1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Marekani na Taliban waandika upya mswada wa kuondoa majeshi

Sekione Kitojo
4 Julai 2019

Wajumbe wa majadiliano wa Taliban na Marekani wanakwenda mbio kuandika upya mswada wa makubaliano yatakayoainisha kuondoka  majeshi ya Marekani na NATO kutoka  Afghanistan na uhakikisho wa Taliban kupinga ugaidi.

https://p.dw.com/p/3LYu9
Russland Moskau Afghanistan-Gespräche Mullah Baradar Taliban
Picha: picture-alliance/AA/S. Karacan

Makubaliano hayo  pia  ni  pamoja  na  kupata  uhakikisho  madhubuti wa  Taliban  wa kupambana  na  ugaidi kabla  ya  mkutano wa  amani kwa  ajili  ya makundi  yote  ya  Afghanistan  utakaofanyika  siku  ya Jumapili. 

Afghanistan Herat Taliban Kämpfer
Wapiganaji wa Taliban wakipambana na majeshi ya Marekani nchini AfghanistanPicha: picture-alliance/AP Photo/A. Khan

Maafisa  ambao  wako  karibu  na  majadiliano  hayo, lakini  ambao hawana  mamlaka  ya  kuyazungumzia , wanasema  majadiliano yameingia  katika  nyakati  za  usiku  jana  Jumatano na  wajumbe watarejea  tena  leo  Alhamis  katika  mazungumzo,  hayo  ya  ana kwa  ana  ambayo  yamechukua  siku  sita   kati  ya  wapiganaji hao na  mjumbe  wa  Marekani Zalmay Khalilzad.

Suhail Shaheen, msemaji wa  ofisi  ya  kisiasa  ya  Taliban nchini Qatar , mapema  aliliambia  shirika  la  habari  la  Associated Press kwamba  mswada  wa  makubaliano  unaandikwa  upya  kujumuisha vipengee  vilivyokubaliwa  kwa  pamoja. Pande  hizo  mbili  bado zimegawika  kuhusiana  na  muda wa  kuyaondoa  majeshi, wakati Marekani  inataka  muda  zaidi.

Maafisa  wa  Taliban , ambao  walizungumza  kwa  masharti  ya kutotajwa   majina, wamesema  Marekani  inataka  miezi 18 kukamilisha  kuviondoa  vikosi  vyake vyote  hata  kama  rais  wa Marekani  Donald Trump  amekiambia  kituo  cha  televisheni  cha Fox News  mapema  wiki  hii  kuwa  uondoaji  wa  vikosi  tayari umeanza  kimya  kimya  na  kwamba nguvu  za  vikosi  hivyo imepunguzwa  hadi  wanajeshi 9,000. Taarifa  ya  rais  Trump imekuwa  tangu  wakati  huo  ikikinzana  na  taarifa  za maafisa waandamizi  wa  Marekani,  ambao  wamesema  nguvu  ya  majeshi hayo  haijabadilika  na  iko  katika  jumla  ya  wanajeshi 14,000.

USA Zalmay Khalilzad in Washington
Mjumbe wa Marekani katika Afghanistan Zalmay KhalilzadPicha: picture-alliance/AP Photo/J. Martin

Dhamira ya Trump 

Pamoja  na  hayo, taarifa  ya  Trump  imeimarisha  dhamira  ya  rais huyo  ambayo  mara  kwa  mara  amekuwa  akieleza ya  kujitoa kutoka  Afghanistan na  kufikisha  mwisho  vita  hivyo  vya  Marekani vilivyodumu  kwa  muda  wa  miaka  18, vita  virefu  kabisa  katika historia.

Nia  yake  hiyo  ya  kuondoa  majeshi  imeimarisha   nafasi  ya Taliban ,  kundi  ambalo  linadhibiti  nusu  ya  nchi  na  kupata maridhiano  muhimu  katika  kupanga  mkutano  unaokuja  wa  amani , ambao  hautajumuisha  ujumbe  wowote  rasmi  kutoka  katika serikali  ya  Afghanistan.

Afghanistan | Drohnen | Taliban | Sicherheitskräfte
Majeshi ya serikali ya Afghanistan yakipambana na Taliban kwa kutumia ndege zisizo na rubani Picha: DW/S. Tanha Shokran

Ujerumani  na  Qatar , nchi  ambazo  zinasimamia  kwa  pamoja majadiliano  na  kutoa  mialiko, zimesema  washiriki  "watahudhuria tu , kama wajumbe  binafsi, "  shari  ambalo  rais Ashraf Ghani amelipinga  kwa nguvu kabisa. Hajazungumzia  lolote  kuhusu mkutano  wa  Jumapili.

Taliban wamekataa  kabisa  kuzungumza  na  serikali ya  Ghani, wakiita kibaraka  wa  Marekani, lakini   wamesema  maafisa  wa serikali  wanaweza  kuhudhuria  mkutano  huo  kama  raia  wa kawaida.

Mwandishi: Sekione  Kitojo / ape

Mhariri:  Mohamed Khelef