1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mapambano makali yazuka Mogadishu watu 16 wameuwawa

1 Februari 2010

Viongozi wa Umoja wa Afrika wanaokutana Ethiopia watiwa wasiwasi na hali ya mambo nchini Somalia

https://p.dw.com/p/LoRh
Wapiganaji wa kundi la Al Shabaab washambulia ikulu ya raisPicha: AP
Mapigano makali yametokea nchini Somalia ambapo wapiganaji wa makundi ya itikadi kali Yaliifyatulia makombora ikulu ya rais kwenye mji mkuu Mogadishu jana usiku tukio lililowafanya wanajeshi kuanza kufyetua risasi ya wanamgambo hao na kuua kiasi cha watu 16.Mapigano hayo yametokea wakati mkutano wa Umoja wa Afrika ukiendelea huko mjini Addis Ababa nchini Ethiopia ambapo suala la Somalia ni miongoni mwa masuala katika ajenda.
Zwölfter Gipfel Afrikanische Union
Kikao cha Umoja wa Afrika kinazitaka Somaliland na Puntland kuisadia Somalia kupambana na wapiganajiPicha: picture alliance / Photoshot
Waziri wa mambo ya nje wa Somalia anayehudhuria mkutano huo unaojadili pia kuhusu Somalia,Ali Jama Jangeli alitoa mwito wa kupelekwa wanajeshi zaidi kusaidia kurudisha hali ya usalama nchini humo.Aidha hii leo kikao hicho kimeyataka majimbo yaliyojitenga na Somalia,ya Puntland na Somaliland kushirikiana kupambana na wanamgambo nchini Somalia. Katika mapigano yaliyozuka jana usiku kundi la wanamgambo la Al shabaab ambalo linadaiwa na Marekani kuwa ni kundi la wafuasi wa Alqaeda nchini Somalia lilishambulia mara kadhaa ikulu ya rais kutoka sehemu za mji mkuu Mogadishu.Wanajeshi wa serikali kwa upande wake walijibu mashambulio hayo kwa kuwafyetulia risasi.Wakaazi wa eneo hilo pamoja na maafisa wa matibabu wamesema makombora kadhaa yaliangukia upande wa mji wa Suqa Holaha kaskazini mwa mji wa Mogadishu au mji unaojulikana kama soko la mifugo na kusababisha watu wasiopungua 16 kuuwawa na wengine 71 wakajeruhiwa.Kutokana na mwito uliotolewa na waziri wa mambo ya nje wa Somalia,ulioungwa mkono na mawaziri wa nje wa Kenya na Sudan, Djibouti imesema iko tayari kutuma wanajeshi wake 450 kuisadia serikali ya Somalia lakini msemaji wa kundi la al Shabaab ,Sheikh Ali Mohammud Rage hapo jana jioni aliitaka nchi hiyo kutafakari juu ya uamuzi wake huo.Juu ya hilo ameionya serikali hiyo ya Djibouti isipeleke wanajeshi nchini Somalia vinginevyo itakabiliwa na matatizo makubwa.Mzozo huo wa Somalia pia umesababisha wanawake na watoto kuendelea kuteseka nchini humo hali ambayo imemgusa hata katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki Moon.Akizungumza katika ufunguzi wa mkutano huo wa Umoja wa Afrika alisema anapanga kumteua Margot Wallstrom kutoka Sweden kuwa mjumbe wake maalum atakayekuwa na jukumu la kukabiliana na vitendo vya ubakaji dhidi ya wanawake na watoto kwenye maeneo ya mizozo. Mizozo ya muda mrefu nchini Somalia,Sudan na Jamhuri ya kidemokrasi ya Kongo ambako kunashuhudiwa ubakaji wa wanawake na watoto ni suala linalotarajiwa kuugubika mkutano huo unamalizika kesho jumanne.Mapigano nchini Somalia yamesababisha watu 21,000 kuwawa tangu mwaka 2007 yalipoibuka,na watu wengine zaidi ya millioni moja wameitoroka nchi hiyo. Mwandishi Saumu Mwasimba/ RTRE Mhariri Mohammed Abdulrahaman