1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Marekani na Urusi kujadiliana kuhusu sera.

9 Desemba 2007
https://p.dw.com/p/CZGp

Washington. Wizara ya mambo ya kigeni ya Marekani imetangaza kwamba wataalamu wa ngazi ya juu wanaohusika na masuala ya sera kutoka Marekani na Urusi wanatarajiwa kukutana kwa ajili ya mazungumzo ya ushirikiano mjini Budapest Desemba 13. Huku kukiwa na hali ya mvutano kuhusiana na mipango ya Marekani ya kuweka ngao ya ulinzi dhidi ya makombora katika eneo la bara la Ulaya, wajumbe wa majadiliano wa Marekani watajadili mapendekezo ya ushirikiano baina ya nchi hizo mbili kuhusiana na makombora na rada ili kuweza kwa pamoja kuchunguza kitisho cha makombora kutoka mashariki ya kati. Licha ya tathmini mpya ya Marekani ambayo inapunguza kitisho cha kinuklia kutoka Iran, Marekani inaendelea na mpango wake wa ulinzi dhidi ya makombora katika maeneo ya jamhuri ya Chek na Poland. Maafisa wa Marekani wamesema kuwa mipango hiyo ni muhimu kuweza kulinda washirika wake katika bara la Ulaya kutokana na uwezekano wa mashambulio kutoka katika mataifa yenye kiburi , hususan Iran.

Wakati huo huo balozi wa zamani wa Marekani katika umoja wa mataifa ameishutumu ripoti inayohusu mpango wa kinuklia wa Iran, iliyotolewa na mashirika ya ujasusi ya nchi hiyo wiki hii. Kwa mujibu wa ripoti katika gazeti la Der Spiegel nchini Ujerumani , John Bolton amesema taarifa hiyo ilikuwa ni ya siasa chini ya kivuli cha ujasusi. Tathmini ya mashirika ya ujasusi ya Marekani inasema kuwa Iran ilisitisha kuendeleza mpango wa silaha za kinuklia miaka minne iliyopita. Waziri wa mambo ya kigeni wa Iran Manouchehr Mottaki amesema jana Jumamosi kuwa ugunduzi huo katika ripoti hiyo ulikuwa kutokana na shughuli za ujasusi pamoja na satalaiti zilizofanywa na mashirika ya ujasusi ya Marekani, na kwamba barua rasmi ya kupinga kitendo hicho imetumwa kwa serikali ya Marekani.