1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mapigano yaendelea Libya huku Gaddafi akiwa hajulikani aliko

25 Agosti 2011

Wanajeshi watiifu kwa kanali Muammar Gaddafi wamepambana na majeshi ya waasi na kusababisha baadhi ya wakaazi wa mji mkuu Tripoli kuingiwa na hofu kubwa, kwamba huenda hali hiyo ikaendelea kwa muda mrefu.

https://p.dw.com/p/12NHl
Moshi ukitanda katika anga ya mji mkuu, TripoliPicha: dapd

Waasi wa Libya wameendelea kupambana na wafuasi wa kiongozi wa nchi hiyo kanali Muammar Gaddafi mjini Tripoli huku wakiwasaka jamaa na wafuasi wa kiongozi huyo. Waasi hao wamekabiliana na kamanda wa jeshi la Gaddafi kwenye mapigano makali katika shamba lake mjini Tripoli hapo jana.

Msemaji wa waasi hao, Abdel Salam Abu Zaakouk, ameiambia televisheni ya Al Arabiya kwamba mapigano hayo yameendelea katika shamba la mnadhimu wa jeshi la Gaddafi, Abdul Rahman Al Sayd, bila kutoa maelezo ya kina.

Katika tukio lengine msemaji huyo amesema waasi wamemkamata mkurugenzi wa afisi ya Gaddafi, Bashir Saleh, na watoto wake wanne, kwenye shamba la familia yake mjini Tripoli, ambako alikuwa amevalia vazi la Kisudan ili asijulikane.

Milio ya risasi ilisikika nje ya hoteli ya Corinthia katikati ya mji mkuu Tripoli jana jioni na mawingu ya moshi kutanda kutoka upande risasi zilikotokea. Mwandishi wa habari wa shirika la habari la Uingereza, Reuters, amesema kundi la waasi waliokuwa na silaha waliingia ndani ya hoteli hiyo wakimtafuta mtoto wa kiume wa Gaddafi, Saadi, baada ya kupata taarifa kwamba alikuwa ndani ya hoteli hiyo. Wanaume hao walizuia njia zote na kuanza kupekua kila chumba wakimsaka.

Der libysche Revolutionsführer Muammar al-Gaddafi
Kiongozi wa Libya, Muammar GaddafiPicha: AP

Mpaka sasa Gaddafi mwenyewe hajulikani aliko, lakini jana alisikika akisema kwenye ujumbe wake kwamba, "Nimetembea katika barabara za Tripoli bila kujilikana. Nimewaona vijana waliokuwa tayari kuulinda mji. Walionekana hawaamini utawala wetu uko hatarini."

Vikosi vinavyomtii Gaddafi vinauzingira mji unaodhibitiwa na waasi wa Zuwarah, magharibi mwa Tripoli. Waasi mjini humo wamelemewa na wameomba msaada kutoka mji wa Ziltan na maeneo mengine ya kusini yanayodhibitiwa na waasi. Juhudi zinaendelea kupeleka waasi kwenda kuwasaidia wenzao mjini Zuwarah.

Waandishi watekwa wengine waachiwa

Wapiganaji wafuasi wa Gaddafi jana waliwateka nyara waandishi wanne wa habari wa Italia waliokuwa wakisafiri kwenye motokaa kuelekea mji mkuu Tripoli wakitokea Zawiyah. Wafuasi wa Gaddafi waliisimamisha gari yao na kumuua dereva kabla kuwakamata waandishi hao na kuwapeleka ndani ya nyumba.

Mwandishi mmoja wa gazeti la Avvenire Catholic aliruhusiwa kupiga simu kwa wahariri wao kuelezea masaibu yaliyowakuta. Wawili wanafanya kazi na gazeti la Corriere della Sera na wa mwisho anaandikia gazeti la La Stampa.

Waandishi wa habari wa kigeni ambao walikuwa wakizuiliwa katika hoteli ya Rixos mjini Tripoli wameachiwa huru.

Wamarekani wanne waliokuwa wakizuiliwa na vikosi vya Gaddafi wameachiwa huru baada ya waasi kulikomboa gereza moja mjini Tripoli hapo jana, ambalo lilikuwa likishikiliwa na wafuasi wa kiongozi huyo. Afisa wa wizara ya mambo ya kigeni ya Marekani, ambaye hakutaka kutajwa jina, amethibitisha taarifa hizo akisema idadi ya Wamarekani walioachiwa Libya tangu mwezi Juni mwaka huu imefikia wanane.

Ufaransa kuendelea kuisaidia Libya

Wakati huo huo, Ufaransa imeapa kuendelea kuwasaidia raia wa Libya. Rais wa Ufaransa Nicolas Sarkozy amesema nchi yake itaendelea na harakati za kijeshi nchini Libya mradi itaendelea kuhitajika na waasi.

Akizungumza jana kwenye mkutano na waandishi wa habari mjini Paris, baada ya kukutana na kiongozi wa baraza la kitaifa la mpito, Mahmoud Jibril, Sarkozy alisema Ufaransa iko tayari kuendelea na operesheni ya kijeshi chini ya azimio namba 1973 la Umoja wa Mataifa.

Frankreich EU Nicolas Sarkozy
Rais wa Ufaransa, Nicolas SarkozyPicha: AP

Rais Sarkozy, kiongozi wa kwanza wa nchi za magharibi kuwatambua waasi kama serikali halali, amewaalika viongozi wa dunia kuhudhuria mkutano Septemba mosi kujadili juhudi za kuijenga upya Libya.

Urusi, China, India na Brazil, nchi ambazo zimekuwa na wasiwasi kuhusu operesheni ya kijeshi ya jumuiya ya kujihami ya NATO iliyoanza mwezi Machi mwaka huu, zitaalikwa kwenye mkutano huo unaolezwa kuwa wa marafiki wa Libya.

Marekani yaishinikiza Afrika Kusini

Kwa upande mwingine Marekani inataka baraza la usalama la Umoja wa Mataifa liishinikize Afrika Kusini iachane na msimamo wake wa kukataa kuachia dola bilioni 1.5 mali ya Libya kwa ajili ya kugharimia misaada ya dharura ya kibinadamu nchini Libya. Wanadiplomasia wa Afrika Kusini wanasema hawapingi msaada wa kibinadamu kupelekwa Libya lakini suala la kuregeza vikwazo vya Umoja wa Mataifa linahitaji ridhaa pana ya baraza la kitaifa la mpito la Libya.

Serikali ya Afrika kusini inataka kusibiri mkutano wa kilele wa Umoja wa Afrika unaofanyika leo na kesho mjini Addis Ababa Ethiopia, kabla kuendelea mbele na suala hilo.

Mwandishi: Josephat Charo/AFPE/RTRE/

Mhariri: Sekione Kitojo