1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mapigano ya Kordofan yaingia Kusini,hali ya wasiwasi

Saumu Ramadhani Yusuf13 Juni 2011

Umoja wa Mataifa umesema kwamba mapigano katika eneo tete la Kordofan Kusini yamesambaa katika eneo la mpakani na kuingia Sudan Kusini.

https://p.dw.com/p/11ZZt
Wakaazi wa Abyei wakimbia nyumba zaoPicha: DW

Kitisho hicho kimekuja wakati viongozi wa pande zote mbili,Sudan Kusini na Kaskazini wakiendelea na mazungumzo juu ya mzozo wa eneo hilo nchini Ethiopia. Mazungumzo ya mjini Adis Ababa kati ya Salva Kiir na Omar El Bashir yanafanyika huku waziri wa mambo ya nje wa Marekani, Hillary Clinton, aliyeko ziarani barani Afrika, akitangaza ridhaa ya nchi yake, ya kuunga mkono wazo la kupeleka wanajeshi wa kulinda amani katika jimbo linalozozaniwa la Abyei.

Rais wa Sudan Omar al-Bashir na kiongozi wa Sudan Kusini Salva Kiir wamekuwa katika mazungumzo tangu jana Jumapili mjini Adis Ababa, nchini Ethiopia, mazungumzo yenye lengo la kutafuta mwafaka juu ya mzozo katika jimbo la Abyei na eneo la mpakani la Kordofan Kusini.

Sudan Referendum
Raia wa Sudan Kusini akipeperusha bendera ya jimbo hilo litakalotangaza uhuru wake kamili July 9Picha: picture alliance/dpa

Harakati hizo zinakuja ikiwa ni mwezi mmoja kabla ya Sudan Kusini kutangaza uhuru wake. Wapatanishi wanaohudhuria mazungumzo hayo wameyataja kuwa yanayokabiliwa na hali ya wasiwasi na kwamba huenda yakachukua muda wa masaa mengi kumalizika.

Mazungumzo hayo yanafanyika huku Umoja wa Mataifa ukithibitisha kwamba mapigano yaliyokuwa yanaendelea tangu siku kadhaa zilizopita huko kuisini mwa  Kordofan, jimbo pekee la Kaskazini linalozalisha mafuta yamezagaa katika eneo zima la mpakani na kuingiaa Kusini. Ofisi ya shirika la Umoja wa Mataifa linalohusika na masuala ya kibinadamu la OCHA imetoa tamko ikisema kwamba mapigano hayo yanahusisha mashambulizi ya mabomu na mizinga yameripotiwa katika maeneo 11 kati ya 19 kwenye jimbo hilo la Kordofan Kusini na kuenea hadi katika mji wa Pariang, Sudan Kusini.

Ama kwa upande mwingine, waziri wa mambo ya nje wa Marekani, Hillary Clinton, atakutana na kiongozi wa  wa Sudan Kusini, Salva Kiir, mjini Addis Ababa, Ethiopia, jioni hii lakini hatokutana na rais Omar Al Bashir wa Sudan Kaskazini. Akiwa nchini Tanzania, Clinton amezungumzia juu ya msimamo wa Marekani wa kuunga mkono pendekezo la kutuma wanajeshi wa kulinda amani huko Abyei na kusisitiza kwamba Sudan Kaskazini inabidi iondoe wanajeshi wake katika eneo la mpakani.

Jeshi la Sudan Kusini linasema kwamba ndege za kivita za upande wa kaskazini zimeshambulia ardhi yake mapema hii leo baada ya kusambaa kwa mapigano ya Kordofan Kusini.Tayari mashirika ya misaada yanahofia kwamba idadi ya waliouwawa ikazidi ingawa hadi sasa ni watu wachache walioripotiwa kujeruhiwa.

Flash-Galerie Sudan Brennendes Lager
Jeshi la Kaskazini ladaiwa kushambulia kutoka angani dhidi ya KusiniPicha: picture-alliance/dpa

Maafisa wa Sudan Kusini wamekuwa wakisema kwamba vikosi vya wanajeshi wa kaskazini vimeua raia kadhaa katika mashambulizi ya angani katika eneo la mpaka wa kusini. Kwa siku nane mfululizo mapigano yamechacha kati ya wanajeshi wa Sudan na vikosi vya jeshi la waasi wa zamani SPLA katika eneo la kusini mwa Kordofan.

Umoja wa Afrika mjini Adis Ababa unaosimamia mazungumzo kati ya al- Bashir na Salva Kiir umetoa taarifa yake kabla ya kikao cha leo, na kusema kwamba mazungumzo hayo yataelekezwa zaidi kuhusu jimbo tete la Abyei miongoni mwa masuala mengine muhimu yanayoikabili Sudan katika kipindi hiki cha kihistoria. Sudan Kusini inajiandaa kutangaza uhuru wake kamili July 9, chini ya makubaliano ya amani baada ya miongo kadhaa ya mzozo na kaskazini na mapigano ya sasa yanatishia kugubika hatua hiyo ya kihistoria, hasa ikiwa jeshi la Kusini litaingilia kati.

Mwandishi Saumu Mwasimba/AFPE

Mhariri Othman Miraji.