1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mapambano yaendelea Jerusalem

Admin.WagnerD14 Septemba 2015

Mvutano ulioanza jana (13.09.2015) bado unaendelea baina ya vijana wa Kipalestina na polisi wa Israel katika eneo tukufu uliopo msikiti wa al-Aqsa pamoja na mabaki ya hekalu takatifu kwa upande wa Wayahudi.

https://p.dw.com/p/1GW70
Israel Al Aqsa Moschee Palästinenser Gefechte Neujahr Jüdisch
Picha: picture-alliance/dpa/A. Sultan

Ni siku ya pili tangu kuanza kwa mapambano kati ya vijana wa Kipalestina pamoja na polisi wa Israel, katika uwanja uliopo msikiti mtukufu wa al-Aqsa mjini Jerusalem. Kituo cha redio Israel kimeripoti kuwa vijana kadhaa waliokuwa wanawarushia mawe polisi wamekamatwa karibu na msikiti huwo.

"Pale walinzi wa ndani ya msikiti wa al-Aqsa wanapopinga na kuandamana juu ya Wayahudi kuingia msikitini, hayo ni maandamano ya amani. Wanaposema Allahu Akbar yaani Mungu mkubwa, hayo ni maaandamano ya amani ya kuwapinga Wayahudi wenye misimamo mikali kuingia msikitini, ambao wanasaidiwa na polisi pamoja na vikosi vya Israel," amesema Mkurugenzi wa msikiti wa al-Aqsa Omar Kisswani.

Mapigano hayo yanafanyika katika eneo tukufu kwa pande zote mbili - Wapalestina na Waisrael - na katika wakati ambapo Mayahudi wanaadhimisha kuanza kwa mwaka mpya wa Rosha Hashana wa dini yao, ambao ulianza rasmi usiku wa Jumapili.

Polisi wa Israel walilivamia eneo hilo Jumapili huku mapigano yakiwa yanapamba moto baada ya vikundi viwili vya Kiislamu kuwekewa marufuku kupiga doria katika maeneo ya msikiti huwo. Polisi imesema walivamia eneo hilo kuhakikisha usalama wa Wayahudi pamoja na watalii wakati wa masaa ya matembezi ndani ya eneo hilo.

Watu wasio Waislamu wanaruhusiwa kuingia katika uwanja wa msikiti huwo lakini Wayahudi hawana ruhusa ya kusali ili kuepusha hatari ya kutokea mvutano na waislamu wanaokwenda kusali ndani yamsikiti huwo.

Eneo hilo ulipo msikiti wa al-Aqsa ni moja kati ya maeneo matukufu katika dini ya Kiislamu lakini pia kwa upande wa Israel ni eneo yalipo magofu ya hekalu ya Kiyahudi iliyotajwa ndani ya biblia na kwa hiyo pia ni eneo takatifu kwa dini ya Kiyahudi.

Polisi kulinda usalama

Palästina Israel Zusammenstöße in Jerusalem
Picha: Getty Images/AFP/A. Gharabli

Polisi wamesema vijana wa Kiislamu walikuwa na mpango wa kuwavamia Wayahudi waliyokuja kufanya ibada zao katika eneo yalipo mabaki hayo ya mwisho ya ukuta wa hekalu takatifu kwa wayahudi.

Kulingana na taarifa za vyombo vya habari vya Israel, Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu, kesho ataitisha mkutano wa dharura na baraza la mawazri, kujadili suala la uslama, baada ya kumalizika maadhimisho ya mwaka mpya wa Rosha Hashana.

Wapalestina wana wasiwasi kuwa Israel watabadilisha sheria za eneo hilo, huku makundi ya Kiyahudi ya mrengo wa kulia yakiwa yanatafuta njia za kujenga hekalu mpya katika eneo hilo.

Wapalestina wanapinga udhibiti wa Isarel wa maeneo hayo matukufu ikiwamo msikiti wa al-Aqsa katika mji mkongwe wa Jerusalem. Eneo hilo lilitiwa mikononi na Israel baada ya vita vya mwaka 1967.

Mwandishi: Yusra Buwayhid/dpae/afpe

Mhariri: Iddi Ssessanga