1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Marekani na Urusi zimetia saini mkataba wa START

8 Aprili 2010

Rais Obama na Dmitry Medvedev wameionya Iran kuhusiana na mpango wake wa Kinuklia

https://p.dw.com/p/Mqbd
Rais Barack Obama na mwenzake Dmitry Medvedev katika kasri la mjini Prague baada ya kusaini mkataba wa STARTPicha: AP

Marekani na Urusi zimesaini mkataba wa kihistoria wa kupunguza silaha za kinyukliya, ambao umetajwa na viongozi wa pande zote mbili kuwa ni kitendo kitakachoimarisha usalama kote ulimwenguni. Rais wa Marekani, Barack Obama, na Dmitry Medvedev wa Urusi baada ya kutia saini mkataba huo huko Prague unaofahamika kama START wamesema hatua ya kuiwekea vikwazo vipya Iran huenda ikahitajika ili kuishinikiza jamhuri hiyo ya kiislamu kuachana na mpango wake wa Kinyuklia.

Viongozi wa Marekani na Urusi wamesaini makuliano ya kihistoria ya kimkakati ya kupunguza silaha za nyuklia na kusema kwamba hatua ya kuiwekea vikwazo vipya Iran ni muhimu ili kuitia shinikizo nchi hiyo iachane na shughuli zake za nyuklia. Rais Barack Obama na mwenzake wa Urusi, Dmitry Medvedev, wametia saini mkataba huo wa Start katika sherehe maalum iliyofanyika kwenye kasri la Mediaeval, mjini Prague, baada ya kufanya mazungumzo ya kina kuhusiana na masuala mbali mbali, tangu usalama wa nyuklia, mpango wa nyuklia wa Iran hadi suala la mzozo wa Kyrgyzstan ambako nchi zote mbili, Urusi na Marekani, zimeweka vituo vyao vya kijeshi. Akizungumza baada ya kutia saini mkataba huo, rais Obama alisema kwamba kuzuia kuenea kwa silaha za maangamizi makubwa ni hatua itakayochangia katika kuziimarisha tawala zisizokuwa na silaha hizo, na pia kuifanya Marekani na ulimwengu mzima, kwa jumla, kuwa mahala pa salama na amani,aliongeza kusema

START-Abkommen
Rais Barack Obama, katikati akitembea pamoja na rais wa jamhuri ya Czech Vaclav Klaus, kushoto alipowasili katika kasri la PraguePicha: AP

''Ikiwa Marekani na Urussi zinashindwa kushirikiana katika masuala muhimu sio jambo zuri kwa nchi zetu na wala sio kitu kizuri pia kwa ulimwengu mzima, kwa jumla. Sote tumeondoa pengo hilo na kuthibitisha juu ya faida za ushirikiano wetu. Hatua ya leo ni muhimu na ya kihistoria katika suala la usalama wa nyuklia pamoja na upunguzaji wa silaha hizo na pia katika ushirikiano kati ya Marekani na Urussi.''

Russisches Atom U-Boot
Marekani na Urusi zitapunguza kila mmoja kiasi silaha 1550 za Kinuklia ikiwa ni pamoja na mitambo ya kufyatua makomboraPicha: picture alliance/dpa

Urusi, kwa upande wake, imesema kwamba inaweza kujiondoa katika mkataba huo mpya ikiwa itahisi inapewa kitisho na mpango wa Marekani wa kuweka makombora ya ulinzi katika Ulaya ya Mashariki.Ikulu ya Kremlin imesisitiza hii leo kwamba mkataba huo wa Start utadumu ikiwa tu Marekani itapunguza makombora yake ya ulinzi. Hata hivyo, baada ya kutia saini mkataba huo, rais Dmitry Medvedev ametoa ishara kwamba ni mkataba utakaozifaidisha nchi zote mbili akisema-

''Kilichomuhimu zaidi ni kwamba ni hali inayotoa ushindi katika pande zote. Hakuna atakayepoteza katika mkataba huu. Naamini kwamba mkataba huu unaonyesha hali halisi ya ushirikiano wetu. Pande zote mbili zimepata ushindi na tukizingatia ushindi huo ni kwamba ulimwengu mzima umeshinda.''

Ushindi kwa ulimwengu mzima, lakini sio kwa serikali ya Iran, hiyo ndio picha iliyojitokeza baada ya kusainiwa kwa START, kufuatia matamshi ya rais Obama kwamba

''Silaha za nyuklia sio tu ni suala la Marekani na Urusi. Zinatishia usalama wa nchi zote, kwa jumla. Silaha za nyuklia katika mikono ya magaidi ni hatari kwa watu wote kote duniani kuanzia Moscow hadi NewYork, kuanzia kwenye miji ya Ulaya hadi kusini mwa Asia.''

Rais Medvedv, kwa upande wake, amesema anasikitika kwamba Tehran haijakubaliana na mapendekezo ya Umoja wa mataifa, na hivyo basi kuna uwezekano Baraza la Usalama la Umoja huo likachukua hatua ya kuiwekea vikwazo zaidi nchi hiyo.Leo hii pia Obama atakutana na viongozi 11 kutoka nchi za Ulaya mashariki na kati katika juhudi za Marekani za kutafuta ushirikiano zaidi katika eneo hilo.

Mwandishi Saumu Mwasimba/ AFPE

Mhariri Othman Miraji