1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mapigano yaripuka upya Tripoli

31 Julai 2014

Mapigano makali yameripuka karibu na uwanja wa ndege mjini Tripoli kati ya makundi hasimu ya itikadi kali huku vikosi vya zima moto vikipambana na janga linaloteketeza matangi ya mafuta

https://p.dw.com/p/1Cn11
Wanamgambo wa Mistrata wakiwania uwanja wa ndege wa TripoliPicha: picture-alliance/AP Photo

Kutokana na kuzidi kuwa mbaya hali ya mambo nchini Libya,nchi kadhaa zimewahamisha raia na watumishi wa wakala zao za kidiplomasia.. Hispania imetangaza kuwahamisha kwa muda watumishi wa ofisi yao ya ubalozi huku visiwa vya Philippines vikisema vimekodi meli kuwahamisha raia wake 13 elfu.Ugiriki pia inatuma meli kuwahamisha raia wake wake wasiopungua 200 kutoka Libya.

Baada ya siku mbili tulivu kidogo,waasi wameanza upya kuuhujumu uwanja wa ndege,wakitumia silaha nzito nzito na nyepesi pia" amesema mkuu wa vikosi vinavyoshughulikia ulinzi wa Uwanja wa ndege al Jilani al Dahech wakatai wa mahojiano na shirika la habari la Ufaransa AFP.

Kwa mujibu wa mashahidi mapigano yameripotiwa pia katika njia inayoelekea uwanja wa ndege na katika eneo la magharibi la mji mkuu Tripoli.Mizinga pia imehanikiza kutoka eneo la kati la mji mkuu.

Matangi ya mafuta yanateketea

Wakati huo huo vikosi vya zima moto vinaendelea kupambana na janga la moto linaloteketeza matangi ya mafuta yenye shehena ya lita milioni 900 ya mafuta na gesi. Shughuli zao zilibidi kusitishwa mara kadhaa tangu jumapili iliyopita kwasababu ya mapigano.

Libyen Treibstofftanks Brand Explosion Rakete Zerstörung Feuer Evakuierung
Matangi ya mafuta yafuka motoPicha: Reuters

Mapigano yanaukaba mji mkuu ambako shughuli za benki na tawala zimesita tangu siku kadhaa zilizopita.Wakaazi wa Tripoli wanasumbuliwa na ukosefu wa mafuta,umeme na maji.

Mji mkuu Tripoli umejiinamia na maduka mengi yamefungwa hata kama eneo la kati hadi wakjati huu lilikuwa limesalimika.

Bunge jipya huenda likakutana jumamosi

Mashariki ya Libya,mjini Benghazi hali ni shuwari kidogo baada ya siku kadhaa za mapigano yaliyoangamiza maisha ya karibu watu mia moja na kupelekea wanamgambo wa itikadi kali kukidhibiti kituo muhimu cha kijeshi mjini humo.

Libyische Flüchtlinge in Tunesien 2011
Wananchi wayapa kisogo maskani yao kutokana na mapiganoPicha: Joel Saget/AFP/Getty Images

Makundi ya wanamgambo wa itikadi kali wanaidhibiti pia hospitali al Jala,iliyoko katika eneo la kati la Benghazi,baada ya kutimuliwa hapo awali na waandamanaji.

Kutokana na hali ya vurugu inayotawala nchini humo,bunge lililotokana na uchaguzi wa juni 25 iliyopita,limeamua kukutana jumamosi ijayo katika mji wa mashariki wa Tobrouk,masaa 48 kabla ya muda uliopangwa hapo awali wa kuitishwa kikao hicho cha ufunguzi mjini Benghazi.

Hata hivyo haijulikani kama kikao hicho kweli kitaitishwa,baada ya spika wa bunge lililomaliza mhula wake kushikilia kikao cha ufunguzi kitaitishwa kama ilivyopangwa Agosti nne ijayo, lakini mjini Tripoli na sio Benghazi.

Mwandishi:Hamidou Oummilkheir/Reuters/AFP

Mhariri: Josephat Charo