1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Marekani kupeleka wanajeshi zaidi Afghanistan

P.Martin - AFPE18 Februari 2009

Rais wa Marekani Barack Obama ameidhinisha kupeleka wanajeshi 17,000 ziada nchini Afghanistan.Amesema,vikosi hivyo vinahitajiwa kuleta utulivu Afghanistan ambako hali ya usalama inazidi kuwa mbaya.

https://p.dw.com/p/Gwc6
President Barack Obama gestures during a town hall meeting to discuss the economy, Tuesday, Feb. 10, 2009, at the Harborside Event Center in Fort Myers, Fla. (AP Photo/Charles Dharapak)
Rais wa Marekani Barack Obama.Picha: AP

Wanajeshi hao 17,000 watapelekwa Afghanistan kabla ya uchaguzi mkuu wa Agosti 20 nchini humo.Wanajeshi hao wataimarisha vikosi vya wanajeshi 38,000 wa Kimarekani waliokuwepo Afghanistan kupambana na ugaidi unaoongezeka nchini humo. Rais Obama amesema,ameidhinisha hatua hiyo akitambua kuwa hali inayokutikana Afghanistan na Pakistan inahitaji kushughulikiwa na kuchukuliwa hatua ya dharura.Ni muhimu kutuliza hali inayozidi kuwa mbaya katika nchi iliyokosa kushughulikiwa kimkakati na kwa mwongozo wa dharura unaohitajika.Akaeleza kuwa uamuzi huo umepitishwa kufuatia ombi lililotolewa na Waziri wa Ulinzi Robert Gates kupeleka vikosi ziada kabla ya majira ya joto,ikihofiwa kuwa mashambulizi ya wanamgambo yatashika kasi uchaguzi ukikaribia.

Serikali ya Rais Hamid Karzai nchini Afghanistan inayoungwa mkono na Marekani,inazidi kushinikizwa huku wanamgambo wa Taliban na al-Qaeda wakizidi kuimarika na kuenea kutoka mashariki na kusini mwa nchi hadi sehemu za magharibi na hata ukingoni mwa mji mkuu Kabul.Hali ya usalama ikiwa bora huko Iraq,sasa Marekani inaipa Afghanistan kipaumbele na imepunguza majeshi yake nchini Irak.Obama ameonya kuwa Wataliban wameibuka upya nchini Afghanistan wakisaidiwa na al-Qaeda na hivyo kuhatarisha usalama wa majeshi ya Marekani mpakani na Pakistan.

Rais Obama alipoingia madarakani alitoa amri ya kuchunguzwa upya sera za Marekani katika kanda hiyo ambako uasi unaongezeka hata miaka saba baada ya Marekani kuanzisha vita vyake dhidi ya ugaidi na kuitimua serikali ya Taliban.Seneta John McCain aliekabiliana na Obama mwaka jana katika uchaguzi wa rais,ameunga mkono hatua ya kupeleka vikosi ziada.Wakati huo huo akasema,ni matumaini yake kuwa hiyo ni hatua ya kwanza tu katika utaratibu mpya utakaofuatwa kuhusu Afghanistan.Amesema,wakati umewadia kufuata mkondo mpya.

Kwa upande mwingine,Rais Obama alipozungumza kwa simu na Rais Karzai Jumanne usiku,alimuhakikishia msaada wa Marekani kupambana na ugaidi katika kanda hiyo. Hiyo ilikuwa mara ya kwanza kwa marais hao wawili kuzungumza tangu Obama kuingia madarakani mwezi wa Januari.