1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mapigano yasitishwa Gaza kwa saa 12

26 Julai 2014

Mapigano kati ya Israel na Hamas yanaonekana yataendelea baada ya waziri wa mambo ya kigeni wa Marekani John Kerry kushindwa Ijumaa(25.07.2014)kupatanisha makubaliano ya kusitisha mapigano.

https://p.dw.com/p/1CjD6
Al-Kuds Iran Teheran Anti-Israel Demonstration 25.07.2014
Maandamano kupinga mapigano Gaza mjini TehranPicha: picture-alliance/dpa

Hatua hiyo ingefungua njia ya kupata makubaliano mapana zaidi ya kusitisha mapigano.

Waziri wa ulinzi wa Israel Moshe Yaalon ameonya kuwa nchi yake huenda ikapanua kwa kiasi kikubwa hivi karibuni operesheni yake ya ardhini katika ukanda wa Gaza.

Saa kadhaa baada ya juhudi zilizoongozwa na Marekani kushindwa, pande hizo mbili zimekubaliana kusitisha mapigano kwa muda wa saa 12 kwa misingi ya kiutu kuanzia Jumamosi.

John Kerry / Nahost-Konflikt / Kairo
Waziri wa mambo ya kigeni wa Marekani John KerryPicha: Reuters

Ukingo wa magharibi

Hata hivyo , muda huo mfupi wa kusitisha mapigano hautarajiwi kubadili muelekeo wa uhasama uliopo hivi sasa huku kukiwa na ishara kuwa vita vya Gaza vinautumbukiza pia upande wa ukingo wa magharibi.

Katika siku ya "hasira" Wapalestina katika eneo hilo, ambalo limekuwa kimya kwa miaka kadha , walifanya maandamano dhidi ya operesheni inayofanyika Gaza na hali ya kuongezeka kwa vifo katika eneo hilo.

Katika ukingo wa magharibi , kiasi Wapalestina sita wameuwawa na jeshi la Israel, maafisa wa hospitali wamesema.

Israel / Gazastreifen / Tunnel / Soldat / Nahost-Konflikt
Wanajeshi wa Israel ndani ya ukanda wa GazaPicha: Reuters

Kushindwa kwa hatua za kidiplomasia hivi sasa, baada ya siku kadhaa za diplomasia ya kiwango cha juu katika eneo hilo, kunaashiria kuwa pande zote mbili hazitaki kukubali na kwamba mapigano katika ukanda wa Gaza huenda yakaendelea.

Israel inataka muda zaidi kuharibu njia za chini ya ardhini za Hamas pamoja na maeneo yakurushia maroketi katika ukanda wa Gaza, wakati watawala wa eneo hilo kutoka kundi la Hamas wanataka uhakika wa jumuiya ya kimataifa kuwa mzingiro wa mipaka ya Gaza utaondolewa kabla ya kuanza kwa usitishaji wa mapigano.

Al-Kuds Berlin Anti -Israel Demonstration Palästinenser 25.07.2014
Maandamano kupinga operesheni ya Israel ukanda wa Gaza , mjini BerlinPicha: Reuters

Jeshi la Israel limesema katika taarifa kuwa usitishaji wa mapigano wa saa 12 leo Jumamosi (26.07.2014) utaanza saa mbili asubuhi saa za mashariki ya kati. Lakini imeonya kuwa jeshi hilo litajibu iwapo magaidi wataamua kutumia hali hiyo ya kusitisha mapigano kuvishambulia vikosi vya Israel , ama kushambulia maeneo ya raia nchini Israel.

Shughuli za kutambua na kuharibi mahandaki zaendelea

Jeshi hilo limesema kuwa shughuli za kutambua na kuharibu njia za chini ya ardhi katika ukanda wa Gaza zitaendelea.

Msemaji wa Hamas , Sami Abu Zuhri , amesema mapema jana Ijumaa kuwa kundi hilo limekubali kusitisha mapigano kwa muda wa saa 12, kwa lengo la kuruhusu raia kupata msaada na kukimbilia katika maeneo salama.

Raia katika pande zote mbili wameathirika kwa kiasi kikubwa katika muda wa siku 18 zilzopita.

Palästinenser Israel Gaza Explosion nach Luftangriff
Mripuko wa kombora mjini GazaPicha: Reuters

Katika eneo la Gaza , mashambulizi ya anga ya israel na makombora ya vifaru yamesababisha vifo vya zaidi ya Wapalestina 860, 5,700 wamejeruhiwa, na mamia kwa maelfu wamekimbia makaazi yao na nyumba kadha zimeharibiwa.

Wanajeshi wawili wa Israel wameuwawa jana Ijumaa katika mapigano katika ukanda wa Gaza na kufikisha idadi ya wanajeshi waliouwawa tangu kuanza kwa operesheni ya ardhini kufikia 37.

Mwandishi Sekione Kitojo / ape / afpe

Mhariri : Daniel Gakuba