1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mapigano yapamba moto Pakistan

Oummilkheir9 Oktoba 2007

Eti kweli India iko nyuma ya mapigano haya ya sasa nchini Pakistan?

https://p.dw.com/p/C77x
Wanajeshi wa serikali ya Pakistan
Wanajeshi wa serikali ya PakistanPicha: AP

Wanamgambo 150 wa kiislam na wanajeshi 45 wa Pakistan wameuwawa kufuatia mapigano makali yanayoendelea tangu siku tatu zilizopita katika jimbo la kikabila la Pakistan linalopakana na Afghanistan.Mamia ya watu wanayapa kisogo maskani yao katika eneo hilo.

Mapigano hayo yameripuka jumapili iliyopita katika jimbo la kaskazini la Waziristan baada ya waasi kuushambulia mlolongo wa magari ya wanajeshi.Jeshi lilijibisha mashambulio hayo kwa kutuma wanajeshi wa nchi kavu wakisaidiwa na helikopta za kivita katika eneo la milimani karibu na mji wa Mir Ali.

Mashambulio hayo yanasemekana kua mabaya zaidi kuwahi kushuhudiwa nchini Pakistan tangu nchi hiyo ilipoamua kuunga mkono vita vya Marekani dhidi ya ugaidi mnamo mwaka 2001.

Miili ya wanajeshi wa Pakistan,wengi wao wakiwa wamekatwa vichwa,imegunduliwa na wananchi wanaokimbia mapigano kaskazini mwa Waziristan.Kuna ripoti zinazosema raia wa kawaida pia ,wakiwemo wanawake watatu ,wameuliwa katika mapigano hayo.

Wakaazi wanasema watu wengi wanaoishi Mir Ali,mji wa pili kwa ukubwa katika eneo hilo la milimani,wameyapa kisogo maskani yao baada ya nyumba 50 kubomolewa vitani.

Sheria ya kutotoka ovyo ilitangazwa mjini humo mapigano yaliporipuka na vikosi vya usalama vimelifunga soko kuu pamoja na kuuzingira mji huo.

Wananchi wasiojua la kufanya wanatumia vipaza sauti vya msikitini kuwaomba wanajeshi wasifyetue risasi dhidi ya nyumba zao.

Upande wa upinzani unahoji balaa lote hili limesababishwa na uamuzi wa rais Musharaf wa kushirikiana na Marekani katika vita dhidi ya ugaidi .

“Vita vyote hivi na woga uliotanda,vimesababishwa na mtu mmoja tuu.Wanajeshi wa Pakistan wanauliwa katika maeneo ya kikabila,raia wa Pakistan wanauliwea,watu wanajiripua na kuyatolea mhanga maisha yao.Nchi hii inatumbukia katika janga lisilokadirika-majimbo mawili yanakumbwa na balaa la vita vya wenyewe kwa wenyewe.”

Mikoa ya kaskazini na kusini ya Waziristan katika jimbo la mpakani la kaskazini magharibi,ndiyo kitovu cha maeneo ambayo Marekani inadai wafuasi wa Al Qaida na wataliban wa kutoka Afghanistan wamejenga kambi zao licha ya kuwepo wanajeshi 90 elfu wa Pakistan.

Rais Pervez Musharraf ,aliyeshinda uchaguzi wa rais jumamosi iliyopita,alihakikisha wiki iliyopita,hakuna kambi za Al Qaida nchini mwake.Alikiri hata hivyo kwamba wanaharakati wa itikadi kali ya dini ya kiislam wenye mafungamano na Al Qaida wamejificha katika maeneo hayo.

Wanamgambo wanaopigana Waziristan wanatajikana kua hodari na “wana miliki silaha za kisasa na fedha chungu nzima wanazojipatia kupitia maeneo ya mpakani.”

Maafisa wa Pakistan wanaamini huenda India ikawa nyuma ya wimbi hili jipya la mapigano,lililoripuka baada ya Pakistan kuuvamia msikiti mwekundu mjini Islamabad mwezi July uliopita.

Wakati huo huo kiongozi wa Al Qaida Ossama Ben Laden amewahimiza wanamgambo wa kiislam walipize kisasi kwa kuuliwa watu 100 mskiti mwekundu ulipovamiwa na wanajeshi wa Pakistan.