1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mapigano yachacha Afghanstan

19 Juni 2007

wanamgambo wa kundi la Taliban wameiteka wilaya moja iliyoko kwenye eneo la milima kusini mwa nchi hiyo.

https://p.dw.com/p/CB3U

Hii imetokea wakati wa mapambano ya hivi karibuni ya waasi yaliyosababisha kuuwawa kwa watu kadhaa.

Taarifa za kutekwa kwa wilaya ya Myanishen kusini mwa jimbo la Kandahar imethibitishwa leo hii na wizara ya mambo ya ndani ya Afghanstan ikisema vikosi vyake vimejiondoa katika eneo hilo lakini kwa muda tu na hivi karibuni wanapanga kuikomboa tena wilaya hiyo toka kwa wapiganaji.

Wapiganaji hao wakitaliban waliarifu hapo jana jioni kwamba wameshaiteka wilaya hiyo iliyoko kwenye eneo la milimani na kusema kuwa wamewauwa polisi kiasi cha kumi lakini wizara ya mambo ya ndani imekanusha ripoti hiyo.

Msemaji wa kundi la Taliban Yousef Ahmadi aliliambia shirika la habari la AFP kwamba polisi iliwabidi kukimbilia milimani baada ya kuwazingira kwa siku mbili.

Na kufikia jana jioni tayari kundi hilo la Taliban lilikuwa limeiteka wilaya nzima.

Wapiganaji wa Taliban sasa wamedhibiti ofisi zote za serikali na magari pamoja na silaha katika wilaya hiyo.

Hatua hii inaonekana ni kama pigo kwa jeshi la Nato ambalo limeongeza mapambano yake dhidi ya kundi hilo la Taliban katika eneo la kusini.

Kundi la Taliban lililoanzisha mapigano kwa lengo la kuikomboa Afghanstan nchi ambayo walikuwa wakiiongoza kati ya mwaka 1996 na mwaka 2001 wamekuwa wakishikilia wilaya kadhaa kusini na magharibi mwa nchi hiyo lakini wamekuwa wakitimuliwa baada ya muda wa siku chache.

Hata hivyo wameshikilia kwa miezi sasa wilaya ya Musa Qala katika jimbo la Helmand linalopakana na Uruzgan na Kandahar na wanadaiwa kushikilia pia wilaya nyingine kwenye eneo hilo.

Maafisa wa wilaya iliyotekwa wamedai raia wengi waliuwawa kwenye mapigano ya siku tatu yaliyojumuisha mashambulio ya angani yaliyofanywa na wanajeshi wa NATO.

Wizara ya mambo ya ndani ya Afghanstan lakini imesema ni raia 10 na zaidi ya wataliban 60 waliouwawa kwenye mkoa wa Uruzgan na kupinga madai yaliyotolewa na maafisa wa wilaya hiyo.

Jeshi la Nato kwa upande wake limesema halijapokea taarifa zozote za kuuwawa kwa raia lakini linaamini wengi waliouwawa kwenye mashambulio yake ya angani ni wataliban.

Katika tukio jingine mtu mmoja alijeruhiwa alipokuwa akijaribu kutega bomu nje ya kambi ya wanajeshi wa Marekani nchini humo.kwa mujibu wa jeshi la Marekani bomu hilo liliripuka kabla ya muda wake nje ya kambi yake ya Bagran na mtu aliyehsuika amekamatwa.

Watoto sabaa waliuwawa kwenye shambulio la angani lililofanywa na kikosi kinachoogozwa na Marekani siku ya jumapili.

Shambulio hilo lilidhamiriwa kuwalenga wanamgambo wa kundi la kigaidi la Al Qaeda wanaoendesha hujuma mashariki mwa Afghanstan.

Msemaji wa kikosi cha wanajeshi wa NATO Major John Thomas anasema mapigano bado yanaendelea katika jimbo la Uruzgan: