1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Marekani: Timu ya Trump ina mashaka naye ofisini

John Juma
5 Januari 2018

Rais wa Marekani Donald Trump amejipata katika mzozo mwingine baada ya kuchapishwa kitabu kinachomuangazia kama mtu asiye na uwezo wa kuongoza na pia mtu mwenye kiburi

https://p.dw.com/p/2qPa0
Donald Trump in Palm Beach
Picha: Apicture-alliance/AP Photo/C. Kaster

Rais wa Marekani Donald Trump amejipata katika mzozo mwingine baada ya kuchapishwa kitabu kinachomuangazia kama mtu asiye na uwezo wa kuongoza na pia mtu mwenye kiburi. Hii ni baada ya mawakili wake kushindwa kuzuia kitabu hicho kuruhusiwa kuuzwa. Hayo yakijiri, Rais Trump amepanga kukutana na viongozi wa chama cha Republic.

Wakiijibu barua ya Trump ya kuwataka wasikiruhusu kitabu hicho kuuzwa, wachapishaji wa kitabu hicho chenye kichwa "Fire and Fury: Inside the Trump White House", wameamua kukiruhusu kitabu hicho kuuzwa siku nne kabla ya siku iliyoratibiwa kuzinduliwa.

Kitabu hicho cha kiufichuzi kilichoandikwa na mwandishi wa kisiasa Michael Wolff kinawanukuu baadhi ya washirika wa Trump, wakielezea mashaka yao makubwa kuhusu uwezo wa Trump ofisini. Wolf amejitetea akisema asilimia 100 ya watu wote walio karibu na Trump wana mashaka na uwezo wake kuwa ofisini. Akihojiwa katika kituo cha televisheni, ambapo aliulizwa mifano ya jinsi watu walioko karibu na Trump walivyomuelezea, Wolff alijibu:

Michael Wolff, mwandishi wa kitabu Fire and Fury: Inside the Trump White House"
Michael Wolff, mwandishi wa kitabu Fire and Fury: Inside the Trump White House" Picha: Reuters/B. McDermid

Watu wa karibu na Trump wanamfananisha na mtoto-Wolff

"Nitakuambia mfano mmoja ambao kila mmoja alitoa, na unafanana kwa kila mmoja. Wote walisema Trump ni kama mtoto. Na wanachomaanisha ni kwamba ana tamaa ya kujitosheleza kwanza. Yeye pekee."

Kitabu hicho pia kimejumuisha nukuu nyingi kutoka kwa aliyekuwa mkuu wa mikakati wa Trump Steve Bannon, ambaye pia alipokea ujumbe kutoka kwa mawakili wa Trump kukoma kabisa kujihusisha au kukiruhusu kitabu hicho sokoni.

Katika baadhi ya sehemu za kitabu hicho zilizochapishwa wiki hii, Bannon amenukuliwa akimlaumu mwana wa kwanza wa Trump Donald Trump Jr kwa mahusiano ya kihaini kati yake na wakili anayehusishwa na Urusi.

Ikulu ya Marekani imekipuuza kitabu hicho, mtungaji wake na vyanzo vyake.

Katika ukurasa wake wa Twitter, Rais Trump aliandika hakumruhusu hata kidogo aliyekitunga kitabu hicho kuzuru ikulu wala hakuzungumza naye kuhusu kitabu, na hivyo yote aliyoyaandika ni potovu na uwongo mtupu.

Jalada la kitabu "Fire and Fury"
Jalada la kitabu "Fire and Fury"Picha: Henry Holt and Co.

Akipinga madai kwamba aliyoyasema kitabuni ni uongo, Michael Wolff amesema alikuwa na Trump kwa muda wa saa tatu wakati wa kampeni za urais kando na kuzungumza na wapambe wake wanaozungumza naye kila siku.

Trump kukutana na Warepublicans

Hayo yakijiri, Rais Trump anatarajiwa kukutana na wakuu wa chama cha Republic kwa siku mbili miongoni mwao spika Paul Ryan na kiongozi wa wengi katika seneti Mitch McConnel, kupanga vipaumbele vya  bungeni katika mwaka huu, na pia kujadili mkakati muhimu wa uchaguzi wa wabunge na maseneta utakaofanyika Novemba.

Trump alipata ushindi wa kwanza bungeni mwezi Disemba pale mswada wa kodi ulipopitishwa. Anadhamiria kupata ushindi zaidi kama huo na White House imelenga sera kuhusu miundo mbinu, na mageuzi katika ustawi wa jamii kama vipaumbele. Mswada wa uhamiaji hususan mpango wa kuwasaidia watu waliopelekwa Marekani kinyume cha sheria kama watoto pia ni miongoni mwa ajenda.

Mwandishi: John Juma/RTRE/AFPE

Mhariri: Gakuba, Daniel