1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mapigano yaendelea mjini Tripoli

23 Agosti 2011

Mapigano makali yameendelea mjini Tripoli usiku kucha huku kiongozi wa Libya kanali Muammar Gaddafi akiwa hajulikani aliko.

https://p.dw.com/p/12LbU
Waasi wa Libya mjini TripoliPicha: picture-alliance/dpa

Milio ya risasi na miripuko imerindima usiku kucha katika eneo lililo karibu na makazi ya Gaddafi, Bab al Aziziya, ambamo inaaminiwa angalao mwanawe mmoja amejificha. Ingawa kumekuwa na taarifa kwamba Gaddafi mwenyewe huenda akawa yumo ndani ya makazi hayo, ripoti zimesema alitoroka katika mpaka na Algeria au mji wa bandari wa Sirte, alikozaliwa. Kiongozi wa baraza la mpito la kitaifa, Mustafa Abdul Jalil, amesema anataka Gaddafi akamatwe na kushtakiwa badala ya kuuwawa.

Ndege za kivita za jumuiya ya kujihami ya NATO zimeyashambulia makazi ya Gaddafi mapema leo. Mapigano pia yameripotiwa huko Zawiya.

Ajitokeza baada ya kukamatwa

Seif al Islam, mtoto wa kiume wa Gaddafi ambaye mwendesha mashtaka mkuu wa mahakama ya kimataifa ya uhalifu wa kivita ICC, Luis Moreno-Ocampo, na waasi wa Libya walisema amekamatwa, alijitokeza mapema leo katika hoteli moja ambamo waandishi wa habari wa kigeni wamekuwa wakiishi.

Libyen Saif al Islam Gadhafi in Tripolis
Saif al-Islam, mtoto wa GaddafiPicha: dapd

Seif amewaambia waandishi wa habari nje ya makazi ya babake kwamba utawala wa Gaddafi bado unaudhibiti mji mkuu Tripoli. Seif amesema babake yuko salama na katika hali nzuri mjini Tripoli, alipoulizwa na mwandishi wa habari wa shirika la BBC.

Balozi wa Libya nchini Marekani, Ali Suleiman Aujali, amesema Mohammed Gaddafi, mtoto wa kiume wa kwanza wa Gaddafi ameponyoka na kutoroka baada ya kukamatwa na waasi mjini Tripoli.

Utawala wa Gaddafi wafika kikomo

Akizungumzia hali mpya iliyojitokea Libya, Rais wa Marekani Barack Obama amemtaka Gaddafi amalize umwagaji damu, akisema hali nchini humo ingali ni ya wasiwasi. Amesema kuna wafuasi wa utawala wa Gaddafi ambao bado ni kitisho, lakini jambo moja liko wazi kabisa, "Utawala wa Gaddafi unakaribia mwisho na mustakabali wa Libya uko mikononi mwa raia."

Rais Obama ameahidi kuwa Marekani itakuwa rafiki na mshirika kuisadia Libya yenye demokrasia kuondokana na enzi ya Gaddafi. Obama pia ameuonya upinzani wa Libya dhidi ya vitendo vya kulipiza kisasi kwa miongo minne ya utawala wa mkono wa chuma wa kanali Gaddafi.

"Haki halisi haitapatikana kutokana na ulipizaji kisasi na machafuko. Itapatikana kwa upatanisho na Libya inayoruhusu raia wake kuamua mustakabali wao."

US-Präsident Obama fordert Gaddafis Machtverzicht
Rais Barack Obama wa MarekaniPicha: AP

Rais Obama amesema Marekani itaendelea kushiriki katika operesheni ya Libya na kuipongeza jumuiya ya kujihami ya NATO kwa jukumu lake katika operesheni hiyo ya kumuondoa Gaddafi madarakani. Obama aidha amesema harakati ya kijeshi nchini Libya imedhihirisha mambo ambayo jumuiya ya kimataifa inaweza kuyafanikisha inaposimama kama kitu kimoja.

"Ingawa juhudi hazijaisha Libya, jumuiya ya NATO kwa mara nyingine tena imedhihirisha ni muungano wenye uwezo mkubwa dunaini na kwamba nguvu zake zinatokana na silaha zake na nguvu za maadili yetu ya demokrasia."

Umoja wa Ulaya kuisaidia Libya

Wakati huo huo Umoja wa Ulaya umesema uko tayari kuisadia Libya kwa kila njia katika wiki, miezi na miaka ijayo. Mkuu wa sera za kigeni wa umoja huo, Catherine Ashton, amesema kupitia msemaji wake, Michael Mann, kwamba Libya inaingia katika enzi mpya na ni wakati wa kuanzisha mchakato wa kuelekea Libya mpya itakayojengwa katika misingi ya demorasia, na ambako sheria na haki za binadamu zitaheshimiwa kikamilifu.

Bi Ashton amesema Umoja wa Ulaya utaendelea kutekeleza vikwazo dhidi ya Libya lakini utakuwa tayari kuviondoa mara moja wakati muafaka utakapofika.

Umoja wa Ulaya ungependa kumuona Gaddafi, mwanawe Seif al Islam na mkuu wake wa ujasusi Abdullah al Senussi, wakijibu mashtaka katika mahakama ya kimataifa ya uhalifu, mjini The Hague Uholanzi.

Rais wa Umoja wa Ulaya, Herman van Rompuy na mkuu wa kamisheni ya umoja huo, Manuel Barroso wamesema katika taarifa yao ya pamoja kwamba umoja huo utashirikiana na jumuiya ya kimataifa kuisaidia Libya katika mchakato wa kuimarisha demokrasia na uchumi, utaojikita katika misingi ya haki za kiraia, kuwajumuisha viongozi kutoka makundi yote nchini na kuheshimu mipaka ya Libya.

Umoja wa Mataifa kuijadili Libya

Kwa upande mwingine katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban Ki Moon amewataka wanajeshi wanaomtii Gaddafi wasitishe mapigano.

"Ni muhimu kwa mzozo huu umalizike bila maisha zaidi kuangamia. Navitaka vikosi vya Gaddafi vikomeshe mara moja mapigano kutoa nafasi kwa kipindi cha kukabidhi madaraka kwa amani. Jumuiya ya kimataifa itaendelea kutimiza jukumu lake la kuwalinda raia."

Ban Ki Moon kandidiert für zweite Amtszeit
Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban Ki-moonPicha: picture-alliance/dpa

Ban Ki Moon aidha amesema Umoja wa Mataifa utafanya kikao cha dharura wiki hii kujadili mustakabali wa Libya pamoja na viongozi wa Umoja wa Afrika, jumuiya ya nchi za kiarabu, Umoja wa Ulaya na muungano wa mataifa ya kiislamu.

Mwandishi: Josephat Charo/RTRE/DPAE/AFPE

Mhariri: Saumu Mwasimba