1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mapigano Makali Mashariki mwa Ukraine

Admin.WagnerD19 Juni 2014

Mapigano makali yameripotiwa leo kati ya jeshi la serikali ya Ukraine na wapiganaji wa waasi wa mashariki mwa nchi hiyo wanaotaka kujitenga. Duru za jeshi zimesema kuwa kila upande ulitumia vifaru katika mapigano hayo.

https://p.dw.com/p/1CLuP
Taarifa zimesema kila upande katika mapigano ulitumia vifaru
Taarifa zimesema kila upande katika mapigano ulitumia vifaruPicha: Reuters

Chanzo cha kijeshi katika eneo la mzozo kimeeleza kuwa mapigano yalianza saa kumi alfajiri ya leo karibu na mji wa Krasny Liman ambao tangu mwanzoni mwa mwaka huu umekuwa chini ya udhibiti wa serikali ya mjini Kiev. Wanaharakati wa mashariki wanaotaka kujitenga walijaribu mara kadhaa kuivunja ngome ya jeshi la serikali katika mji huo.

Kwa mujibu wa chanzo hicho, mapigano ya leo yalikuwa makubwa zaidi kuliko mengine yote yaliyoshuhudiwa awali. Kulingana na Dmytro Tymchuk, mchambuzi wa masuala ya kijeshi ambaye anayo mawasiliano na jeshi la Ukraine, mapigano ya leo yalianza pale wanaharakati walipokataa kutii amri ya kuweka silaha zao chini, kuheshimu mpango wa amani uliowekwa na rais mpya wa nchi hiyo, Petro Poroshenko.

Vifaru vyatumiwa kwenye uwanja wa vita

Inadhaniwa kwamba wapiganaji wanaotaka kujitenga wapatao 4000 walishiriki katika mapigano hayo, na kwamba kila upande ulitumia magari ya kivita. Vyanzo vya kijeshi vimedai kuwa huenda hata vifaru vilitumiwa.

Ngome ya wanaharakati waaotaka kujitenga mjini Donetsk
Ngome ya wanaharakati waaotaka kujitenga mjini DonetskPicha: picture-alliance/dpa

Msemaji wa serikali mjini Kiev Vladyslav Seleznyov amethibitisha kutokea kwa mapigano hayo, na kuongeza kuwa kile alichokiita ''Operesheni dhidi ya magaidi'' kitaendelea.

Wakati huo huo Waangalizi wa Umoja wa Mataifa mashariki mwa Ukraine wametoa ripoti yao, wakieleza kuwa watu wasiopungua 356 wameuwa katika eneo hilo tangu kuanza kwa uhasama tarehe 7 Mei. Kwa mujibu wa ripoti hiyo, zaidi ya 250 miongoni mwa waliokufa ni raia.

Umoja wa Mataifa watoa ripoti

Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa anayehusika na haki za binadamu Ivan Simonovic amesema ripoti ya Umoja huo inajumuisha mapendekezo juu ya kumaliza mzozo.

Naibu Katibu Mkuu wa UN anayehusika na haki za binadamu, Ivan Simonovic.
Naibu Katibu Mkuu wa UN anayehusika na haki za binadamu, Ivan Simonovic.Picha: picture alliance/AP Photo

''Ripoti hii inajumuisha mapendekezo kwa serikali ya Ukraine na kwa upande mwingine, bila shaka haja ya kupunguza matumizi ya nguvu kuhakikisha kuwa sheria inaheshimiwa inamaanisha kuwa wanaharakati wataweka silaha chini na kuruhusu mazungumzo ya dhati, yanayokwenda sambamba na katiba ya Ukraine''

Naibu Katibu Mkuu huyo wa Umoja wa Mataifa amewaambia waandishi wa habari kwamba kwa mara ya kwanza, wawakilishi wa upande unaojiita Jamhuri ya Donetsky wamekubali kwamba miongoni mwa wapiganaji wao, wamo wanamgambo wa kujitolea kutoka Urusi, hasa majimbo ya Chechnya na Cossacks.

Huku hayo yakiiarifiwa, makamu rais wa Marekani, Joe Biden amerudia tena msimamo wa Marekani kwamba nchi hiyo itaiwekea vikwazo vipya Urusi, ikiwa itashindwa kutumia ushawishi wake juu ya wanaharakati wanaotaka kujitenga mashariki mwa Ukraine kusimamisha ghasia katika eneo hilo.

Mwandishi: Daniel Gakuba/RTRE/APE

Mhariri: Josephat Charo