1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mapatano yakifikiwa Ireland kaskazini

Mohammed Abdul-Rahman27 Machi 2007
https://p.dw.com/p/CHHR

Baada ya miaka mitano ya utawala wa moja kwa moja kutoka serikali kuu ya Uingereza katika jimbo la Ireland kaskazini, kuanzia tarehe 8 Mei jimbo hilo litakua likijiendeshea mambo yake lenyewe. Haya yanatokana na kukutana kwa mara ya kwanza jana mjini Belfast, Kiongozi wa chama cha Waprotestanti DUP kasisi Ian Paisley mwenye umri wa miaka 80 na kiongozi wa chama cha Sinn Fein cha jamii ya wakatoliki Gerry Adams ikiwa ni kwa mara ya kwanza kabisa.

Bunge la Ireland Kaskazini lilichaguliwa awali 1998, kwa lengo la kumaliza vita vya kiraia vya muda mrefu kati ya jamii mbili za waprotestanti na wakatoliki. Lakini 2002 likasimamishwa na serikali ya Uingereza mjini London, baada ya kuzuka mgogoro wa kutoaminiana kuhusiana madai kwamba IRA bawa la kijeshi la Sinn Fein lilikua likifanya ujasusi ndani ya bunge hilo.

Lakini kilichowezekana jana ,hakikuwahi kufanywa na vizazi vilivyopita. Bw Ian -Paisley kiongozi wa kiprotestanti mwenye msimamo mkali, alifikia maridhiano na mwenzake wa chama cha Sinn Fein mkatoliki .Gerry Adams, ikiwa ni kwa mara ya kwanza kabisa. Sinn Fein ni bawa la kisiasa la jeshi la IRA lililokua likiendesha kampeni ya matumizi ya nguvu na vitisho vya mashambulio ya mabomu.

Hata baada ya ule mkataba wa kihistoria wa Ijumaa kuu wakati wa pasaka 1998, wanasiasa hao wawili hawakukutana. Sasa wamekubaliana kuunda serikali ya pamoja, itakayoongozwa na Paisley huku naibu wake akiwa Martin McGuiness, aliyewahi kuwa kamanda wa jeshi la IRA. Matarajio ya umma hayakupotea. Jee baada ya miaka mingi ya uhasama,sasa kweli umoja utapatikana ?

Sio bure kwa hivyo pale Paisley alipotamka kwamba makubaliano hayo ni “muhimu kwa mustakbali wa jimbo hilo” na Gerry Adams akisema ni “ mwanzo wa enzi mpya ya kisiasa.”

Kuna msingi wa kutosha wa kuwa na serikali ya pamoja. Uhalali wa kidemokrasi wa kushirikiana pamoja kwa masilahi ya umma wa Ireland kaskazini ni matumaini ya siku za usoni baada ya athari za miaka mingi iliopita.

Chama cha kasisi Paisley-DUP kiliibuka na ushindi wa wingi mdogo tu katika uchaguzi wa karibuni na ni ushirikiano wa pamoja tu utakaoleta suluhisho.

Matatizo kama ukosefu wa ajira, elimu na afya yanaisubiri serikali mpya. Katika jimbo ambalo ukosefu wa kuvumiliana kidini na uadui ni jambo lililokuweko tangu vizazi vilivyopita, hakuna utawala unaoweza kutarajia kwamba yataondoka yenyewe.

Serikali ya Uingereza imetenga kitita kikubwa .Mpango wa bilioni moja za fedha kuimarisha makubaliano haya. Kwa hivyo akiandamwa na malalamiko juu ya kushiriki kwake katika vita vya Irak na kashfa za rushwa ndani ya chama chake tawala cha Leba, waziri mkuu wa Uingereza Tony Blair,anataka kuona kuna kitakachomrudishia heba yake , ikiwa ni miezi michache kabla hajan´gatuka madarakani. Anayetarajiwa kuwa mrithi wake, waziri wa fedha Gordon Brown anaweza kuwa mwenye furaha wakati Blair atakapomuachiwa jukwaa la kupambana na wakonservative huku , matatizo makubwa ya ndani katika ajenda yake yakiwa yamepungua .

Kuvumiliana kidini na kisiasa kwa hivyo kwa wakaazi wa Ireland kaskazini pamoja na ushirikiano wa dhati kati ya jamii hizo mbili, waprotestanti na wakatoliki- jimboni humo, ndiyo nguzo muhimu ya mustakbali wa jimbo hilo.