1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Marekani itaendelea kushiriki mazungumzo ya tabianchi

Bruce Amani
7 Novemba 2017

Mkutano wa mabadiliko ya tabia nchi unaendelea mjini Bonn. Wajumbe katika Mkutano huo wa wiki mbili wanajadili kuhusu sheria zitakazotumika ili kuyatekeleza makubaliano ya Paris yaliyofikiwa miaka miwili iliyopita.

https://p.dw.com/p/2nAAP
Deutschland COP23 UN Klimakonferenz in Bonn
Picha: Reuters/W. Rattay

Viongozi wa ngazi ya juu wataanza kuwasili wiki ijayo kwa ajili ya mazungumzo mazito ya siku za mwisho za mkutano huo wa kilele. Lakini tayari wanasiasa wanajiandaa kwa makabiliano kati ya watu wanaodai kuzungumza kwa niaba ya Marekani.

Donald Trump alitangaza mapema mwaka huu kuwa ataiondoa Marekani katika makubaliano ya Paris. Hata hivyo, mchakato wa kujitoa huchukua miaka mitatu maana kuwa Marekani itaendelea kuwa mwanachama hadi wakati huo. Rais Trump anatuma ujumbe mdogo wa wajumbe mjini Bonn ambao utajaribu kuendelea kuyapiga msasa makubaliano hayo.

Jukumu ambalo ujumbe huo unapaswa kutekeleza na kutotekeleza, ni kitu kinachozungumziwa sasa. Kwa mara ya kwanza, Marekani imekuwa nchi ya kwanza kutokuwa na jukwaa lake katika mkutano wa kilele wa mwaka huu wa Umoja wa Mataifa.

COP23 UN Klimakonferenz in Bonn Eröffnung Barbara Hendricks und Gert Müller
Gerd Mueller na Barbara HendricksPicha: Imago/photothek/U. Grabowsky

Naibu mjumbe maalum wa Marekani kuhusu mabadiliko ya tabianchi Trigg Talley amesema Marekani itaendelea kushiriki katika mazungumzo ya kuutekeleza muafaka wa Paris licha ya kitisho cha Trump kuiondoa nchi katika makubaliano hayo. "Rais ameweka wazi kuwa tutaendelea kuzungumza na mataifa kuhusu masuala yanayohusiana na nishati na mabadiliko ya tabianchi na tunategemea kufanya kazi na wenzetu na washirika ili kufanikisha kazi hiyo hapa katika wiki hizi mbili na siku za baadaye".

Lakini muungano wa makundi hasimu ya magavana wa Marekani, mameya na viongozi wa kibiashara, unaojiita "Bado Tuko Ndani”, utafungua jukwaa lake Alhamisi.

Unaongozwa na Gavana wa California Jerry Brown na aliyekuwa Meya wa New York Michael Bloomberg. Waziri wa mazingira wa Ujerumani Barbara Hendricks, ameiambia DW kuwa anaamini ujumbe rasmi wa Marekani unapaswa kushirikishwa. "Kisiasa, kitakachoangaziwa hapa Bonn ni umuhimu kuwa ulimwengu mzima unaendelea kuungana. Msimamo wa Ujerumani ni wazi kwamba makubaliano ya Paris hayajadiliwi upya, na hali ya matumaini ya kisiasa na kiuchumi iko juu mno hata serikali ya Trump haitaweza kuusitisha mwenendo huu".

Wakati huo huo, nchi mbalimbali na taasisi za kifedha zinajiandaa kujaza pengo la mamlaka lililoachwa na Marekani. China inataka kuchukua nafasi hiyo, huku ikiwa na jukwaa kubwa katika mkutano wa kilele wa mwaka huu na kuchukua jukumu la msimamo mkubwa zaidi katika mazungumzo hayo, kwa mujibu wa duru za kidiplomasia. Umoja wa Ulaya pia unaingilia kati kujaza pengo hilo. Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron na Kansela wa Ujerumani Angela Merkel watawasili Bonn wiki ijayo.

Mwandishi: Dave Keating/Bruce Amani
Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman