1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Marekani na aibu ya mauaji iliyoyafanya dhidi ya Wavietnam miaka 40 iliyopita.

Scholastica Mazula14 Machi 2008

Ni miaka arobaini sasa imepita Marekani bado inaona aibu kufuatia mauaji ya kikatili iliyoyafanya My Lai,kijiji kilichoko Vietnam.

https://p.dw.com/p/DOVO
Wanajeshi wa Kimarekani wakijaribu kukwepa mapigano wakiwa wamembeba mwenzao aliyejeruhiwa katika mapambano wakimpeleka katika helkopta yao wakati wa vita vya Vietnam June 24, 1965.

Kikosi cha wanajeshi wa Kimarekani kilipewa amri kukifyatulia risasi kitu chochote ambacho kilikuwa kinatembea katika kijiji hicho.

Kikosi hicho cha wanajeshi kilipoondoka masaa matatu baadaye kutoka kijiji hicho hapo Machi, 16 mwaka 1969, kijiji cha My Lai kilichoko katika nyanda za juu za huko kusini mwa Vietnam kilifekwa kabisa na hakujabakia kitu chochote kilichokuwa hai.

Maiti za watu zilizokuwa zimetapakaa damu, zilionekana kusambaa kila mahali, wakiwemo wanawake, watoto, wazee na hata mbwa.Moshi kutoka nyumba zilizokuwa zinaungua ulionekana kwa mbali.Miili ya wanawakee vijana ilionesha alama ya kubakwa.

Idadi ya watu waliokufa inakisiwa kuwa ni baina ya mia tatu arobini na saba hadi mia tano na nne, wote hao wakiwa ni wahanga wa kikosi hicho cha Kimarekani kilichopata kichaa kwa kuonja damu.

Hapakufyatuliwa hata risasi moja dhidi ya wanajeshi hao wa Kimarekani.

Ni mwaka mmoja baadaye ndipo Umma wa Kimarekani ulipokuja kujua ukweli wa mambo, baada ya ukweli huo kufichwa kwa muda mrefu na jeshi la Kimarekani.

Wakati huo Novemba 1969, upinzani na malalamiko juu ya vita vilivyokuwa vinaendeshwa na Marekani huko Vietnam ulikuwa mkubwa na siri iliyofichuka juu ya mauaji ya My Lai ilizidisha hasira za watu huko Marekani na duniani kote.

Kwa kizazi kizima cha wamarekani, watu wa ulaya na wa Asia, My Lai ilitoa sura ya Mmarekani aliyekuwa mbaya.

Jarida la kila wiki la Time liliandika pale kisa hicho killipofichuliwa kwamba Marekani na Wamarekani lazima wasimame katika kizimba kikubwa kukiri makosa yao juu ya kile kilichotokea My Lai na kwamba jambo hilo haliepukiki.

Katikam majira ya mapukutiko ya mwaka 1969, mamillioni ya wamarekani kutoka Mashariki hadi Magharibi ya nchi hiyo, wakiwemo laki mbili na nusu katika mji wa Washington, walijiunga katika maandamano makubwa kabisa ya kupinga vita kuwahi kuonekana katika historia ya Marekani.

Lakini ilikuwa miaka sita baadaye hapo April 1975, ndipo Wamarekani walipoukimbia kwa hofu mji wa Saigon huku wakipanda helkopta zao zilizokuwa zikitua katika mapaa ya majumba.

Hivyo dola kuu duniani likalala chini limeshindwa na kudhalilishwa,limeshindwa katika vita vya chini kwa chini, limeshindwa na adui ambaye alikuwa anamiliki teknolojia ndogo zaidi.

Vita vya Vietnam vilivyodumu miaka kumi vilichukua roho za wamarekani hamsini na nane elfu ukilinganisha na roho za watu milioni mbili hadi nne wa Vietnam.

Mtetezi mkubwa wa vita hivyo, ROBERT MC NAMARA; aliyekuwa Waziri wa ulinzi wa Marekani kutoka mwaka 1961 hadi 1968, alielezea huzuni lakini siyo masikitiko kuhusu vita hivyo.

Aliita Karne ya 20 kuwa ni karne iliyojionea kumwagika damu nyingi kabisa katika historia ya mwanadamu.

Akaendelea kusema kwamba ikiwa binadamu wanataka karne ya 21 ijiepushe na mambo kama hayo, basi inawabidi wajifunze kutokana na makosa ya karne iliyopita.

Wakati serikali za Vietnam na Marekani zinakaa pamoja kwenye meza ya mazungumzo, lakini watu wengi walioishi katika asubuhi ile ya tarehe 16, machi mwaka 1968 kamwe hawatalisahau tukio hilo.Baadhi yao wanasema hawawachukii Wamarekani wa kawaida lakini wanayachukia majeshi ya Kimarekaani yaliyofanya ukatili huo.