1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mapambano yanaendelea kuudhibiti Kobane

10 Oktoba 2014

Jopo la wanajeshi wa Marekani na Uturuki watakutana wiki ijayo mjini Ankara kujadili mapigano dhidi ya wanamgambo wa IS baada ya Marekani kuibinya Uturuki kujiunga na muungano wa kijeshi unaoongozwa na Marekani.

https://p.dw.com/p/1DT0Y
Kämpfe in Kobane
Mji wa KobanePicha: Reuters/U. Bektas

Wajumbe wawili wa ngazi ya juu wa Marekani wamekutana jana na viongozi wa Uturuki wakitafuta kuishawishi nchi hiyo ambayo ni mshirika wake katika jumuiya ya NATO kuunga mkono mapambano ya angani dhidi ya kundi linalojiita Dola la Kiislamu IS, ambalo limekamata maeneo makubwa ya ardhi nchini Iraq na Syria.

Bildergalerie Kobane
Makombora yakianguka mjini KobanePicha: Christopher Johnson

Licha ya kwamba msemaji wa wizara ya mambo ya kigeni ya Marekani Jen Psaki hakuainisha majukumu maalum yaliyotolewa na Uturuki , amesema nchi hizo mbili zimekuwa na mazungumzo ya kina na yenye maelewano.

Marekani imeitaka Uturuki jana kujiunga na mapigano dhidi ya wapiganaji wa kundi la IS ambaol wanasonga mbele, ambao wamekamata sehemu ya mji muhimu wa mpaka na Syria wa Kobane licha ya mashambulizi ya anga yanayoongozwa na jeshi la Marekani.

Syrien Kobane IS Terror Grenze Türkei 8. Oktober
Mapambano katika mji wa mpakani wa KobanePicha: Aris Messinis/AFP/Getty Images

Katika mapigano hayo ambayo yamesababisha vifo vya mamia ya raia , miito imeongezeka ya kutaka majeshi ya ardhini kuwasaidia wapiganaji wa Kikurdi ambao wamezingirwa katika mji huo wa Kobane.

Uturuki yakataa kuchukua hatua pekee

Lakini baada ya mazungumzo na katibu mkuu wa NATO Jens Stoltenberg , waziri wa mambo ya kigeni wa Uturuki Mevlut Cavosoglu amesema serikali ya nchi yake haiwezi kutarajiwa kuchukua hatua pekee.

Syrien Kobane IS Terror Grenze Türkei 8. Oktober
Mji wa Kobane unaokabiliwa na mapambano makali.Picha: Reuters/U. Bektas

Kobane mji ambao wanamgambo wa Kikurdi bado wanapambana baada ya mapambano ya wiki tatu sasa dhidi ya wapiganaji wa Jihadi, umekuwa eneo muhimu la mapambano katika vita dhidi ya kundi la IS. Waziri wa mambo ya kigeni wa Marekani John Kerry amesema

"Kobane ni msiba kwasababu unawakilisha uovu wa kundi la IS lakini sio tafsiri ama ya maafa ama kiwango kamili cha yale yanayotokea kutokana na mapambano na IS. Ni mji mmoja na kutakuwa na mingine ambako kutakuwa na mzozo na IS katika muda wa miezi ijayo."

Syrien Kobane IS Terror Grenze Türkei 08.10.2014
Vifaru vya Uturuki vikiwa nje ya mji wa KobanePicha: Reuters/Umit Bektas

Afisa wa Kikurdi na wanaharakati wa Syria wamesema kundi la Dola la Kiislamu limeshambulia kwa makombora kituo cha mpakani kati ya Syria na Uturuki leo kujaribu kukikamata na kukata mawasiliano na mji wenye mapigano wa Kobane

Baadhi ya wadadisi wa masuala ya kijeshi wanafikiria kwamba majeshi ya Marekani yangepeleka ndege zaidi za upelelezi katika eneo la Kobane, na kuwezesha kutambua maeneo muhimu ya kushambulia. Lakini maafisa wa Marekani wamekataa kusema lolote kuhusu uwezekano huo.

Mwandishi: Sekione Kitojo / afpe

Mhariri:Yusuf Saumu