1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mapigano zaidi Syria

MjahidA6 Desemba 2012

Vikosi vya serikali ya Bashar Al Assad vimeripotiwa kufanya mashambulizi katika maeneo ya waasi nchini Syria na pia maeneo yalio nje ya mji mkuu Damascus

https://p.dw.com/p/16wXq
Moshi unaotokana na mashambulizi Syria
Moshi unaotokana na mashambulizi SyriaPicha: picture-alliance/dpa

Kulingana na shirika linaloangalia masuala ya haki za binaadamu nchini Syria lililo na makao yake mjini London mapigano ya jana pekee yalisababisha vifo vya watu zaidi ya 104. Idadi hiyo imetolewa na wanaharakati, mawakili na hata wataalamu wa afya.

Hii leo Asubuhi mjini Damascus, vikosi vya serikali vilizingira wilaya ya Zahra kusini mwa nchi hiyo baada ya bomu lililoegeshwa ndani ya gari moja kuripuka. Hakuna visa vyovyote vya majeruhi vilivyoripotiwa katika tukio hilo.

Vikosi vilivyotiifu kwa serikali ya Bashar Al Assad vimekuwa vikishambulia maeneo matatu nje kidogo wa mji wa Damascus, maeneo ya Douma kaskazini mashariki, Daraya, na pia Moadamiyet al-Sham, mji ulio kusini magharibi mwa Syria, Miji inayosemekana kukaliwa na waasi.

Jeshi lililotiifu kwa Bashar al Assad
Jeshi lililotiifu kwa Bashar al AssadPicha: picture-alliance/dpa

Tangu kuanza kwa ghasia miezi 21 iliopita nchini Syria watu takriban 41, 000 wameuwawa huku wengine wengi wakiachwa bila makaazi.

Onyo la Marekani juu ya Syria

Huku hayo yakiarifa maafisa wa Marekani wamesema utawala wa Assad umejitayarisha kutumia mabomu ya angani yalio na gesi ya sumu ambayo huenda yakarushwa katika maeneo yalioshikiliwa na waasi. Kulingana na shirika la habari la NBC lililopeperusha habari hizo jeshi la Syria linasubiri kupewa amri itakayotoka kwa rais ya kuwapa fursa ya kufanya hivyo.

Wakizungumza na shirika hilo maafisa hao wamesema kwa sasa hakuna ushahidi kwamba kuna mpango wa kuchanganya kemikali mbili ambazo kwa pamoja zinatengeneza gesi ya sarin. Gesi ya Sarin ina uwezo wa kuuwa maelfu ya watu kwa dakika kadhaa iwapo itafunguliwa au kuwekwa katika eneo lililo na idadi kubwa ya watu.

Waziri wa mambo ya nje wa Marekani Hilarry Clinton
Waziri wa mambo ya nje wa Marekani Hilarry ClintonPicha: Reuters

Hata hivyo serikali ya Syria kupitia waziri wake wa mambo ya nje Faisal Mekdad imeishutumu Marekani na ulaya kwa ujumla kwa kutumia swala la silaha za sumu kama kisingizio cha kutaka kuiingilia kijeshi nchi hiyo.

Mapema hapo jana waziri wa mambo ya nje wa Marekani Hillary Clinton alisema Marekani ina wasi wasi kwamba serikali ya Syria ina nia ya kutumia kemikali za sumu katika kuukandamiza upinzani. Clinton alisisitiza wito wa kuwepo kwa kipindi cha mpito wa kisiasa huku akisisitiza kuwa rais Assad aondoke madarakani.

Ujerumani yachangia majeshi

Wakati huo huo baraza la mawaziri la Ujerumani hii leo limeidhinisha mpango wa kutuma mtambo wa kuzuia makombora ya kutoka angani na pia mpango wa majeshi 400 kutumwa nchini Uturuk. Majeshi hayo yatalinda mpaka baina ya nchi hiyo na Syria ili kuzuia mapigano kusambaa nchini humo.

Waziri wa Ulinzi Thomas De Maiziere amesema jeshi hilo litakuwa nchini uturuki kwa muda wa mwaka mmoja.

Waziri wa ulinzi wa Ujerumani Thomas de Maiziere
Waziri wa ulinzi wa Ujerumani Thomas de MaizierePicha: dapd

Uturuki ambaye ni mwanachama wa jeshi la NATO na ambayo imewapa hifadhi wakimbizi wengi kutoka Syria imesema inahitaji mtambo huo wa kuzuia makombora ili kujilinda na mashambulizi ya angani yatakayotokea nchini Syria.

Mwandishi: Amina Abubakar/AFP/dpa/Reuters

Mhariri: Yusuf Saumu