1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Marekani na Umoja wa Ulaya wamkosoa Raila Odinga

Sylvia Mwehozi
2 Februari 2018

Marekani na Umoja wa Ulaya wamekosoa hatua ya muungano wa upinzani wa NASA nchini Kenya kumuapisha kiongozi wao Raila Odinga, pamoja na hatua ya serikali kuzima matangazo ya vituo vya televisheni.

https://p.dw.com/p/2s1SN
Kenia symbolische Vereidigung Raila Odinga
Picha: picture-alliance/Anadolu Agency/B. Jaybee

Katika taarifa tofauti zilizochapishwa kwenye tovuti zao,Wizara ya mambo ya nje ya Marekani na Umoja wa Ulaya zimeushutumu muungano wa upinzani wa NASA kwa kumuapisha Raila Odinga kuwa kiongozi wa Kenya na kuusisitizia umuhimu wa viongozi wote kuiheshimu katiba ya Kenya na sheria kwa jumla. Kwa upande wake serikali ya Marekani inavikosoa vitendo vyovyote vinanavyokiuka sheria za nchi.

Taarifa ya Umoja wa Ulaya nayo pia imeelezea kuutambua ushindi wa Uhuru Kenyatta kama rais wa Kenya, na imefafanua  kuwa kuheshimu sheria ni sawa na kuheshimu uhuru wa kutangamana, vyombo vya habari na kujieleza. Kwa mantiki hii hatua ya serikali ya kuvibana vituo 3 vya televisheni kurusha matangazo ni kinyume na maadili. Ifahamike kuwa mahakama kuu tayari imeiamuru serikali kuvifungulia vituo hivyo ili viweze kurusha matangazo ila mpaka sasa bado halijatimia.Vituo vilifungiwa jumanne asubuhi.

Kiongozi wa NRM akamatwa

Kenia symbolische Vereidigung für Raila Odinga | Tom Kajwang, Miguna Miguna
Miguna Miguna (kulia)akiwa amehudhuria sherehe za kujiapisha kwa OdingaPicha: picture-alliance/AP Photo/B. Curtis

Kiongozi wa vuguvugu la NRM lenye mafungamano na muungano wa upinzani wa NASA nchini Kenya Miguna Miguna, amekamatwa na polisi mapema hii leo. Miguna aliyejitangaza kuwa kamanda wa NRM alikamatwa asubuhi pale polisi walipomvamia kwake nyumbani mtaani Runda. Kulingana na mkurugenzi wa idara ya upelelezi George Kinoti, Miguna alikamatwa kwa kushiriki kwenye hafla ya kumuapisha Raila Odinga na kuwa mwanachama wa vuguvugu la NRM.

Wizara ya usalama wa taifa ililipiga marufuku vuguvugu la NRM mapema wiki hii.Miguna Miguna aliyewania ugavana wa kaunti ya Nairobi na kushindwa alikiri siku ya alhamis kuwa yeye ndiye aliyesimamia kiapo cha Raila Odinga siku ya jumanne na pia kuwaamuru wafuasi wao kuyaangusha mabango ya rais Uhuru Kenyatta.

Kwa sasa haijulikani kituo cha polisi anakozuiliwa kiongozi huyo wa NRM, Miguna Miguna. Yote hayo yakiendelea mahakama kuu imeusitisha kwa muda uamuzi wa kukifutilia mbali kibali cha kumiliki bunduki cha mbunge wa Dagoretti Kaskazini Simba Arati.Jaji George Odunga aliamuru pia arejeshewe maafisa binafsi wa ulinzi mpaka pale kesi itakaposikilizwa. Hatua ya kutoa Amri ya kumpokonya kibali cha kimiliki bunduki inachukuliwa kama mbinu ya kuwaandama wanasiasa wa chama cha ODM, mmojawapo ya vyama vinavyounda muungano wa upinzani wa NASA.

Kenia Amtseinführung Präsident Kenyatta
Amiri Jeshi mkuu wa Kenya, Uhuru Kenyatta akikagua gwaride Picha: Reuters/T. Mukoya

Uhuru wa waandishi

Katika tukio jengine waandishi 3 wa habari wanashusha pumzi baada ya mahakama kuu kuwazuwia polisi kwa muda kuwakamata kwa mchango wao katika mchakato wa kumuapisha Raila Odinga.Jaji Luka Kimaru alitoa agizo hilo hadi pale kesi dhidi ya Linus Kaikai, Ken Mijungu na Larry Madowo wote wa kampuni ya utangazaji ya Nation Media itakaposikilizwa. Watatu hao wanatarajiwa kufika mbele ya idara ya upelelezi Jumatatu ijayo kuwasaidia wachunguzi kadhalika wamepewa dhamana ya laki moja ya muda kuzuwia kukamatwa.

Mwandishi: Thelma Mwadzaya - DW, Nairobi

Mhariri: Iddi Ssessanga