1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mapatano ya kwanza juu ya Dafur

17 Februari 2009

Waasi na serikali ya Sudan watia saini mapatano ya Doha.

https://p.dw.com/p/Gvuw

Taarifa kutoka Doha, mji mkuu wa Qatar, zinasema serikali ya Sudan na waasi wa chama cha Justice and Equality Movement-chama kinachogombea usawa na haki mkoani Dafur,wametia saini hivi punde mapatano yatakayofungua mlango wa mazungumzo makubwa zaidi yenye shabaha ya kukomesha ugomvi wa miaka 6 mkoani Dafur,Sudan ya magharibi.Qatar,ambayo imekuwa mwenyeji wa mazungumzo ya amani kati ya chama hicho cha waasi na serikali kuu ya Sudan kwa muda wa wiki sasa, ilitangaza jana kufikiwa maafikiano hayo.

"Maendeleo makubwa yamefikiwa na sasa tumefikia mapatano."Alinukuliwa waziri mkuu wa Qatar, Sheikh Hamad bin Jassem al-Thani kuwaambia maripota.

Wahisani wa mazungumzo haya ya Doha-Qatar,Umoja wa Mataifa,Umoja wa Afrika na Jumuiya ya nchi za kiarabu-Arab League wamesisitiza hatahivyo kuwa ni ya kwanza na wanakusudia kufungua njia kwa mkutano mkubwa zaidi juu ya hatima ya Dafur,mkoa wa magharibi wa Sudan.

"Tunatumai kuanzisha mazungumzo hayo mnamo muda wa wiki mbili hivi na miongoni mwa maswali mengine, itazungumzwa swali la kusimamisha mapigano na yale yanayohusiana na kubadilishana wafungwa."aliongeza Sheikh Hamad,ambae pia ni waziri wa nje wa Qatar.

Chama cha waasi chenye silaha kali zaidi miongoni mwa vile vya waasi-JEM (kwa ufupi) kiliyasusia mapatano yalioshindwa kuleta amani yaliotiwa saini 2006 na kikundi kingine cha waasi.

Na Mei mwaka jana JEM ikaanzisha hujuma kali zisizowahi kuonekana dhidi ya mji mkuu wa Sudan,Khartoum.

Kwa muujibu wa UM ,watu laki 3 wameuwawa na zaidi ya milioni 2.2 wameyakimbia maskani yao tangu pale waasi huko Dafur, waliposhika silaha kupambana na serikali kuu ya Khartoum, hapo Februari,2003.

Sudan ambayo Rais wake Omar al-Bashir anakabiliwa na uwezekano wa kutolewa hati ya kimataifa ya kukamatwa kwake kwa tuhuma za uhalifu wa vita huko Dafur, inadai idadi ya waliouwawa ni 10.000 tu.

Amin Hassan Omar, mmoja kati ya wajumbe wa serikali ya Sudan amenukuliwa kuungama kwamba wameafikiana kimsingi kuwaacha huru wafungwa wao waliohusika na mzozo wa Dafur.Mapatano yaliofikiwa leo yalifuatia kikao kirefu cha hapo jana kati ya viongozi wa wajumbe wa pande hizo mbili-Kiongozi wa JEM Khalil Ibrahim na Nafie Ali Nafie,msaidizi wa rais Bashir.

Kikao hicho kilihudhuriwa na Bw.Ahmed Ben Abdallah al-Mahmud, waziri wa dola wa Qatar anehusika na siasa za nje na Djibril Bassole,mpatanishi wa kikosi maalumu cha UM na Umoja wa afrika kwa mzozo wa Dafur.

Kiongozi wa chama cha waasi (JEM) Khalil Ibrahim, alisema hapo yalipoanza mazungumzo ya Doha kwamba, mazungumzo marefu zaidi yatawezekana tu pindi serikali ya Sudan itakapokuwa tayari kukomesha harakati za wanamgambo wa kiarabu wa shirika wa serikali huko Dafur na kufungua mlango wa uwakilishi wa nyadifa za juu kwa waasi ndani ya serikali kuu ya Sudan.