1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mapigano yaikumba Eritrea na Ethiopia

Sylvia Mwehozi14 Juni 2016

Eritrea na Ethiopia zimetupiana lawama kwa kuanzisha mapigano mwishoni mwa juma baina ya majeshi yake katika eneo la mpakani linalotumiwa na nchi zote mbili la Tsorona.

https://p.dw.com/p/1J6Eu
Äthiopien äthiopische Soldaten auf dem Weg zu Mogadishu
Picha: picture-alliance/dpa/A. Albadri

Eritrea na Ethiopia zimetupiana lawama kwa kuanzisha mapigano mwishoni mwa juma baina ya majeshi yake katika eneo la mpakani linalotumiwa na nchi zote mbili la Tsorona, ikiashiria kuendelea kwa mgogoro wa mpaka uliochochea vita baina ya mataifa hayo mawili mwaka 1998 hadi 2000.

Ethiopia imesema kwamba hali ilitulia hapo jana, baada ya wakaazi wanaoishi upande wa nchi hiyo kutoa taarifa za kusikika kwa milipuko iliyodumu siku nzima ya Jumapili hadi Jumatatu asubuhi.

Eritrea nchi iliyo Pembe ya Afrika, ilijipatia uhuru kutoka mikononi mwa Ethiopia mnamo mwaka 1991. Takribani watu 70,000 waliuawa katika vita ya kugombea mpaka baina ya mataifa hayo mawili.

Waziri wa habari wa Eritrea amesema kwamba serikali ya Ethiopia ilianzisha mashambulizi dhidi ya nchi yake katika eneo la mbele la Tsorona.

Msemaji wa Umoja wa Mataifa amewaambia waandishi wa habari mjini New York kuwa katibu mkuu Ban Ki-moon anao wasiwasi juu ya mapigano hayo na tayari anataka kuzifikia pande zote mbili.

Amesema kwamba "katibu mkuu anazitaka serikali zote kujizuia na kufanyia kazi utatuzi wa tofauti zao kwa njia ya amani, ikiwemo utekelezaji wa makubaliano ya amani waliyosaini mwaka 2000" amesema waziri huyo.

Umoja wa Mataifa ulipeleka kikosi cha kufuatilia makubaliano ya kusitishwa kwa mapigano mwaka 2000 katika mpaka baina ya nchi hizo mbili , lakini hata hivyo ilikiondoa kikosi hicho 2008 kutokana na vikwazo vilivyowekwa na Eritrea na hivyo kushindwa kufanya kazi kwa ujumbe huo.

Rais wa Eritrea Isayas Afewerki
Rais wa Eritrea Isayas AfewerkiPicha: picture-alliance/dpa

Ethiopia kwa upande wake nayo imekanusha kuanzisha chokochoko ikisema kwamba ni majeshi ya Eritrea yaliyoanzisha fujo hizo.

Waziri wa habari wa Eritrea Yemene Ghebremeskel hakuwa na maoni juu ya majeruhi au taarifa nyingine juu ya mashambulizi hayo.Maafisa wa Ethiopia nao hawajatoa taarifa ikiwa kulikuwa na majeruhi.

Umoja wa Mataifa unaishutumu Eritrea kwa ukiukwaji wa muda mrefu wa haki za huduma za kitaifa ambapo raia wa nchi hiyo hutumia muda mrefu wakilipwa ujira mdogo kwa mujibu wa sheria.

Charlotte King, mchambuzi mwandamizi wa Afrika katika kitengo cha intelijensia ya uchumi anasema wakosoaji wa Eritrea wataona kama nchi hiyo inajaribu kukwepa tahadhari ya jumuiya za kimataifa dhidi ya uhalifu wa ubinaadamu na kuhalalisha mahitaji yake ya kijeshi.

Eritrea iliyo na vikwazo vya Umoja wa mataifa inasema mataigfa yenye nguvu yameshindwa kuishinkiza Ethiopia kukubaliana na usuluhishi wa kimataifa unaotawala mpaka huo. Ethiopia imesema inataka mazungumzo kwa ajili ya utekelezaji.

Mwandishi:Sylvia Mwehozi/Reuters

Mhariri: Iddi Ssessanga