajerumani hao wanasema kweli. Hakutakiwi kuwa na vita vingine zaidi Ulaya. Mdahalo unapaswa kuwa chombo muhimu cha sera ya nje katika taifa lenye utawala wa demokrasia. Hata linapokuja suala la jinsi Urusi inavyotendewa sasa kuhusiana na mzozo wa Ukraine. Lakini mwito huu kutoka kwa watu ambao bila shaka wamefaulu kufanikisha mambo mengi katika nyanja za siasa, biashara na utamaduni unakosa shabaha yake linapokuja suala la mgororo wa sasa.

Ni sahihi kabisa kusema hakutakiwi kuwa na vita Ulaya, lakini ukweli ni kwamba vita vilianza msimu wa machipuko uliopita wakati rais wa Urusi Vladimir Putin alipotumia harakati ya kijeshi kulitwaa eneo la Crimea na kulifanya kuwa sehemu ya shirikisho la Urusi. Sababu pekee kwa nini vita hivyo havikuwa vikubwa kati ya Urusi na Ukraine ni kwa kuwa serikali ya mjini Kiev iliyokuwa imelemewa ilijiepusha na kufanya harakati ya kijeshi kulilinda aneo la Crimea. Mashariki mwa Ukraine hata hivyo vita ambavyo vimesababisha vifo vya maelfu ya watu na uharibifu mkubwa vinaendelea waziwazi. Pasipo Urusi kupeleka wanajeshi na silaha vita hivi havingewezekana. Kwa mantiki hiyo mwito wa Wajerumani mashuhuri hauzingatii ukweli halisi.

Ingo Mannteufel, Leiter der Europa-Redaktion der DW
Ingo Mannteufel, Mkuu wa Idhaa ya Ulaya ya DWPicha: DW

Ubaya zaidi ni kuwa mwito huo unatoa taswira kwamba mataifa ya Magharibi ikiwemo Ujerumani, yatafanya operesheni ya kijeshi dhidi ya Urusi. Serikali ya Ujerumani na viongozi wa nchi wanachama wa Umoja wa Ulaya wameshafutilia mbali suluhisho la kijeshi katika mzozo huo. Licha ya changamoto zote kansela wa Ujerumani Angela Merkel na waziri wa mambo ya kigeni, Frank Walter Steinmeier, wameendeleza mdahalo wa kidiplomasia na Urusi. Lingekuwa jambo la busara kwa Wajerumani waliotia saiti mwito huo kuziunga mkono jitihada hizi za kidiplomasia. Mwito huo pia unakosa kuwahimiza viongozi wa Urusi kutenda haki kwa hali ilivyo sasa na kutimiza wajibu wao kulinda amani.

Masuala muhimu yamepuuzwa

Pendekezo kwamba waandishi wa habari hawafahamu hofu ya Urusi kuhusu jumuiya ya kujihami ya NATO kuinyemelea pia linalenga kubuni hadithi. Waliosaini mwito wa kutofanya vita na Urusi walipuuza mambo mawili muhimu. Kwanza, hakuna mipango yoyote madhubuti ya NATO kuikubali Georgia na Ukraine kuwa wanachama. Mwaka 2008 uanachama wa nchi hizo mbili ulikataliwa na uamuzi huu ulithibitishwa tena mwaka huu wakati wa mkutano wa kilele wa jumuiya hiyo uliofanyika nchini Wales. Pili, waliosaini mwito huo hawapaswi kusahau kwamba, mbali na masilahi ya kiusalama ya Urusi, pia kuna hofu ya raia wa Ukraine na Georgia, ambao wameshuhudia sehemu za nchi zao zikichukuliwa na Urusi kutumia nguvu za kijeshi.

Wajerumani mashuhuri wanajikanganya katika kumalizia mwito wao. Baada ya kuwakumbusha wasomaji kuhusu matumaini yaliyokuwepo mnamo mwaka 1990, ya kuundwa Ulaya yenye mshikamano katika uhuru na demokrasia, mwito huo unamaliza kwa kusema, "Hadi ulipotokea mzozo wa Ukraine, tuliamini tuko katika njia sahihi barani Ulaya." Kwa mitazamo mingi kauli hii haina maana.

Kuwa sehemu ya Ulaya yenye demokrasia ndicho wanachokitaka raia wa Ukraine. Kile kinachohusishwa na Warusi kwa haki hakitakiwi kunyimwa raia wa Ukraine. Na kama Urusi imefukuzwa nje ya Ulaya na siasa za Ulaya, kama inavyodhaniwa katika mwito huo, basi haiwezekani kwamba Ulaya imekuwa katika mkondo sahihi katika miongo iliyopita. Hata wanasiasa wa Urusi wenyewe wangepinga msimamo huu kwa kuwa ukosoaji wa Urusi wa sera ya Ujirani wa Ulaya ni wa zamani sana kuliko mzozo nchini Ukraine.

Mwandishi: Ingo Manteufel/Josephat Charo

Mhariri:Mohammed Abdul-Rahman