1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mapadri wahusishwa na udhalilishaji kingono Marekani

Isaac Gamba
15 Agosti 2018

Ripoti ya uchunguzi uliofayika kwa miaka miwili inaeleza kuwa zaidi ya watoto 1,000 walidhalilishwa kingono na mapadiri katika jimbo la Pennsylivania nchini Marekani.

https://p.dw.com/p/33Bzf
USA Pennsylvania Missbrauchsskandal | Josh Shapiro
Picha: picture-alliance/AP Photo/M. Rourke

 Akitangaza hapo jana ripoti ya uchunguzi huo  Mwanasheria Mkuu wa jimbo la Pennsylivania  Josh Shapiro amesema  maafisa wa kanisa Katoliki wanadaiwa kuwapuuza kabisa wahanga wa udhalilishaji huo wa kingono na kuwalinda watuhumiwa wa vitendo hivyo. 

Ameongeza kuwa maafisa waliweza kuwashitaki watu wawili tu ikiwa ni pamoja na padri aliyekili kuhusika na udhalilishaji huo wa kingono.

Katika uchunguzi wao, jopo la wazee  wa mahakama  liliwahoji mashahidi kadhaa na kufanikiwa kufichua zaidi ya nusu milioni ya kurasa za nyaraka kadhaa za siri  katika dayosisi nne tofauti nchini humo.

 Nyaraka hizo za siri zinahusisha maelezo yaliyoandikwa na baadhi ya mapadri wakikiri kufanya vitendo hivyo vya udhalilishaji .

 

Maelfu wamedhalilishwa

USA Pennsylvania Missbrauchsskandal
Baadhi ya wahanga au ndugu wa waliodhalilishwa kingono na mapadri katika jimbo laPennsylivania MarekaniPicha: picture-alliance/AP Photo/M. Rourke

Ripoti hiyo inaeleza zaidi kuwa waliofanyiwa udhalilishaji huo wanaweza kuwa maelfu kadhaa kutokana na baadhi ya kubukumbu kupotea huku wahanga wengi wakiogopa kujitokeza kuripoti udhalilishaji waliofanyiwa.

 Ripoti hiyo inaongeza kuwa wahanga wengi wa vitendo hivyo vya udhalilishaji ni wavulana ingawa hata wasichana nao pia walidhalilishwa.

Baadhi ya mapadri wanaoendelea kuhudumu hadi sasa  na wale wazamani ambao wametajwa katika ripoti hiyo walikwenda mahakamani kuzuia kutolewa hadharani kwa ripoti hiyo ya uchunguzi wakidai kuwa inakiuka haki yao ya kikatiba  na mchakato wa kimahakama.

Hata hivyo  Mahakama ya Juu  ya jimbo la Pennsylvania iliamua kuwa umma una haki ya kuiona ripoti hiyo ya uchunguzi ingawa pia ilizuia kutangazwa hadharani  majina ya wanaohusishwa na udhalilishaji huo  hadi pale kesi ya msingi dhidi yao itakaposikilizwa Septemba mwaka huu.

Kwa upande mwingine ripoti imemtaja  kadinali Donald Wuerl ambaye pia ni askofu wazamani wa Pittsburgh ikidai kuwa aliidhinisha uhamisho kwa baadhi ya mapadri wanaotuhumiwa kufanya vitendo hivyo badala ya kuwafuta kazi ikiwa ni pamoja na kuwasaidia kifedha mapadri ambao walilazimika kujiuzulu kutokana na kashifa hiyo.

Katika maelezo yake hapo jana Jumanne , Kadinali huyo alisema alitimiza wajibu wake kwa uadilifu ikiwa ni pamoja na kuzingatia wahanga wa vitendo hivyo vya udhalilishwaji huku akizuia  vitendo hivyo kutoendelea kufanyika.

Licha ya uchunguzi huo kuwekwa hadharani lakini bado kuna changamoto kubwa kutokana na ukweli kuwa baadhi ya wale wanaousishwa na kashifa hiyo ya udhalilishaji kingono uliofanyika katika jimbo la Pennsylivania Marekani  wamefariki na matukio mengi ya udhalilishaji yalifanyika miaka mingi iliypita hali inayofanya kuwa vigumu kuwashitaki.

Mapadri kati ya 5,700 na 10,000 wa kanisa Katoliki wanatuhumiwa kuhusika na udhalilishaji kingono nchini Marekani  lakini ni wachache tu  wanaoripotiwa kushitakiwa na hatimaye kutiwa hatiani hiyo ikiwa ni kwa mujibu wa chombo kinachofuatilia maadili ya viongozi wa kanisa.

Mwandishi: Isaac Gamba/ DW/APE

Mhariri: Iddi Ssessanga