1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mapambano yanaendelea Libya

3 Machi 2011

Uasi Libya unazidi kujipanga, na unaomba kuungwa mkono duniani, ukielekea kutafuta udhibiti wa eneo la magharibi karibu na mji mkuu, Tripoli.

https://p.dw.com/p/10So6
Machafuko LibyaPicha: AP

Utawala wa rais Barack Obama nchini Marekani unaendelea kugongana vichwa katika kuijadili hali nchini Libya.

Libyen Unruhen Proteste in Tobruk Plakaten Demonstration
Picha: dapd

Huku mapambano yakizidi kati ya wafuasi wa kiongozi wa Libya, kanali Muammer Gaddafi, na waasi waliodhibiti maeneo mengi ya nchi hiyo, katibu mkuu wa Umoja wa Nchi za Kiarabu, Arab League, Amr Moussa, amesema mpango wa amani kwa nchi hiyo kutoka rais wa Venezuela, Hugo Chavez, unasukwa.

Alipoulizwa iwapo Gaddafi aliukubali mpango huo, Amr Moussa, aliyezungumza na shirika la habari la Reuters kupitia njia ya simu, alisema kuwa hajui, na yeye binafsi hakubaliani na mpango huo wa amani.

Libyen Unruhen Öl Ölpreis Wintershall
Picha: picture alliance/dpa

Bei ya mafuta ilishuka kufuatia taarifa hizo za kutafutwa mpango wa amani, ambapo waekezaji waliangalia uwezekano wa makubaliano ya kibiashara yaliofikiwa na nchi ya Venezuela. Hugo Chavez ni rafiki wa karibu wa Muammar Gaddafi.

Mashambulio zaidi

Waasi wameyalipiza mashambulio ya ardhi na angani yalioanzishwa na vikosi vya Gaddafi katika mji wa Brega, uliopo mashariki mwa nchi hiyo, wakati Gaddafi amezionya nchi za nje zenye nguvu kutokea mashambulio mingine mithili ya Vietnam, iwapo wataingilia mapinduzi dhidi ya utawala wake wa miaka 41.

Muammar Gaddafi
Kanali Moammar Gaddafi.Picha: AP

Waasi katika mji wa Benghazi wameomba usaidizi wa mashambulio ya angani yanayoungwa mkono na Umoja wa mataifa kusaidia kusitisha mashambulio ya mamluki wa Kiafrika ambao wanasema Gaddafi anawatumia dhidi ya raia nchini humo.

Msemaji wa baraza la kitaifa la uasi nchini Libya, Hafiz Ghoga, amesema wanaomba kushambuliwa maeneo makuu waliomo mamluki hao. Naibu balozi wa Libya wa Umoja wa mataifa, ambaye alikuwa miongoni mwa wajumbe wa kwanza waliojitenga na Gaddafi, amesema Umoja wa mataifa huenda ukaunga mkono pendekezo la marufuku ya ndege kutoruka Libya iwapo baraza la kitaifa nchini humo litatoa ombi rasmi.

Serikali ya Marekani inakuwa makini kuhusu kuidhinisha marufuku hiyo dhidi ya Libya, ikisisitiza hatari zilizomo za kidiplomasia na za kijeshi, lakini imezipeleka meli za kivita katika bahari ya meditarenia.

Umoja wa Nchi za Kiarabu umesema unapinga uvamizi wa moja kwa moja wa jeshi la nchi za nje, lakini huenda ukaidhinisha marufuku ya kutoruka ndege juuya anga ya Libya kwa ushirikiano na Umoja wa Afrika, AU.

Mwandishi Maryam Abdalla/Rtre /Ape
Mhariri: Miraji Othman