1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mapigano yachacha nchini Chad

7 Mei 2009

Chad yailaumu Sudan kwa kuwaunga mkono waasi wa UFR

https://p.dw.com/p/HlIW
Wakimbizi katika kambi ya Touloum mashariki mwa Chad.Picha: AP

Huku mapambano kati ya waasi na vikosi vya serikali yakiendelea kuchacha mashariki mwa Chad. umoja wa mataifa unasema kuwa utachukua hatua za kuwalinda raia.mapigano yalizuka kusini mwa eneo la Goz Beida jana jumatano na kuwalazimu wafanyakazi wa kutoa misaada wa umoja wa mataifa kuondolewa kutoka kambi za wakimbizi.

Hadi sasa hakuna majeruhi au vifo vlivyoripotiwa katika mapigano hayo. Waasi wanasema kuwa lengo lao kuu ni kufika katika mji mkuu wa Chad N`Djamena.

Wakati huo huo Chad imeishutumu Sudan kwa kuyatuma makundi yaliyojihami, waliovuka mpaka siku mbili tu baada ya nchi hizo mbili mahasimu, kutia saini makataba wa kuleta mapatano kati yao, shughuli iliyofanyika nchini Qatar.

Waziri anayehusika na mawasiliano nchini Chad Mahamat Hissene alikiambia kituo cha Radio ya taifa kuwa Sudan ilituma makundi yaliyojihami muda mfupi kabla ya mapatano ya Doha,madai ambayo yalikanushwa kwa haraka na Sudan.

Chad na Sudan zilirejesha uhusiano wa kidiplomasia kati yao mwezi Novemba mwaka uliopita baada ya kusitisha uhusiano huo mwezi mei.Mataifa hayo mawili pia yamekuwa yakilaumiana kwa muda mrefu kwa kuendesha vita kati yao huku yakiwa yanawatumia waasi.

Mwezi mei mwaka uliopita Sudan iliishutumu Chad kwa kuwaunga mkono waasi kutoka jimbo la Darfur walioushambulia mji mkuu wa Sudan Khartoum, shutuma ambazo zilijibiwa na Chad iliyosema kuwa hapo awali Sudan iliwaunga mkono waasi walioushambulia mji wake mkuu N`Djamena.

Siku ya Jumapili sudan na Chad walitia sahihi mkataba wa mapatano kati yao mjini Doha chini ya upatanishi wa Qatar na Libya.

UN Generalsekretär Ban Ki Moon
Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki Moon.Picha: picture-alliance/ dpa

Jana Jumatano Katibu mkuu wa umoja wa mataifa Ban Ki Moon alisema kuwa vikosi vya kudumisha amani vilivyo nchini chad na Jamhuri ya Afrika ya kati, vitawalinda raia. Ban Ki Moon alisema kuwa visa vyo vyote vya kuhatarisha maisha ya raia vitakabiliwa vilivyo.

Aidha alizitaka nchi za Chad na Sudan kutatua tofauti zao kwa njia za kidiplomasia.

Hapo jana waziri wa ulinzi nchini Chad Ahmat Mahamat Bashir alisema kuwa vikosi vya Chad vilifanya mashambulizi ya angani dhidi ya waasi mashariki mwa nchi na kuongeza kuwa Chad imejiandaa kukabiliana na waasi hao ikiwa wataendelea kusonga mbele.

Bashir pia alisema kuwa wanajeshi walikuwa wakisambazwa kukabilaina na makundi ya waasi katika Jamahuri ya Afrika ya kati karibu na mpaka na Chad .

Waziri huyo wa Ulinzi wa Chad alimshutumu rais wa Sudan Omar El Bashir kwa kuwaamrisha mamluki kuishambulia Chad na kuapa kuwa waasi hao watakabilöiwa vilivyo.

Sudan na Chad zimekuwa na uhasama kwa muda mrefu huku kila nchi ikiishutumu nyingine kwa kutaka kuingusha serikali yake.Waasi nchini Chad wa Chad`s Union Resitance Forces UFR walisema kuwa walipigana vita vya muda mfupi na wanajeshi wa serikali karibu na mpaka wa Sudan na pia karibu na mpaka wa Jamhuri ya kati na kuongeza kuwa wanaendelea kusongea mbele.

Msemaji wa waasi hao alisema kuwa wanafanya kila jitihada kufika katika mji wa N`Djamena alioutaja kuwa lengo lao kuu. Ali Hemchi alisema kuwa waasi waliyateka magari 12 ya kijeshi na kuharibu mengine katika miji ya Tisssi Na Haraz Mangue baada ya wanajeshi kukimbia.

Mwandishi :Jason Nyakundi/AFP

Mhariri: Thelma Mwadzaya.